KIUNGO wa Yanga, Jonas Mkude, ni miongoni mwa wachezaji wa kikosi hicho wanaofanya mazoezi kuelekea fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Azam utakaochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani hapa.
Mkude alikosekana ndani ya kikosi cha Yanga kwa muda wa takribani wiki mbili baada ya kutokuwa vizuri kiafya.
Daktari wa Yanga, Moses Etutu, amesema kwa sasa wachezaji wote wanafanya mazoezi baada ya kikosi hicho kufika Zanzibar.
“Kwa ujumla wachezaji wote hali zao kiafya ni wazima, tumekuwa na wachezaji wawili mpaka wanne ambao walikuwa na shida kidogo kama kuumwa malaria na homa akiwemo Jonas Mkude lakini wameanza mazoezi vizuri,” alisema Etutu na kuongeza.
“Hali ya hewa hapa ni upepo na kibaridi kidogo kulinganisha na Dar es Salaam, lakini sidhani kama hali hii itabadilisha mabadiliko ya kimwili kwa wachezaji, pengine inaweza kutusaidia kupunguza uchovu na kuwafanya wachezaji wasichoke mapema, hivyo ni hali ya hewa nzuri na haina madhara kwa wachezaji.”