RIPOTI MAALUMU: Hali ya viwanja kabla na baada ya AFCON -3

VIWANJA ni miongoni mwa mahitaji makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) katika kutoa haki za uenyeji wa fainali za mataifa ya Afrika (Afcon).

Tanzania itaandaa fainali hizo mwaka 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda kupitia mpango uliopewa jina la ‘Pamoja Bid’ na hili hilo lifanikiwe ni lazima kuwepo na viwanja vinavyokidhi vigezo na mahitaji ya Caf kwa nchi mwenyeji.

Miongoni mwa mahitaji ya Caf ili kutoa uenyeji wa Afcon kwa nchi ni kuwa na viwanja sita ambavyo kati ya hivyo, viwili ni viwe na uwezo wa kuingiza mashabiki 40,000, viwili viwe na uwezo wa kuingiza mashabiki 20,000 na vingine viwili vinavyoingiza mashabiki wasiopungua 15,000.

Kenya, Uganda na Tanzania hapana shaka zina idadi stahili ya viwanja angalau sita ambavyo vinakidhi kuandaa Afcon 2027 kwa kigezo cha idadi ya mashabiki ambayo caf inahitaji viwe navyo ili kuandaa mashindano hayo.

Viwanja vinavyoingiza mashabiki 40,000 au zaidi vipo vitatu ambavyo ni Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam (Tanzania) unaoingiza mashabiki 60,000, Nelson Mandela (Namboole) ambao upo Kampala (Uganda) ukiwa na uwezo wa kuingiza mashabiki wapatao 45,200 na ule wa Moi ambao upo Nairobi (Kenya) ambao unaingiza mashabiki 60,000.

Kwa viwanja vya mashabiki 20,000 na 15,000, Tanzania yenyewe kwa mujibu wa maombi ya kuandaa fainali hizo, iliwasilisha majina ya viwanja vya Amaan (Zanzibar) unaoingiza mashabiki 15,000 na mwingine itakaoujenga Arusha wa Samia ambao utaingiza mashabiki 30,000.

Uganda mbali na Namboole, pia wamepanga kutumia Uwanja wa Nakivubo unaoingiza mashabiki 35,000 na imepanga kujenga vingine viwili katika miji ya Hoima na Lira ambavyo kila kimoja kitaingiza mashabiki wasiopungua 15,000.

Kenya ukiondoa Moi, imepanga pia kutumia Uwanja wa Nyayo unaoingiza mashabiki 30,000 na ule wa Kipchoge Keino-Eldoret ambao unaingiza mashabiki 20,000.

Rais wa Caf, Patrice Motsepe alisisitiza kuwa shirikisho hilo halitokuwa na msamaha kwa Tanzania, Kenya na Uganda ikiwa zitashindwa kutimiza vigezo vinavyohitajika vya kuandaa fainali hizo hasa kile cha miundombinu na viwanja.

“Tuko na msimamo mkali kwenye suala la vigezo ambavyo tumezipa hizi nchi kuanzia uhuru wa mizunguko ya watu ndani na nje ya nchi zote pamoja na miundombinu.

“Tutatuma timu kwa utaratibu wa kawaida kufanya tathmini na kuangalia hatua zinazopigwa kwa sababu uhalisia ni kwamba tunataka kuendeleza hadhi ya juu ya mpira wa miguu Afrika,” alisisitiza Motsepe.

Hali ya viwanja Tanzania na vita ya muda Afcon

Uwepo wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Amaan Zanzibar na huo wa Samia utakaojengwa Arusha ambao utakagharimu kiasi cha Sh286 bilioni ni jambo linaloipa matumaini Tanzania kuwa hadi ifikapo Desemba 2025, itakuwa na viwanja vitatu vinavyokidhi hadhi ya uenyeji wa mashindano hayo na kukubalika na Caf baada ya timu ya wataalam wa ukaguzi wa viwanja wa shirikisho hilo kufanya hivyo.

Na hilo linadhihirika kupitia hotuba ya waziri wa utamaduni, sanaa na michezo, Damas Ndumbaro wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2924/2025 ambapo alisisitiza

“Haya ni maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Afcon 2027. Kiwanja hiki (Uwanja wa Samia) kinatarajiwa kuwa kimekamilika ifikapo Desemba 2025. Mashindano haya ya Afcon yatachagiza kuwapo kwa fursa lukuki za ujenzi wa miundombinu, kujenga uchumi, kuvutia utalii, ajira na kuitangaza Tanzania kimataifa,†alisema Ndumbaro.

Hata hivyo, hofu kubwa iliyopo hivi sasa ni ile ya kuona ujenzi na ukarabati huo wa viwanja unafanyika ndani ya muda sahihi na wa haraka na sio mwendo wa kinyonga.

Upo uwezekano mkubwa wa viwanja vya Benjamin Mkapa na Amaan  kurekebishwa ndani ya muda unaohitajika lakini kukamilika kwa ujenzi wa Uwanja wa Samia ni jambo linalosubiriwa kuona kama litatimizwa ndani ya muda ambao serikali imepanga kutokana na historia ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vilivyowahi kutumika kwa fainali za Afcon kwa nchi mbalimbali hapo nyuma.

Uwanja wa Alassane Ouattara uliochezewa fainali ya Afcon 2023 ambao unaingiza mashabiki 50,000, ujenzi wake ulifanyika kwa miaka minne kuanzia 2016 hadi 2020.

Fainali ya Afcon 2021 ilichezwa kwenye Uwanja wa Olembe uliopo Cameroon ambao ujenzi wake ulitumia miaka mitatu, kuanzia 2018 hadi 2021.

Uwanja wa Benjamin Mkapa upo katika ukarabati ambao unagharimu kiasi cha Sh31 bilioni ambao utaufanya uwe katika kategoria namba nne ambayo kwa maana nyingine ni hadhi ya nyota tano.

Ukarabati huo unafanyika katika vyumba vya wachezaji (dressing room), vyumba vya waandishi wa habari na eneo la watu mashuhuri zaidi (VVIP).

Pia wanabadilisha viti vyote vya uwanja, mfumo wa matangazo wa uwanja (PA system), ubao wa matangazo kuwa wa kidijitali, mfumo mzima wa TEHAMA, marekebisho kwenye eneo la uwanja kwa kuweka magoli mapya pamoja na maboresho kwenye neo la benchi la ufundi.

Ikumbukwe kwamba mwaka jana, ripoti ya mkaguzi mkuu wa serikali ilionyesha kuwa kuna matunzo duni ya Uwanja wa Benjamin Mkapa ambayo yanafanya hadhi yake ishuke.

“Hata hivyo, nimebaini mapungufu kadhaa kuhusiana na utendaji wa viwanja ambayo yanahitaji usimamizi wa menejimenti; Miundombinu na vifaa duni, viti vimevunjika na havijarekebishwa, hii inaweza kuwakatisha tamaa mashabiki kuhudhuria mechi na inaweza kuathiri mapato. Pia, nimebaini hali isiyoridhisha kuhusu miundombinu ya choo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Matengenezo yasiyotosheleza, uangalizi duni wa uwanja kutokana na kutokuwepo kwa mpango wa matengenezo wa mali ambao umesababisha usalama kuwa mdogo kwasababu viyoyozi havifanyi kazi vizuri. Usambazaji wa maji na mfumo wa usafi haukufanya kazi kwa njia inayoridhisha. Mapungufu katika Usalama Uwanjani, taratibu za kiusalama hazifanyi kazi kwani mfumo wa utambuaji wa moto na mfumo wa tahadhari (alarm system) haufanyi kazi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakati mfumo wa kuzima moto kwa maji haufanyi kazi kwa uwanja wa Uhuru.

“Nilibaini kuwa mapungufu haya ya utendaji katika viwanja vya mpira unatokana na matengenezo yasiyotosheleza, usimamizi duni, na ukosefu wa fedha za kutosha kwa ajili ya matengenezo. Ninaamini kuwa utendaji usioridhisha wa viwanja vya mpira unaweza kuwa na athari kubwa kwenye mapato, ushiriki wa mashabiki, na utendaji wa timu Ni muhimu kuchukua hatu kushughulikia kwa kutekeleza mapendekezo sahihi ili kuweza kusaidia ufanisi wa viwanja na kuhakikisha vinadumu kwa muda mrefu,” inafafanua ripoti hiyo.

Kitendo cha Uwanja wa Amaan, kuandaa mashindano ya Shule Afrika zilizo chini ya Caf kinaupa Uwanja huo mwanga mzuri kuelekea fainali za Afcon 2027.

Viwanja vya mazoezi tatizo kubwa

Miongoni mwa masharti ya kuandaa fainali za Afcon ni kuwa na viwanja vitatu vya mazoezi pembezoni au maeneo ya jirani na ulipo uwanja husika ambao umekidhi vigezo vya kutumika kwa mashindano hayo.

Kwa maana hiyo, ikiwa viwanja vitatu vya Tanzania vitatumika kwa Afcon, kunatakiwa kuwepo na viwanja tisa vya mazoezi vyenye hadhi ya kimataifa ambavyo vitapitishwa na timu ya ukaguzi ya viwanja ya Caf.

Mmoja wa wajumbe wa kamati ya leseni za klabu alilithibitishia gazeti hili kuwa kwa sasa ni uwanja mmoja tu unaokidhi kutumika kwa ajili ya mazoezi kwa fainali za Afcon ambao ni ule wa Black Rhino uliopo Karatu, Arusha kutokana na kukidhi vigezo vya kutumika kwa mazoezi.

“Ule ni uwanja ambao umekamilika na wenye sifa stahiki za kutumika kwa ajili ya mazoezi ya timu kwenye fainali za Afcon. Caf wako ‘serious’ (makini) sana kwenye suala la ubora wa viwanja vya mazoezi na mechi na wanafanya hivyo ili kulinda usalama wa wachezaji,” alisema mjumbe huyo ambaye hakupenda jina lake kutajwa hadharani.

Kwa mujibu wa muongozo wa viwanja wa Caf, uwanja wa mazoezi wa kutumika kwa Afcon unapaswa kutimiza vigezo saba ambavyo ni

(i) Taa zenye uwezo usiopungua lux 500

(ii)Angalau chumba kimoja cha kubadilishia nguo chenye siti 23 na maloka

(iii)Eneo la benchi lenye siti 20 kwa ajili ya wachezaji wa akiba na maofisa wa timu.

(iv)Magoli mawili yanayohamishika

(v)Mabomba yasiyopungua matatu ya kuogea, vyoo visivyopungua viwili vya haja kubwa, masinki matatu na vyoo visivyopungua vitatu vya haja ndogo.

(vi)Fensi inayohakikisha usalama kuuzunguka uwanja husika

(vii)Milango inayohakikisha usalama ya kuingia na kutokea.

Wahenga walisema kuzaa sio kazi bali kazi ni kulea mwana.

Usemi wa hili unaweza kutumika kuelezea hatima ya viwanja vitakavyojengwa na kukarabatiwa kwa ajili ya Afcon, vitakuwa katika hali gani mara baada ya fainali hizo kufikia tamati.

Kiasi kikubwa cha fedha kinapaswa kutumika kwa ajili ya kutunza viwanja hivyo vinginevyo vinaweza kupoteza ubora na hadhi kama ambavyo imewahi kutokea katika nchi kadhaa ambazo zimewahi kuandaa fainali hizo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirikisho la kimataifa la Saveya, matunzo ya uwanja unaoingiza mashabiki wanaofikia 400, gharama zake za matunzo kwa mwaka ni kiasi kisichopungua Dola 27,000 (Sh 70 milioni).

Tafiti hiyo inaeleza kwamba uwanja unaoingiza mashabiki wanaofikia 1,200, gharama za matunzo kwa mwaka hakipaswi kupungua Dola 60,000 (Sh 156 milioni).

Hata hivyo, bajeti ya matunzo ya viwanja vingi vya soka nchini imeonekana kuwa chini jambo ambalo linaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa matunzo duni ya viwanja hivyo.

“Kwa mwezi nimekuwa nikipatiwa kama shilingi 600,000 kwa ajili ya kutunza uwanja huu na kama kuna mechi kubwa mwezi huo, ndio napewa angalau Sh 1 milioni. Hata hivyo fedha hizo ninazopewa hazitoshi kulinganisha na mahitaji ya matunzo hivyo najitahidi kuhakikisha mambo yanaenda,” alisema mmoja wa mameneja wa viwanja vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Related Posts