HAKUNA shaka kuwa uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, umeanza kugubikwa na utata na ikiwa mamlaka hazitakuwa makini, hakika waweza kuvurugika. Anaandika Oliver Mwikila … (endelea).
Hii ni kwa sababu, hata kabla ya uchaguzi wenyewe kuanza kufanyika, tayari kumeibuka utata unaotokana na kuwapo sheria tatu zinazosimamia uchaguzi mmoja: Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura ya 288, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 na sheria inayounda Tume Huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024.
Sheria za Serikali za Mitaa, Miji, Hlmashauri za wilaya na miji midogo, zinampa mamlaka waziri wa Tamisemi kutunga kanuni za kusimamia uchaguzi huo. Sheria zote hizo tatu, zote zimepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Lakini iliyopitishwa karibu zaidi ni sheria inayounda Tume Huru ya Uchaguzi. Ilipitishwa katika mkutano wa Bunge wa Februari mwaka huu.
Pamoja na mengine, sheria hii mpya, imeipa mamlaka Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia na kuendesha chaguzi zote nchini, ukiwamo wa Serikali za Mitaa.
Kifungu cha 10 (1)(c) cha sheria hiyo kinataja jukumu la Tume Huru ya Uchaguzi kuwa ni “kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji Tanzania Bara, kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika Sheria itakayotungwa na Bunge.”
Hii maana yake ni kwamba, mamlaka ya kusimamia uchaguzi wowote nchini, yamewekwa mikononi mwa tume hiyo.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 64 (1), mamlaka yote ya kutunga sheria juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara, yameachwa mikononi mwa Bunge.
Lakini kinachosikitisha ni kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, hawataki kutumia Tume ya Uchaguzi waliyoiunda wenyewe, kusimamia uchaguzi. Hawataki.
Wanataka uchaguzi usimamiwe na waziri wa Tamisemi, ambaye kwa mujibu wa sheria, ni Rais wa Jamhuri ya Muungano; mwenyekiti wa chama kilichoko Ikulu na mgombea mtarajiwa wa urais katika uchaguzi ujao.
Aidha, mwenyekiti huyo wa chama tawala aliyejivika mamlaka ya kusimamia uchaguzi, chama chake, kinatarajiwa kusimamisha wagombea katika uchaguzi huo nchi mzima, kushindana na wagombea wengine wa vyama vya siasa.
Haya yanaweza kuthibitishwa na kauli ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Joseph Kizito Mhagama, aliyoitoa kwenye kituo kimoja cha televisheni.
Akiwa na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasi (TCD), Prof. Ibrahim Lipumba, mbunge huyo wa Madaba mkoani Ruvuma, alidai kuwa serikali kupitia Tamisemi, iko sahihi kuandaa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mhagama ndiye aliyechambua, kushauri Bunge na kubariki yaliyomo katika kifungu cha 10 cha muswada wa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, kilichoipa mamlaka tume hiyo, kusimamia, kuratibu na kuendesha uchaguzi wa mitaa, vijiji na vitongoji.
Hakuna kokote katika rekodi za Bunge, ambako Mhagama amesikika akikishauri chombo hicho chenye mamlaka ya kutunga sheria, kuwapo sheria nyingine inayopingana na hiyo inayotungwa. Hakuna.
Wala wananchi hawajamsikia Mhagama au mbunge mwingine yeyote wa CCM, akiwasilisha hoja bungeni inayoitaka Serikali kupeleka muswada mpya wa sheria, utakaofuta vifungu vinavyompa mamlaka waziri wa Tamisemi kusimamia uchaguzi.
Hilo halijafanyika kwa kuwa wanajua kuwa uchaguzi ukisimamiwa na Tamisemi, tayari ni mtaji kwao.
Badala yake, wananchi wamewasikia wabunge wao, wakipitisha kwa shangwe na vigelegele, makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, Tamisemi yaliyowasilishwa bungeni na Mohammed Mchengerwa, waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi).
Katika hotuba yake, Mchengerwa alisema serikali iko katika maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa na kwamba wizara hiyo, inaomba kuidhinishiwa Sh. 12 bilioni, kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi huo.
Alisema, hadi Machi 2024, Tamisemi imepokea takribani Sh. 5.6 bilioni sawa na asilimia 46.67 ya fedha iliyoidhinishwa kutoka Hazina.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, tayari uhakiki wa maeneo ya utawala umefanyika. Rasimu ya tangazo la serikali la maeneo ya utawala limetolewa, rasimu ya kanuni za uchaguzi na vikao vya wadau, vinavyolenga kupata maoni ya rasimu ya kanuni, tayari vimefanyika. Japokuwa hadi sasa kanuni hizo wadau wa uchaguzi hawajaziona ili kutoa maoni yao.
Hofu kubwa ya wananchi kuhusiana na umuhimu wa uchaguzi huu kusimamiwa na Tamisemi inatokana na kile kilichotokea katika chaguzi zilizopita, hasa uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019.
Katika muktadha huo, nani anaweza kusema hapa kuwa uchaguzi huu, utaweza kuwa huru na haki? Nani anaweza kuamini maneno ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, (Bara), Abdulrahaman Kinana, kwamba chama chake, kina nia thabiti na dhamira ya dhati ya kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao, unaendeshwa kwa uwazi, huru na haki? Nani! Kama hadi sasa kanuni za uendeshaji wa uchakuzi wa Serikali za mitaa bado Tamisemi inalazimisha ziwe chini yake badala ya Tume Huru ya Uchaguzi.
Kinana amenukuliwa mara kadhaa, akieleza kuwa kutokana na utashi na dhamira njema ya Rais Samia, chaguzi zijazo zitakuwa huru na haki.
Alisema, “Rais Samia ametoa kauli nyingi juu ya umuhimu wa kuwa na uchaguzi huru na haki. Amediriki hata kusema, CCM haina hati miliki ya nchi hii. Tumepewa dhamana ya kuongoza kwa miaka mitano, baada ya hapo, tutarudi tena kwa wananchi ili waamue wanavyotaka.
“Hivyo basi, ni matumaini yangu, kwamba tutakwenda kwenye uchaguzi mkuu ujao, tukiwa na muafaka na maelewano yanayokidhi haja ya kuwa na uchaguzi huru na haki.”
Hakuna asiyefahamu kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa, ndio mwanzo wa uchaguzi mkuu. Viongozi watakaopatikana kwenye chaguzi hizi, watakuwa na nafasi kubwa ya kusimamia na kuendesha uchaguzi unaokuja, kuanzia uandikishaji wapiga kura hadi uchaguzi wenyewe.
Swali ambalo wananchi wanajiuliza ni hili, nani anayemtuma Mchengerwa na chama chake, kuvuruga uchaguzi? Bila shaka aliyemtuma Mchengerwa kuvuruga uchaguzi, ni yule mwenye maslahi mapana na uchaguzi huo.
Hivyo basi, ni muhimu kwa Rais Samia, kuepusha mapema kuvurugika kwa uchaguzi huu. Vinginevyo, ataingia kwenye historia ya mtangulizi wake, anayekumbukwa kwa kuvuruga uchaguzi wa mitaa wa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Asikubali kufikishwa huko.