Seoul. Rais Samia Suluhu Hassan amewasili nchini Korea Kusini tayari kwa ziara ya siku sita, ambako pamoja na mambo mengine atashuhudia itiaji saini wa mikataba mbalimbali ya ushirikiano.
Rais Samia amewasili jijini Seoul saa 12 jioni kwa saa za Korea (saa 6 mchana saa za Tanzania) na kesho Juni mosi, 2024 ataanza ziara ya kitaifa na baadaye Juni 4 na 5 atashiriki mkutano kati ya Korea Kusini na viongozi wa mataifa ya Afrika.
Katika ziara hiyo Rais Samia ameambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji na Waziri wa Nchi, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais wa Zanzibar, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Natu Mwamba.
Katika ziara hii, Serikali za Tanzania na Korea Kusini zitatiliana saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano yenye thamani ya Sh6 trilioni.
Pamoja na shughuli nyingine za kiserikali, Rais Samia atatunukiwa shahada nyingine ya udaktari wa hesima na Chuo Kikuu cha Korea cha Usafiri wa Anga ikiwa ni shahada yake ya tano kutunukiwa na vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya Tanzania.
Tanzania na Korea zimekuwa na ushirikiano wa miaka 32 katika maeneo ya elimu, afya na miundombinu.
Baada ya mazungumzo ya viongozi wakuu wa nchi hizi mbili, mikataba saba ya ushirikiano itasainiwa.
Mikataba hiyo ni pamoja hati ya makubaliano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Sayansi na Miamba na Madini ya Korea, ushirikiano utakaojikita katika utafiti, uchoraji ramani, rasilimali na shughuli za maabara.
Mikataba mingine ni ushirikiano katika maendeleo ya uchumi wa buluu, kutambua vyeti vya mabaharia, tamko la pamoja la uanzishwaji wa majadiliano kuhusu mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi.