RC Serukamba ataka kodi isikusanywe kibabe

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba amesema kodi haiwezi kukusanywa kwa ubabe, akiwataka maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo kutumia lugha nzuri.

Amesema ikiwa mteja ana deni na wanataka kuifunga akaunti yake, ni vizuri wafuate utaratibu ikiwamo kuzungumza naye ili atakapokaidi ndipo wachukue hatua zinazofuata.

Serukammba amesema hayo leo Mei 31, 2024 wakati akizungumza na wafanyabiashara kupitia Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Iringa ambao walitoa malalamiko dhidi ya TRA.

Miongoni mwa malalamiko ya wafanyabiashara hao ni matumizi ya lugha mbaya, kufungiwa akaunti, kubambikwa madeni ya kodi za nyuma, tozo mara mbili pamoja na kusainishwa mikataba ya mashine za kutolea risiti za EFD kwa wanaodhaniwa hawatumii.

“Msikusanye kodi kwa vitisho, tumieni lugha nzuri wakati mnapowafanyia wafanyabiashara makadirio na nikuombe meneja utenge muda wa kukutana na hawa wafanyabiashara,” amesema Serukamba.

Aidha, amewatoa hofu wafanyabiashara hao kuwa suala la mikataba ya mashine za EFD halitajitokeza tena na kwenye eneo la madeni ya nyuma, wakae na wafanyabiashara kukubaliana nao.

“Na nyie wafanyabiashara jitahidini mkiuza mtoe risiti na mkilipa  kodi tunzeni kumbukumbu zenu,” amesema Serukamba.

Awali Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Iringa, Cola Mtende,  amesema ikiwa hotuba ya mkuu huyo wa mkoa itafanyiwa kazi, malalamiko ya wafanyabiashara kwa TRA yatapungua.

“Malalamiko tuliyonayo ndiyo yamesababisha tuandae mkutano huu na tumuite mkuu wa mkoa, kama yatafanyiwa kazi basi tutaendesha biashara zetu kwa amani,” amesema.

Baadhi ya wafanyabiashara walisema kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita walikuwa wakipigiwa simu au kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kuhusu matumizi ya mashine za EFD lakini walipoenda walipewa mikataba kwamba, wakiivunja watatozwa faini mpaka Sh1.5 milioni.

“Wiki mbili zilizopita niliambiwa situmii mashine wakaniita na kunipatia mkataba huu,” amesema James Mgimba mmoja wa wafanyabiashara.

Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Aziz Rajab amesema malalamiko ya wafanyabiashara hao yatafanyiwa kazi na kwamba mlango wa ofisi yake upo wazi.

“Ofisi ipo wazi muda wowote na mwenye shida ya kuniona muda wowote awe huru, tutabandika namba za simu za viongozi kwenye ubao watangazo na kwenye mlango wa kuingilia ili muweze kupiga,” amesema.

Related Posts