MYOMA YENYE ZAIDI YA KILO 4.2 ILIVYO MTESA MAMA WA MIAKA 44 KWA MIAKA MITANO

Na WAF – Mtwara.

Timu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia wanaoendelea kutoa huduma za matibabu karibu na wananchi kwa sasa wamefanikiwa kumtoa uvimbe kwenye mfuko wa kızazi ( Uterine Myoma) wenye uzito wa kilogram 4.2 kwa Bi. Anna Kanjula mwenye umri wa miaka 44 mkazi wa kata ya Likombe mkoani Mtwara

Hayo yamebainishwa Mei 30, 2024 na Daktari Bingwa wa wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Mbagala Rangi tatu, manispaa ya Temeke jijini Dar Es Salaam Dkt. Musa Kakiziba katika kambi ya matibabu ya madaktari bingwa wa Rais Samia halmashauri ya wilaya ya Mtwara Mjini mkoani Mtwara iliyoanza kazi tarehe 27 Mei, 2024 hadi Mei 31.

Dkt. Kakiziba amesema tatizo hilo lilikuwa likimsumbua mgonjwa huyo kwa zaidi ya miaka mitano na ulikuwa ukiongezeka ukubwa kadri siku zilivyokuwa zinakwenda.

“Kutokana na kutoweza kumudu gharama za matibabu ilisababisha uvimbe huo kukuwa ukubwa na ulikuwa ukimuangalia ni Kama mama mjamzito anayekaribia kujifungua, baada ya ujio wa madaktari bingwa alifika na tukamfanyia vipimo na hatimae tumeweza kuutoa uvimbe huu uliokuwa ukimtesa kwa zaidi ya miaka tano” amesema Dkt. Kakiziba na kuongeza

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutuleta karibu na wananchi ili kuwawezesha kuwapatia huduma na kuwaondolea gharama za matibabu na kuwapa tabasamu” amesema Dkt. Kakiziba.

Kakiziba ametaja chanzo cha tatizo hakijulikani ila baadhi ya vichocheo/ homoni (hormones) zilizoko kwenye mwili wa mwanamke (estrogen) zinahusishwa kuongeza ukuaji wake ndio maana mwanamke akikoma hedhi huu uvimbe unapungua , maana vichocheo vinakuwa vimepungua.

Katika hatua nyingie madaktari bingwa wa Rais Samia wameweza kumtoa mtoto kipande cha jalada la daftari sikioni ambacho alikitumia kutoa uchafu sikioni, mtoto huyo amekaa na karatasi hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu.

Related Posts