MAKATIBU WAKUU SEKTA YA UVUVI NA UKUZAJI VIUMBE MAJI WA EAC WAKUTANA ARUSHA


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kawaida wa Sita wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji katika Ziwa Victoria la EAC kwa Ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Arusha.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Mhandisi Abdillah Mataka akifuatilia Mkutano.


Kamishna wa Uvuvi katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Uganda Bi. Daisy Olyel Aciro akikabidhi Uenyekiti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mazingira, Kilimo na Mifugo Bw. Emmanuel Niyungeko wa Burundi kwenye Mkutano wa Kawaida wa Sita wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji katika Ziwa Victoria la EAC kwa Ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Arusha.

 Picha ya pamoja

MKUTANO wa Kawaida wa Sita wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji katika Ziwa Victoria la Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ngazi ya Makatibu Wakuu umefanyika leo tarehe 30 Mei 2024 jijini Arusha.

Mkutano huo ulio ongozwa na Mwenyekiti wake Bi. Daisy Olyel Aciro ambaye pia ni Kamishna wa Uvuvi katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Uganda, umepokea na kujadili taarifa ya kikao cha Wataalam kilichofanyika kuanzia tarehe 27 hadi 29 Mei 2024, ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa Mawaziri wa Sekta hiyo utakaofanyika terehe 31 Mei 2024 jijini Arusha.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo Bi. Aciro ameeleza kuwa rasilimali za samaki na viumbe maji vimeendelea kuwa tegemeo kubwa la kiuchumi na chakula kwa wananchi wengi katika ukanda Afrika Mashariki, hivyo juhudi kubwa zinahitajika kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kustawi.

Aliongeza kusema Baraza hilo kupitia Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo kuweka mifumo ya usimazi endelevu wa rasilimali samaki na viumbe maji, mifumo ya uhifadhi na ufuatiliaji ili kuongeza tija zaidi.

Vilevile Bi. Aciro ametoa wito kwa LVFO kuendelea kutumia fursa na nafasi iliyonayo kutafuta rasilimali fedha kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuweza kutekeleza miradi mipya inayoibuliwa kwa manufaa ya Jumuiya.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe ambaye pia aliongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo, amehimiza kuhusu umuhimu wa Jumuiya na wadau kuendelea kuunganisha nguvu na kushirikiana katika kuendeleza rasilimali samaki na viumbe maji kufuatia mchango mkubwa wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa Jumuiya.

Katika Mkutano huo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imewakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Mhandisi Abdillah Mataka.

Katika hatua nyingine Uganda imekabidhi Uenyekiti wa Baraza hilo kwa Jamhuri ya Burundi ambayo itashika nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Related Posts