Dar es Salaam. Shahidi wa tatu katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kuiba Sh90 milioni, Jones Rugonzibwa (57) ameeleza jinsi alivyoshuhudia bosi wake akilia muda mfupi, baada kuachiwa na askari ambao walikuwa wamemshikilia kwa zaidi ya saa saba eneo la Kurasini, wakishinikiza awapatie fedha.
Rugonzibwa ameyasema hayo leo Mei 31, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini hapa, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi, wakati kesi hiyo inayowakabili washtakiwa watano wakiwemo waliokuwa askari polis.
Shahidi huyo ambaye ni Meneja Uendeshaji kutoka kampuni ya RHG General Traders Ltd, amedai Grace Matage ambaye ni bosi wake, alimwambia kuwa askari hao walimshikilia kwa muda wakimshinikiza awapatie fedha kwa madai ya kughushi nyaraka.
Hata hivyo, bosi wake huyo aliwapatia Sh90 milioni badala ya Sh200 milioni walizokuwa wanataka na hivyo wakamwachia.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 197/2023 ni waliokuwa askari kanzu watatu mwenye namba F 7149 D/Coplo Ramadhani Tarimo (42) maarufu kama Rasta mkazi wa Kipawa; G 7513 D/Coplo Majid Abdallah (35) na mkazi wa Kunduchi na WP 6582 D/ Coplo Stella Mashaka (41) mkazi wa Railway.
Wengine ni waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya RHG General Traders Ltd, Ashiraf Sango (31) na Emmanuel Jimmy (31), wote wakazi wa Dar es Salaam.
Akiongozwa kutoa ushahidi na wakili wa Serikali, Neema Moshi, shahidi huyo amedai Agosti 28, 2023, saa 4 asubuhi akiwa ofisi wake eneo la Mnazi Mmoja walifika watu zaidi ya wanne na kuingia katika ofisi ya Matage.
“Baada ya hao watu kuingia ofisini kwa bosi wangu na kuongea nao kwa muda, bosi wangu alitoka ofisini kwake na kuja ofisi kwangu na kuniambia, wale unao waona pale ni askari wanataka twende polisi, hivyo naomba unisindikize,” amedai Rugonzibwa.
Amesema walipanda magari mawili meusi yaliyofunikwa madirishani, aina ya Toyota Vanguard na wengine Toyota Mark X.
“Baada ya kupanda gari, msafara ulianza hadi Kituo cha Polisi Msimbazi na tulipofika, Grace alipitishwa mlango wa nyuma na aliongozana na Stella, huku mimi nikiendelea kubaki ndani ya gari pamoja na dereva wao,” ameeleza.
Amedia kuwa bosi wake aliambiwa anatakiwa kwenda kutoa maelezo, hivyo waliongozana na Stella (mshtakiwa wa tatu) hadi ndani.
“Nikiwa ndani ya gari na dereva pamoja na mtu mwingine ambaye alikuwa amevaa kibaragashia, nilimuuliza hakuna utaratibu wa kumpa dhamana bosi wangu? Niliambiwa subiri, na baadaye niliambiwa tunahama kiwanja tunaenda sehemu nyingine.
“Baada ya muda, Stella na Grace walirejea kwenye gari na tukaanza safari ya kwenda Barabara ya Kilwa eneo la Kurasini na walipofika huko, Grace na wale askari walikaa tofauti na sisi,” amedai Rugonzibwa.
Amedai wakiwa wanaelekea Kurasini karibu na Ofisi za Uhamiaji, waliongozana na Majid, Dustan, Stella, Deo Mugasa Didier pamoja na wengine ambao walikuwa wamepanda gari lingine.
Aliendelea kudaiwa kuwa wakiwa Kurasini, watu hao walikuwa wanazunguka zunguka eneo hilo, huku Deo akiwa amevaa bastola kiunoni na wakati mwingine alikuwa akiitoa kiuno na kuishikilia mkononi na kumtaka Grace atoe fedha, ndipo aachiwe wakidai kuwa ana kesi ya kughushi nyaraka.
Ameendelea kudai kuwa baada ya muda, alimuona mmoja wa wafanyakazi wenzake aitwaye Shafii eneo hilo na alipomuuliza amekuja kufanya nini, Shafiii alimjibu ameleta fedha.
Baada ya majadiliano ya muda mrefu, Grace aliachiwa na watu hao na hivyo akamwambia Rugonzibwa waondoke eneo hilo.
“Bosi wangu (Grace) aliachiwa saa 12 jioni tangu saa tano asubuhi alipokamatwa na alitoka eneo hilo akiwa Analia. Aliniambia walikuwa wamemkamata ila kwa sasa wamemwachia, hivyo aliomba waondoke,” ameeleza.
Alipoulizwa alipata taarifa lini za bosi wake kuibiwa fedha na watu hao, alijibu kuwa baada ya muda (hakuutaja) Grace alimwambia wale watu waliompeleka Kurasini walimwibia Sh90 milioni.
Shahidi huyo aliwatambua washtakiwa katika kesi hiyo ambao walienda ofisi kwake, Kurasini kuwa ni Tarimo ambaye alikuwa na amesokota nywele wakati huo, Majid na Stella.
Pia alimtambua Ashiraf na Emmanuel ambao walikuwa wafanya kazi wenzake, kabla ya kufukuzwa kazi na ofisi kutokana na utovu wa nidhamu.
Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili wanne ambao ni Peter Kibatala, anayemtetea Stella, Wakili Method Ezekiel anayemtetea Tarimo na Majid, Aliko Mwamanene anayemtetea Ashraf huku Baraka Katale akimtetea Emmanuel.
Ifutayo ni sehemu ya maswali aliyoulizwa na Kibatala:
Kibatala: Mzee wangu shikamoo.
Kibatala: Kule Kurasani mlipokuwa mmekwenda ulimpigia simu mtu yoyote kumweleza hicho kilichokuwa kinaendelea pale?
Kibatala: Bila shaka ulipokuwa eneo lile hukufukuzwa wala hukunyang’anywa simu.
Shahidi: Sikufukuzwa ila niliambiwa nikae mbali na wale watu, ndio maana hata kilichokuwa kinazungumzwa na wao nilikuwa sisikii.
Kibatala: Unakumbuka uliandika lini maelezo Polisi?
Shahidi: Sikumbuki Mheshimiwa.
Kibatala: Bosi wako alinyanganywa simu?
Wakili Katale yeye alimuuliza shahidi maswali yafuatayo:
Katale: Ofisi ya bosi wako inatenganishwa na kioo, ni sahihi?
Katale: Uliona watu wangapi wanaingia ofisini kwa bosi wako?
Shahidi: Niliona zaidi ya wanne
Katale: Siku ile ulikuwa sawa?
Shahidi: Ndio, nilikuwa sawa ila nilikuwa nimechoka sijalala na nilikuwa na njaa. Halafu mimi akili yangu ipo sawa, hata siku ile ilikuwa sawa na mpaka sasa niko sawa.
Hakimu Msumi baada ya kusikiliza ushahidi huo, aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 14, 2024 itakapoendelea na washtakiwa wamerudishwa rumande kwa kuwa shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha halina dhamana.