Mstaafu anapokuwa ombaomba kwenye nchi aliyoijenga mwenyewe

Inasikitisha sana huyu mstaafu anapoishia kuwa ombaomba kwenye nchi yake hii aliyoipatia uhuru na akaijenga kwa jasho na damu yake.

Nchi ambayo alikubali mshahara wake kukatwa Paye (Lipia Kadri Unavyolipwa) kwa miaka 40 ya ajira yake ili nchi iweze kujenga shule na watoto wa nchi wasome bure hadi kufikia kuwa wawakilishi wetu wa kuweza kujipangia kupokea mshahara wa Sh14 milioni kwa mwezi wakati yeye akiishia kupokea  pensheni ya Sh100,000 kwa mwezi!

Ni zaidi ya kusikitisha. Ni aibu ambayo inashangaza sana kwamba waheshimiwa na wawakilishi wa wananchi wanajifanya hawaioni lakini wanaiona.

Aibu ya kwamba huyu mstaafu ambaye aliijenga nchi mpaka pa kuwawezesha waheshimiwa na wawakilishi kujilipa Sh14 milioni kwa mwezi wakati mstaafu aliyeiwezesha nchi kulipa mshahara wa namna hiyo anapostaafu anaishia kulipwa Sh100, 000 tu kama pensheni yake ya mwezi, kwa miaka 19!

Kwa hakika, waheshimiwa na wawakilishi hawa wanapaswa kufikiri tu kwamba hawa wastaafu walioipokea nchi na kuijenga wangepata akili kama yao ya kujijengea ufalme na kujilipa mshahara wa Sh14 milioni kwa mwezi kama wao, nchi hii ingeishafilisika zamani na wao wangeishia kukuta ukoko tu kwenye sufuria iiyotumika kupikia keki ya Taifa, ambayo sasa inaliwa na waheshimiwa na wawakilishi wa wananchi tu na siyo wananchi wenyewe!

Wastaafu wameishia kuwa ombaomba kweli. Kwa miaka 19 sasa wamekuwa wakiomba nyongeza ya pensheni yao ya ‘Laki si Pesa’ kwa mwezi ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha, kama wengine wote walivyowezeshwa, lakini hakuna mheshimiwa wala mwakilishi yeyote anayeliona hilo kama linamhusu. Bidii yao yote iko kwenye kujifanya kukataa kikokotoo ambacho kwa vile hakiwagusi kwenye mafao yao, ni ‘drama’ tu na ndiyo maana kikokotoo kinasonga mbele.

Ndiyo, kwa miaka 10 kidogo mstaafu amekuwa akiomba yale maneno ‘matibabu ya bure kwa wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60’ yageuzwe kuwa kweli na yasiishie kwenye kanga tu, tena za rejekti, kwa vile yanasababisha pensheni yao njiwa ya ‘Laki si Pesa’ ichape yebo mapema inapolazimika kununua kifurushi cha ‘Bima ya Afya’ kilichopaswa kutolewa bure na Siri-kali, lakini wahusika wameuchuna tu na kuweka nta masikioni. Haliwahusu, kama vile hawatastaafu wala kuzeeka!

Labda ni kwa kuwa ‘Bima ya Afya’ ya waheshimiwa na wawakilishi wetu inawawezesha kwenda Mumbai, Ujerumani au Uingereza kutibu hata mafua tu! Ingekuwa nao wanapaswa kwenda Amana, Bombo au Bungado, kikokotoo kingeishachapa lapa na wastaafu wangekuwa wanafaidika na matibabu ya bure kwa wazee wa Taifa. Ni bahati mbaya sana kwamba imekuwa ‘mwanambuzi kamba ni yake’.

Mstaafu wetu anajikuta akishangaa mno wawakilishi wetu wanaposimama na kukemea kwa ukali kuhusu kikokotoo ambacho hakihusishwi kwenye Sh14 milioni zao wala kwenye mafao yao, lakini hakuna, rudia tena kwa msisisitizo, hakuna hata mwakilishi mmoja anayesimama na kukemea kwa ukali kuhusu mstaafu aliyeijenga nchi hii kupewa pensheni ya ‘Laki si Pesa’ kwa mwezi. Ni kama vile ‘nyongeza ya pensheni kwa mstaafu’ hakuna inayemhusu, kama vile wao hawatastaafu!

Inasikitisha mno wastaafu wanapowaona wawakilishi wakifikia hatua ya kutaka kuruka ‘samasoti’, kutoa machozi, kupiga magoti na kuunga mkono hoja ndani ya Bunge wanapotaka majimbo yao kuwekewa maji, kuwekewa lami, kuletewa dawa na kadhalika, lakini siyo kwa kutaka wastaafu kuongezewa pensheni yao ya mwezi ya ‘Laki si Pesa’!

Hili kila mwakilishi anaogopa kulisemea na kulikemea. Kwa kuwa hata Siri-kali yenyewe haishughuliki nalo, hakuna mwakilishi anayeshughulika nalo, asije akachafua bure nafasi yake ya kuteuliwa.

Mstaafu amefanywa kuwa ‘ombaomba’ kwenye nchi yake mwenyewe aliyoipigania uhuru wake na kuijenga kwa moyo mkuu. Nyongeza ya pensheni yake ya ‘Laki si Pesa’ anaomba kwa miaka 19 sasa mpaka midomo imeota sugu. Matibabu ya bure kwa wazee ameomba lakini anaishia kupewa maneno ya kanga tu. Hivi hili si linataka utashi tu na busara ya kawaida tu?

Yaani pamoja na kushauriwa kikejeli na waheshimiwa kuhamia Burundi wakiona mambo yanaendeshwa segemnege na wao kuamua ‘kubanana hapahapa’ maana nchi hii ni yao wote, ndio hasira za waheshimiwa na wawakilishi hao zimeishia kwenye kuwageuza wastaafu wetu kuwa ombaomba wa kudumu? Wastaafu wenyewe wa kima cha chini, kama siyo cha chizi wamebaki wangapi jamani? Mnataka nyongeza ya pensheni muwapelekee Kinondoni?

Mstaafu wetu anakiri kuwa linapokuja suala la hesabu kichwani hana tofauti na Watanzania wengi. Kichwa humuuma, lakini anajua kuwa Sh14 milioni mara idadi ya waheshimiwa 360 ni sawa na shilingi… mama wee!  bilioni tano na milioni arobaini (Sh5.04 bilioni) kwa mwezi! Hela ya kumpa nyongeza ya pensheni yake mstaafu kuwa japo Sh500, 000 kwa mwezi haipatikani hapo?

Halahala wawakilishi wetu, msiwafikishe wastaafu wetu mahali pa kujiuliza kati ya andazi na wawakilishi wetu, wachague nini… Japo jibu lao linaweza kuwa hadi mwaka kesho kwenye uchaguzi mkuu.                                                           

Related Posts