Makonda kumtesa Samia kama ilivyokuwa Mwinyi na Mrema

RAIS Samia Suluhu Hassan, yuko hatarini kutumbukia katika shimo alilopitia aliyekuwa rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi. MwanaHALISI limeelezwa. Anaripoti Saleh Mohammed … (endelea).

Kiongozi huyo wa nchi aweza kutumbukia shimoni, ikiwa ataendelea kunyamazia; na au kubariki, hatua ya mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kutumia shida za wananchi, “kujinufaisha binafsi.”

Mwinyi alitumbukia katika shimo la kisiasa, wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, pale alipomruhusu Augustine Mrema, “kutumia matatizo ya wananchi, kujinufaisha binafsi kisiasa.”

Mrema aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, katika serikali ya Mwinyi, alijipa mamlaka ya kushughulikia watu na migogoro, iliyokuwa ikitikisa nchi na kujigeuza kuwa mwarobaini wa matatizo hayo.

Augustine Mrema

Mwenendo na utendaji wa Makonda, unatajwa na wachambuzi wa mambo, kwamba unamuweka kwenye wakati mgumu Rais Samia na chama chake (CCM), kama ilivyokuwa wakati wa Mwinyi na Mrema.

Chini ya utawala wa Mwinyi, mwanasiasa huyo aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani na naibu waziri mkuu, aliingilia utendaji wa kila wizara, hali iliyosababisha mvurugano ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika kitabu chake, “Safari ya Maisha Yangu,” rais huyo mstaafu anaeleza majuto yake, kufuatia uamuzi wake wa kumnyamazia Mrema kufanya kazi zisizomhusu.

“Waswahili husema, unadhani umepata kumbe umepatikana,” anaeleza rais Mwinyi na kuongeza, “Niliukumbuka msemo huo, miezi kadhaa baada ya kumteua Mrema kuwa naibu waziri mkuu. Huo ni uamuzi ambao baadae nilikuja kuujutia sana.”

Mwinyi anasema, Mrema aligeuka mwiba kwa chama chake na kwamba kama siyo jitihada za Mwalimu Julius Nyerere, kumnadi Benjamin Mkapa, katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, chama chake kingeanguka.

Katika uchaguzi huo, uliohusisha vyama vingine vya siasa, Mrema alitangaza kukihama CCM na kujiunga na NCCR- Mageuzi, kilichomfanya kuwa mgombea wake wa urais.

Katika uchaguzi huo, Mrema alipata asilimia 27.7 ya kura zote za urais, mbele ya Mkapa aliyepata asilimia 61.8 ya kura hizo.

Mrema kama alivyo Makonda, alikuwa akitoa amri kwa watu mbalimbali au viongozi kufika mbele yake, kabla au baada ya kusikiliza anachoita, “shida za wananchi,” na wakati mwingine kutoa uamuzi wa jambo hilo, bila kujali sheria za nchi.

“Mrema alianza utaratibu wa kupita kwenye ofisi za serikali ikiwemo wizara, kukagua vitu mbalimbali kama mahudhurio ya wafanyakazi. Baadhi ya mawaziri walimkatalia kwa kuwa cheo cha naibu waziri mkuu, hakitambuliki kikatiba. Cleopa Msuya na Joseph Warioba walimkatalia,” anaeleza Mwinyi.

Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi

Anasema, “nilianza kutambua kuwa Mrema anavuka mipaka na juhudi za kumdhibiti hazikufanikiwa. Nikawa sina njia; ila ni kufanya mabadiliko kwenye baraza la mawaziri. Mwaka 1994, nikamtoa katika wizara ya mambo ya ndani na kuondoa cheo cha naibu waziri mkuu.”

Kupitia mabadiliko hayo ya baraza la mawaziri, rais Mwinyi alimteua Mrema kuwa waziri wa kazi, “jambo ambalo lilimkera sana na akazua visa kimoja baada ya kingine.”

Anaongeza, “ilipofika mwaka 1995 aliona wazi kuwa hakuna uwezekano wa kugombea urais kupitia CCM. Akaamua kujiuzulu uwaziri na baada ya mwezi mmoja akahamia NCCR Mageuzi kilichokuwa kinaongozwa na Mabere Marando,” anaeleza Mwinyi.

Makonda alikuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi. Aliondolewa kwenye wadhifa huo aliokuwa anaupenda, baada ya kusuguana na baadhi ya mawaziri na kuudhihaki mhimili wa mahakama.

Mwanasiasa huyo anatumia uzembe, uvivu, ulaji rushwa wa baadhi ya watendaji ndani ya serikali na chama tawala kujijenga kisiasa, huku Rais Samia, akionekana kutenda kazi zake, mithili ya rais Mwinyi na Mrema.

Akiwa katibu mwenezi, tarehe 1 Novemba 2023, Makonda alimpa Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, miezi sita kushughulikia kero za ardhi zinazowakabili wananchi. Alitoa agizo hilo, akiwa katika ziara zake mkoani Dodoma.

Akawataka mawaziri wapeleke ofisini kwake, ripoti ya kazi zao, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa chama hicho. Utaratibu wa CCM kutumia vikao vyake vya Kamati Kuu (CC) na NEC, kujadili na kushauri namna bora ya kuendesha serikali.

MwanaHALISI limeelezwa kuwa tangu kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, tarehe 31 Machi 2024, Makonda ameibua misuguano kadhaa ndani na nje ya CCM juu ya matendo yake yanayokiumiza chama hicho.

Miongoni mwa matendo yaliyofanywa na Makonda na ambayo yanatajwa kuwa yanakiumiza CCM, ni pamoja na kukusanya mamia ya wananchi kwa madai ya kusikiliza shida zao, huku akishindwa kuzitatua kikamilifu.

Aidha, Makonda amekuwa akitajwa kujihusisha na masuala ambayo yako kwenye vyombo vya kisheria na wakati mwingine kutoa maagizo yanayokwenda kinyume na taratibu za utawala bora.

Mathalani, Makonda amewatuhumu hadharani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Juma Hamsini, akidai amefanya ubadhirifu wa fedha za umma na Lines Sanga – meneja Tarura mkoa wa Arusha, kuwa mtu asiyestahili kushika wadhifa huo.

Katika kutekeleza kazi hizi, Makonda amekuwa akizunguka na waandishi wa habari kwa lengo la kujijenga, huku akijinasibu kutatua matatizo ya wanyonge.

“Kuna wakuu wa mikoa wengi wanafanya kazi vizuri tena wanatembelea kata kwa kata. Wanasikiliza wananchi na kutatua matatizo yao. Lakini hawatumii kamera mara kwa mara. Anachokifanya huyu, siyo kutatua shida za masikini, bali kutafuta umaarufu wa kisiasa,” anaeleza.

Naye aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema, wananchi wana uelewa mpana na wanajua matatizo yao yamesababishwa na serikali ya CCM, kwa hiyo anachokifanya Makonda, kinawasaidia kuwaumbua.

“Hizi ngonjera anazofanya Makonda zinasaidia sana kuianika CCM na serikali yake. Ni jambo la hatari kugeuza ofisi ya umma kuwa ya usalama wa taifa, polisi na mahakama. Akiachwa kuendelea, ataumiza wengi. Ataonekana anawaonea huruma wananchi, lakini atakuwa anaumiza wengine wengi,” anasema Lema.

Alisema, mifumo ya utawala wetu inasababisha haki kuchelewa kutendeka kwenye vyombo vya sheria, hivyo tusipokuwa makini tutajikuta tunaumiza watu wasio na hatia.

Alisema, “…hakuna kesi ya siku moja, inayosikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi wa upande mmoja, kisha ukasema unatatua matatizo ya wananchi. Hakuna kitu kama hicho.

“Yaani mtu anakwenda kusema mumewe amemuacha na mtoto na hampi matumizi, halafu Makonda anatoa agizo mhusika akamatwe. Hizi ni kesi za kifamilia hazipaswi kutatuliwa hadharani mbele ya kamera na hiyo siyo kazi ya mkuu wa mkoa.”

Anaongeza: Makonda alifanya haya haya wakati akiwa mwenezi, sasa wenzake wanasafisha alivyoharibu. Serikali itengeneze mifumo bora ya kutoa haki badala ya kuacha mtu mmoja, kukusanya wananchi, kupiga nao picha na kuzionyesha kwa jamii kuwa unatatua matatizo yao.”

Mkazi wa Ngarenaro mkoani Arusha, Said Mkondya, anasema anachokifanya Makonda ni hadaa na kusaka huruma ya wananchi, kwa kuwa matatizo yote yamesababishwa na CCM na serikali yake.

Related Posts