Mke mbaroni kwa mauaji ya mumewe, ni baada ya penzi la bodaboda kukolea

JESHI la Polisi mkoani Songwe linamshikilia mwanamke mmoja anayedaiwa kushirikiana kula njama na hawara yake ambaye ni dereva bodaboda, kumuua mumewe ili wapate uhuru kustawisha penzi lao la wizi. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe… (endelea).

Mbali na mwanamke huyo ambaye ni mtumishi Idara ya afya, mkoani Songwe, pia jeshi la polisi linamshikilia dereva bodaboda huyo kwa ajili ya upelelezi wa mauaji hayo.

Kamanda wa polisi mkoani Songwe, Augustino Senga.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 31 Mei 2024 mjini Songwe, Kamanda wa polisi mkoani humo, Augustino Senga amesema marehemu Victor Mwakapenda (41) mkazi wa Mtaa wa  Ilembo alikutwa ameuawa na watu wasiofahamika na mwili wake kutupwa kwenye pori la Mpoloto – Mbeya vijijini.

Kamanda Senga amesema Mwakapenda ambaye alikuwa anaishi na mkewe huyo, alitoweka nyumbani kwake tangu tarehe 30 Aprili mwaka huu hatimaye mwili wake uliokotwa tarehe 9 Mei mwaka huu katika msitu huo Mpoloto uliopo katika kijiji cha Igale wilaya ya Mbeya vijijini.

Mwili huo uliofanyiwa uchunguzi, ulibainika kuwa na majeraha usoni, kichwani na maeneo mbalimbali ya mwili.

Amesema mwili huo ulipelekwa katika hospitali ya Ifisi jijini Mbeya na kuuhifadhi mpaka ndugu zake walipoutambua tarehe 29 Mei mwaka huu na kukabidhiwa kwa ajili ya mazishi ambayo yamefanyika katika kijiji cha Isongole wilayani Ileje mkoani Songwe.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Senga amesema mbali na wawili hao, jeshi hilo linaendelea  kuwasaka watuhumiwa wengine kuhusika na tukio hilo.

“Ni kweli tunawashikilia watu wawili ambao inadaiwa walikuwa na mahusiano na siku ambayo marehemu alitoweka, dereva bodaboda ndiye aliyekuwa amembeba marehemu na mkewe akiwapeleka kwa mganga,” amesema Kamanda Senga.

Akitaja chanzo cha mauaji hao, Kamanda Senga amesema mwanamke alimueleza mumewe waende kwa mganga wa kienyeji ili wakanywe dawa.

“Wakiwa njiani katika maeneo ya Senjele walitokea watu wawili wasiofahamika ambao walisimamisha pikipiki hiyo na kumchukua mwanaume huyo huku wakmueleza mwanamke huyo na dereva bodaboda warudi walikotoka ndipo walipotoweka na mume huyo.

“Wakiwa njiani mwanaume huyo, alikuwa na hofu kuwa huenda anakoenda hakuna usalama ilibidi awaandikie meseji watu wake wa karibu akiiandika namba ya pikipiki hali iliyorahisisha kukamatwa kwao,” amesema.

Mwili wa Victor Mwakapenda ukihifadhiwa kwenye nyumba yake ya milele.

Ameongeza kuwa watu hao wa karibu ndiyo waliopeleka malalamiko na kuonesha meseji polisi na kuanza kumsaka dereva bodaboda na kumkamata pamoja na mwanamke huyo ambaye ni mtumishi wa serikali idara ya afya.

”Tumewashikilia watu hawa mwawili na bado tunaendelea kuwasaka wauaji kwa sababu vitendo hivi havikubaliki ndani ya jamii hivyo jeshi la polisi halitasita kuwakamata watu wanaovunja sheria kwa kutoa uhai wa watu wengine kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kimapenzi,’ ‘amesema.

Akizungumza na MwanaHALISI katika maziko hayo, Balozi wa Shina namba moja mtaani hapo, Aliki Songa alipokuwa anaishi marehemu, naye amesema kifo hicho cha jirani yake kinahusishwa na wivu wa mapenzi kati ya marehemu na mkewe aliyekuwa anachepuka.

Hata hivyo baadhi ya majirani wa wanandoa hao, wamesema mwanamke alionyesha kumchoka mumewe hadi kufikia hatua ya kutafuta hawara (kibenteni) na mapenzi yalivyozidi kunoga wakafikia hatua ya kupanga njama hizo mbovu za kumuua mumewe huyo.

Akizungumza msibani kwa majonzi, kaka wa marehemu Mwakapenda amesema kifo cha mdogo wake hakivumiliki na kama mdogo wake alikuwa na ugomvi angemfikishwa kwenye vyombo vya sheria kuliko kumuua kinyama. wahusika.

Related Posts