Rais wangu mama Samia; Wananchi wa Igoma watendewe haki

RAIS wangu mama Samia, wananchi wa eneo la Igoma Truck Terminal, mtaa wa Mwembeni, kata ya Igoma jijini Mwanza, wanateseka kwa sababu ya watendaji wako. Wamezibiwa barabara ya kupita na wawekezaji wa kiwanja namba 109 kitalu B. Anaandika Leonard Manyama… (endelea).

Kiwanja hiki ni mali ya halmashauri ya jiji la Mwanza ambacho awali kilibaki bila kuendelezwa na hatimaye wananchi kukivamia. Hata hivyo, halmashauri ya jiji la Mwanza ilipata maombi ya wawekezaji kutoka katika kampuni tatu tofauti.

Lakini kabla ya kupewa, ofisi ya mipango miji ya jiji la Mwanza ilipendekeza kwa kamati ya mipango miji, ardhi na maliasili ya jiji la Mwanza, pamoja na mambo mengine, kuingizwa kwenye mchoro na hatimaye kurasimishwa kwa barabara ya wananchi ambayo ilikuwa ikitumika kwa muda mrefu ili kuondoa usumbufu.

Barua ya afisa mipango miji ya jiji la Mwanza iliyosainiwa na Hosiana B Kusiga ya tarehe 2/11/2014, kwenda kwenye kamati ya mipango miji, ardhi na maliasili ya jiji la Mwanza inasema: “Mwombaji alipe gharama zote za upimaji, gharama za kuandaliwa hati pamoja na gharama za kugawa kiwanja ili kuingiza njia ya mita sita ambayo imekuwa ikitumika kupita kuelekea soko la mbao Igoma, na kwenda kanisa la KKKT kama ambavyo imeshauriwa na diwani wa kata husika ili kutosumbua wananchi kabla ya kumilikishwa kiwanja.”

Rais wangu haya yote sasa yamepuuzwa na wawekezaji wa eneo hilo na mamlaka husika zinaonekana kufyata mkia. Wananchi wanajiuliza kuna nini? Ikiwa ofisi ya mipango miji iliwataka wawekezaji kabla ya kumilikishwa eneo hilo kuwasilisha michoro ya uendelezaji wa eneo kwa kuzingatia matumizi yaliyopo, kimeshindikana nini mpaka  barabara hii kuzibwa na kuleta usumbufu kwa wananchi?

Rais wangu mama Samia, barabara hii ni kubwa, licha ya kuhudumia wafanyabiashara wa soko la mbao la Igoma na waumini wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), inahudumia pia waumini wa kanisa la Waadiventista Wasabato, msikiti wa Qiblatain pamoja na wanafunzi wa shule za msingi Uhuru na Shamaliwa.

Hawa wote sasa wanalazimishwa kupita barabara ya mzunguko mrefu iliyobuniwa na wawekezaji hawa, barabara ambayo inadaiwa kusababisha kadhia nyingi kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuhatarisha maisha yao.

Aidha, wawekezaji hawa wameziba hata mkondo wa maji uliokuwa unapita eneo hilo na kwenda kuungana na mfereji wa barabara kubwa. Kitendo cha kuziba mkondo wa maji kimesababisha maji kufurika katika makazi ya watu na kuleta madhara makubwa.

Rais wangu mama Samia, hii barabara iliyozibwa, ilitambuliwa rasmi katika ramani za makazi na kupewa jina la Ndofe. Ndugu zetu wawekezaji wameiziba bila kujali yote haya. Lakini cha kushangaza zaidi ni pale wanapoonekana kuendelea kukaidi maagizo ya serikali yanayotolewa kwao.

Barua ya mkurugenzi wa jiji la Mwanza ya tarehe 19/12/2023, yenye namba ya kumbukumbu MCC/L/66448/24 iliyosainiwa na Aron T Kagurumjuli kwenda kwa wawekezaji hao, pamoja na mambo mengine iliwaelekeza kubomoa ukuta huo.

Barua ya Kagurumjuli inasema, “Imebainika kuwa ukuta uliojenga katika kiwanja chako namba 109 B lgoma umeleta athari kwa jamii kama ifuatavyo. Kuziba barabara iliyozoelewa kutumika japokuwa si rasmi na kuzuia mkondo wa maji ya mvua yaliyokuwa yakikatiza kwenye kiwanja.

Hii imekuwa ikisababisha mafuriko kwenye makazi ya wananchi mara tu mvua zinaponyesha. Unaagizwa kufanya yafuatayo. Kubomoa ukuta huo unaozuia mkondo wa maji. Kujenga mtaro mkubwa utakaowezesha mkondo wa maji kutoka upande wa juu kupita kati yako na jirani. Aidha, unakumbushwa kulipa deni la kodi ya pango la ardhi ya kiwanja hiki. Nakutakia utekelezaji mwema.” Rais wangu, leo ni zaidi ya miezi sita sasa tangu maagizo hayo yatolewe lakini hakuna chochote kilichofanyika.

Kiburwa Kibamba

Rais wangu mama Samia, gazeti hili liliwasiliana na mkurugenzi wa jiji la Mwanza ndugu Kiburwa Kibamba kutaka kujua ni kwanini mpaka sasa maagizo yake hayajatekelezwa na hivyo kuendelea kusababisha kero kwa wananchi. Lakini katika hali ya kushangaza, mkurugenzi alisema hana taarifa yotote juu ya kadhia hiyo.

Alipoelezwa kwamba inakuwaje anakosa taarifa za kadhia hiyo wakati ofisi yake ndio imeagiza kubomolewa kwa ukuta, alisema hawezi kuongea vitu ambavyo hana uhakika navyo na kwamba wakati barua hiyo inaandikwa yeye hakuwepo ofisini na kwamba yeye hana barua ya aina hiyo ofisini kwake.

Alipoulizwa na mwandishi inakuwaje anakosa taarifa za kadhia hiyo wakati jambo hilo liko ofisini kwake tangu mwaka 2014, alisisitiza kwamba kipindi hicho yeye hakuwepo ofisini na kwamba hata alipoingia hawezi kusoma kila kitu.

Rais wangu hawa ndio watendaji wako. Hawa ndio wenye dhamana ya kukuwakilisha kwa wananchi na ndio wanaokutafsiri kwao. Hii ndio picha wanayoipeleka kwao na ndivyo wanavyotaka wananchi wakuelewe.

Rais wangu mama Samia, baada ya kuona kwamba wamekosa msaada, wananchi hawa walikuandikia barua tarehe 25/09/2023 wakilalamikia jambo hilo na baadaye kukuandikia barua ya pili hivi karibuni. Wanasema katika barua yao ya pili kwako kwamba “barua tuliokuandikia awali ilizaa Kikao cha tarehe 13/10/2023 baina ya uongozi wa serikali ya mtaa na wawekezaji ambapo katika kikao hicho (wawekezaji) waliridhia kuwa barabara hiyo wataifungua na kuacha mita sita kama ambavyo walikubaliana na halmashauri.

Rais wangu mpaka leo kama nilivyosema hakuna utekelezaji wowote. Hawa wananchi hawana uhakika kama barua zao umeziona na wanatamani uwaagize wasaidizi wako wengine wawasaidie maana walio karibu nao wameshindwa kutatua kero yao. Tafadhali usiwaache.

Rais wangu mama Samia, katika barua yao ya pili kwako wananchi hawa wanasema hata mkuu wa wilaya ya Nyamagana, dada yangu Amina Makilagi ameshindwa kuwasaidia. Wamekuandikia hivi “Mheshimiwa Rais mnamo tarehe 21/1/2024 mkuu wa wilaya Amina Makilagi, alifanya kikao cha pamoja kati ya wawekezaji na wananchi na waathirika katika maeneo ya Mtaa wa Mwembeni ambapo katika kikao hicho naye alitoa agizo la kuwaamuru wawekezaji wavunje ukuta ndani ya siku saba na vyombo mbalimbali (vya habari) viliripoti tukio hili. Mpaka tunakuandikia barua hii hakuna kilichotekelezwa wala kufanyiwa kazi.”

Gazeti lilimtafuta mkuu wa wilaya kupata kauli yake juu ya madai haya. Kwa isivyo bahati, yeye aligoma kusema chochote mpaka kwanza atumiwe barua ya mkurugenzi iliyoanza kutoa amri ya kubomolewa kwa ukuta huo akidai alitaka kuona kwanza kilichoagizwa na mkurugenzi ili alinganishe na maagizo aliyotoa.

Lakini hata alipotumiwa barua husika, bado aligoma kutoa ufafanuzi na kumtaka mwandishi kufika ofisini kwake ili kupewa vilelelezo. Hata alipotakiwa kuthibitisha kwamba amewahi kuagiza ukuta kubomolewa na kwa nini maagizo yake yameendelea kupuuzwa, aligoma kwa madai kwamba ni lazima mwandishi afike ofisini. Baadhi ya wawekezaji walipotafutwa walikana kupewa maelekezo ya kubomoa ukuta wakati Mbunge Festo Kiswaga hakupokea simu wala kujibu maswali aliyotumiwa.

Related Posts