Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi Mhe. Geophrey Pinda amewatembelea na kuwafariji wananchi wa kijiji cha Ukingwamizi katika kitongoji cha Itumba kata ya Mwamapuri kufuatia watu saba kupoteza maisha kwa ajali ya Mtumbwi.
Ajali hiyo iliyotokea mwishoni mwa wiki kufuatia maji kutoka mto Kavuu kuzunguka maeneo ya kitongoji cha Itumba ambapo miili ya watu watano imeopolewa huku miili ya watu wawili ikiwa haijapatikana.
Akizungumza na wananchi wa kijiji Ukingwamizi tarehe 30 Mei 2024 mkoani Katavi, Mhe. Pinda amewapa pole wafiwa na kuwaeleza kuwa serikali iko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha msiba wa ndugu zao waliopoteza maisha kwenye ajali.
‘’Serikali iko na nyie ndiyo maana mmeona walikuja na kulala hapa kuhakikisha wanafanikisha upatikanaji wa miili ya ndugu zetu’’ alisema Mhe. Pinda
Amewaambia wananchi wa kitongoji cha Itumba kuwa, baada ya ajali hiyo hivi sasa ni vyema wakaanza kuchukua tahadhari madhubuti kwa kuhakikisha vyombo vya usafiri wanavyotumia kwenye maji vinaimarishwa na kuangaliwa kila wakati kwa kuwa vikikaa muda mrefu vinaoza na hivyo kuwa rahisi kupitisha maji.
Aidha, amewataka wanaotumia mitumbwi kuhakikisha pia mizigo inawekwa kulingana na uwezo wa chombo hicho sambamba na abiria wanaopanda kutokuwa wengi kupita kiasi.
Mhe. Pinda amewaeleza wananchi wa kitongoji cha Itumba kuwa, ipo haja kwa sasa kuhakikisha mito kwenye halmashauri ya Mpimbwe inalindwa kwa kupanda miti katika kingo ili kuepuka uharibifu wa mazingira sambamba na vyanzo vya maji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe katika wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Bi. Shamimu Daud amewapa pole wananchi wa kitongoji cha Itumba kufuatia watu saba kupoteza maisha kwa ajali ya Mtumbwi.
Ametoa shukurani za dhati kwa wananchi wa Itumba kwa kusaidia juhudi za kutafuta miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
‘’kwanza natoa shukurani za dhati kwa wale wote kwa kazi kubwa waliyoifanya katika eneo hili, wananchi ambao pia wamejitolea kuingia na kutafuta wenzetu na watumishi wote kwa kazi zilizofanyika hapa’’. Amesema Shamimu.