Dodoma. Jumla ya Sh30.5 bilioni zimetumika katika awamu ya kwanza ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwwa).
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis amesema hayo leo Mei 31, 2024 bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Najma Giga aliyehoji kwa nini Serikali isiweke kwenye Mpango wa Maendeleo wa kila mwaka kipaumbele cha kudhibiti vitendo vya udhalilishaji watoto nchini.
Akijibu swali hilo, Mwanaidi amesema Serikali imejumuisha masuala yote ya ukatili na udhalilishaji wa watoto katika Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwwa).
Amesema ambapo tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi wa kwanza inaonyesha jumla ya Sh30.5 bilioni zimetumika katika utekelezaji wa afua za kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
“Serikali ikiwa imetumia Sh25 bilioni na wadau wa maendeleo wametumia Sh5.5 bilioni ya fedha hizo,” amesema.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kutenga fedha za utekelezaji wa mpango kazi wa pili wa Mtakuwwa ikiwa ni jitihada za kuendelea kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hapa nchini.
Katika swali la msingi, Najma amesema ukatili wa kijinsia unaongezeka kwa kasi hasa ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo.
Amehoji mpango wa pili wa kutokomeza ukatili, wameweka kiasi gani cha fedha kutekeleza afua.
Pia amehoji hawaoni umuhimu wa kushirikiana na wadau wa dini kufanya nao makongamano kwa kuwa wao hukataza mabaya na kueneza mema.
Akijibu swali hilo, Mwanaidi amesema katika mpango wa pili wa Mtakuwwa wametenga Sh9.8 bilioni kwa ajili ya kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mbunge wa Viti Maalumu Fatma Taufiq amesema kumekuwa na matukio ya kupiga picha watu waliopata matukio ya udhalilishaji, na kuhoji nini kauli ya Serikali kuhusiana na kadhia hiyo.
Akijibu swali hilo, Mwanaidi amesema Serikali inakemea vikali vitendo vya kupiga picha udhalilishaji na kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kufanya hivyo.