SAFARI ZA DUBAI KUFUNGUA VIVUTIO VYA UTALII NA UWEKEZAJI TANZANIA

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imesema kuanzishwa kwa safari za Dubai ni utekelezaji wa mpango wake wa biashara ambao unaongeza wigo wa mtandao wa safari za kimkakati za kimataifa kutoka vituo viwili (2) hadi kufikia vituo vitatu (3).  

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mha. Ladislaus Matindi kwenye Kongamano la wadau wa ATCL lilofanyika katika hoteli ya One and the Only Royal Mirage, jana nchini Dubai.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mha. Ladislaus Matindi amesema ATCL ilianza kuifungua Tanzania kwa kuanzisha safari za Mumbai, India na baada ya mafanikio makubwa ikaongeza safari za Guangzhou, China na sasa imeanzisha safari za Dubai, Nchi za Falme za Kiarabu ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Mpango Biashara wa ATCL.

“Dubai ni sehemu muhimu ya muunganiko wa safari na Air Tanzania tumekuwa tukipata abiria sio tu kwa wanaoanzia Dubai lakini hata wale wanaounganisha safari kutoka nchi mbalimbali kupitia Dubai”.

Matindi ameongeza kuwa katika kuhakikisha Air Tanzania inafahamika vizuri, ATCL imefanya Kongamano jijini Dubai lililowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo mawakala wa tiketi za ndege, wasafirishaji wa watalii na mizigo, waandishi wa vyombo vya habari na wahamisishaji kutoka Tanzania na Dubai ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa masoko wa kuhakikisha ATCL inakubalika kibiashara na kuonesha vivutio na fursa zilizopo nchini Tanzania.

“Dubai ni soko lenye mvuto na lina ushindani mkubwa. Ili kufanikiwa ni lazima tufanye juhudi kubwa kuhakikisha kuwa wadau wetu wanaelewa vizuri Tanzania kuna nini. Tunahitaji kufanya juhudi za kupiga kelele kwa sauti ya juu ili kusikika na kujulikana, la sivyo watalii, wafanyabiashara na wawekezaji, watatumia ndege zingine kwenda kwenye nchi zinazosikika zaidi”, amesema Matindi. 

Matindi ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha utekelezaji wa Mpango Biashara wa ATCL ikiwemo kuruhusu ufunguzi wa kituo cha tatu cha safari za kimataifa na ameahidi kuongeza idadi ya safari za ndege Dubai kutoka mara nne (4) kwa wiki hadi kufikia safari za kila siku ifikapo Desemba 2024 ikiwa biashara na idadi ya ndege itaruhusu. 

Naye Balozi wa Tanzania wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Lt. Gen (Mstaafu) Yacoub Mohamed ameipongeza ATCL kwa kufanya kongamano la wadau wake hususan baada ya ufunguzi wa kituo kipya ambacho kina ushindani mkubwa. 

“Sekta ya Utalii inakuwa kwa kasi kutokana na Serikali kuboresha miundombinu na kuweka mazingira rafiki kwa wadau mbalimbali. Unapotumia ndege za Air Tanzania unalinda soko la ndani na kuchangia ukuaji wa uchumi”, amesema Mhe. Balozi Mohamed. 

Katika wasilisho lake kwenye Kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mussa Mbura amesema TAA itaendelea kuzingatia ulinzi na usalama wa viwango vya kimataifa ili kuwezesha ndege zinazotoka kwenye viwanja vya ndege nchini kuruhusiwa kutua maeneo mbalimbali duniani.  

Air Tanzania inafanya safari za ndani ya nchi kwenye mkoa wa Dar es Salaam, Arusha, Bukoba, Dodoma, Geita, Kilimanjaro, Kigoma, Songwe, Mpanda, Mwanza, Songea, Tabora na Zanzibar. Aidha kwa safari za kikanda ni Bujumbura, Entebbe, Hahaya, Harare, Lubumbashi, Lusaka, Nairobi, Ndola na safari za kimataifa ni Mumbai, Guangzhou na Dubai.

Related Posts