Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amekutana na Waziri wa Ulinzi wa China Dong Jun hii leo, wakati wa mazungumzo ya Shangri-La nchini Singapore.
Katika miaka ya hivi karibuni, kongamano hilo ambalo hufanyika kila mwaka limekuwa kipimo cha uhusiano kati ya Marekani na China. Wakuu wa ulinzi kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni wanahudhuria.
Soma pia: Zelenskiy atoa wito kwa Biden na Xi kushiriki mkutano wa amani
Mataifa hayo mawili yataanza tena mawasiliano ya kijeshi “katika miezi ijayo”. Haya ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Marekani. Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amekaribisha mipango ya kuunda “jopo kazi litakaloshughulikia mgogoro na mawasiliano” pamoja na China, ifikapo mwishoni mwa mwaka.
Austin ameonyesha wasiwasi wake kuhusu shughuli za kijeshi za China karibu na Taiwan, akiongeza kuwa China haipaswi kutumia hali ya mpito wa kisiasa wa Taiwan, ambayo ni “sehemu ya mchakato wa kawaida wa kidemokrasia,” kama kisingizio cha “kuchukua hatua za kulazimisha.”
Aidha kupitia taarifa hiyo, Marekani imesisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru wa usafiri wa baharini katika Bahari ya China Kusini.
Kwa upande wake, msemaji wa Wizara ya ulinzi wa China Wu Qian, amesema “wakati wa mkutano, wakuu hao wawili wa ulinzi walibadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na uhusiano wa kijeshi kati ya China na Marekani, suala la Taiwan, suala la Bahari ya China Kusini, mgogoro wa Ukraine, na mzozo wa Palestina na Israel.”
Ameyaita mazungumzo hayo kuwa “chanya, ya kimkakati na yanayoweza kutekelezeka. Akieleza kuwa huu ulikuwa ni mfano mzuri na wa vitendo.
Masuala tata barani Asia yaibuliwa kwenye mkutano huo
Msemaji huyo amewaambia waandishi wa habari kuwa, katika mkutano huo, Dong Jun wa China amemuambia Austin kwamba hatua za Marekani kuhusu Taiwan zimekiuka sana kanuni ya China Moja.
Dong ameendelea kusema kuwa ingawa China imejitolea kusuluhisha hali ya kutoelewana kati yake na Ufilipino kwenye Bahari ya China Kusini lakini, uvumilivu wake dhidi ya uchochezi una kikomo.
Akigusia mzozo wa Ukraine, Dong amemueleza Austin kwamba China inashikilia “msimamo usio na upendeleo.”
Msemaji huyo amesema, “wameheshimu ahadi yao ya kutotoa silaha kwa upande wowote wa mzozo. Wametekeleza udhibiti mkali wa usafirishaji wa bidhaa za kijeshi kuambatana na sheria na kanuni”.
Dong pia ametoa wito kwa mwenzake wa Marekani kusaidia kuleta amani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Macho yote yanaelekezwa kwa mawaziri hao wanaofanya mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana tangu mwaka 2022.
Soma pia: Xi: China na Marekani zapaswa kuwa washirika, sio washindani
Mkutano huo unatoa matumaini kwa mazungumzo zaidi ya kijeshi kuhusu masuala yenye utata kati ya mataifa yenye nguvu zaidi ulimwenguni.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amepangiwa kutoa hotuba katika kongamano hilo siku ya Jumamosi huku Waziri wa Ulinzi wa China Dong Jun akitarajiwa kuhutubia siku ya Jumapili.