Katesh. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesimulia kisa cha urais mwaka 2005 alipofunga safari kutoka Bunda, Mkoa wa Mara kwenda kwa Waziri mkuu wa wakati huo, Fredrick Sumaye kumuomba amwachie Jakaya Kikwete awanie urais.
Dk Nchimbi wakati huo amesema alikuwa na miaka 31 na Mkuu wa Wilaya ya Bunda na uamuzi huo alikuja kubaini kuwa alikosea na wala Sumaye hakumchukulia hatua zozote.
Ametoa simulizi hiyo leo Ijumaa, Mei 31, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Katesh, Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara, akielezea jinsi alivyomfahamu Sumaye ambaye alikuwapo kwenye mkutano huo.
Dk Nchimbi ameanza kwa kusema
Mzee Sumaya ni muungwana sana:” Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2005, mimi nikiwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, nikampigia simu Waziri Mkuu na kumuomba miadi ya kukutana naye nyumbani kwake.”
Akasema njoo tu kijana wangu hakuna shida.
“Nilipokwenda alinikaribisha vizuri, akaniuliza unasemaje, nikamweleza Mzee nimekuja kukuona, kwanza unafanya kazi vizuri lakini hili la urais mwachie Kikwete, urais umwachie Kikwete akaniuliza kwa nini?”
Dk Nchimbi amesema alimweleza kwa sababu ya mazingira kunahitaji kubadilishana badilishana. Akitoka huyu anakuja huyu
“Akaniambia hilo jambo zuri, lakini mwambie aje yeye tuongee.
Nikaenda kwa Kikwete kumweleza kuwa waziri mkuu amekubali kukuachia lakini uende mkaongee,” ameeeleza Dk Nchimbi.
Baada ya maelezo hayo, akatulia kidogo kisha akasema:” Kwani (Kikwete) alikwenda? hakwenda.” Watu waliokuwapo mkutanoni wakafurahia akiwemo Sumaye mwenyewe.
“Nikaja kumuuliza siku nyingine kwa nini hukwenda? Akaniambia wewe bado kijana mdogo hujajua. Sasa nikienda mimi ni waziri yeye ni waziri mkuu nikienda kumweleza ataona mimi waziri nafaa kuliko yeye waziri mkuu,” amesimulia Dk Nchimbi.
Katika kuhitimisha hilo, DK Nchimbi amesema:”Nikaona kumbe nilikosea. Angekuwa mwingine (waziri mkuu) hata kazi ningefukuzwa. Lakini ndio kwanza siku hiyohiyo na chakula nikapewa.”
Katika uchaguzi huo wa 2005, Sumaye hakuchukua fomu ndani ya CCM. Makada kadhaa walijitosa, lakini hata hivyo mwishowe Kikwete ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje, alipitishwa na chama hicho kupeperusha bendera yake na kuibuka mshindi wa nafasi ya urais.
Mwaka 2015 katika mbio za kusaka mrithi wa Kikwete, Sumaye alikuwa miongoni mwa makada 38 wa CCM waliojitosa kuchukua fomu ndani ya chama hicho ili kupitishwa kuwania kuwa Rais.
Hata hivyo, hakufanikiwa kwani jina lake lilikuwa miongoni mwa yaliyokatwa mapema na Kamati Kuu. Dk John Magufuli ndiye alipitishwa kuwania urais na akashinda.
Jambo jingine kumhusu Sumaye, Dk Nchimbi amesema: “Nilipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda nilikuwa kijana wa miaka 31 au 32. Wikendi moja nilikwenda kupumzika Mwanza. Nikasema Jumamosi, Jumapili hakuna kazi, huko nyuma ikatokea ajali ya boti wawili, watatu wakapoteza maisha.”
Nikapigiwa simu waziri mkuu anataka taarifa, mimi habari yenyewe sina. Nikajibu niko eneo la tukio nawapa jibu sasa hivi. Nikapiga simu na kupewa taarifa, lile eneo lilikuwa ili kufika ilihitaji muda wa saa tatu na nusu lakini nilitumia saa mbili na nusu na nilikuwa naendesha mwenyewe,” amesema
Dk Nchimbi amesema: “Kwa hiyo mzee alikuwa anafuatilia kila kitu kuanzia ngazi ya wilaya na mikoa na ndio utendaji mzuri unaopaswa kuwa.”