Simba yamuandalia ‘sapraizi’ Bocco | Mwanaspoti

UONGOZI wa Simba umefunguka namna nahodha  wa zamani, John Bocco alivyokuwa na jukumu la kusaidia kutuliza migomo na kuongoza wachezaji wenzake nje na rekodi ya kutwaa mataji manne.

Bocco amedumu miaka saba kikosi cha Simba baada ya kujiunga msimu wa 2017/18 na kutwaa mataji hayo ya Ligi Kuu na kuisaidia kucheza robo fainali tano za michuano ya CAF, nne zikiwa za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho.

Akizungumza na Mwanaspoti, mjumbe wa Bodi, Issa Masoud alisema wanatambua juhudi na mchango wa mchezaji huyo na kwamba watafanya jambo ili kumuaga.

“Bocco alikuwa sio mchezaji tu, bali kiongozi katusaidia sana kutuliza timu na kuongoza wenzake kwenye mazingira yote ya furaha na matatizo,” alisema Masoud na kuongeza:

“Sio rahisi kumuacha aende zake bila kumfanyia kitu chochote nafikiri kuna kitu kitafanyika lakini siwezi kusema ni lini taarifa itatoka hapo baadaye.”

Kabla ya kutua Simba, Bocco aliitumikia Azam kwa misimu tisa mfululizo akishiriki pia kuipandisha Ligi Kuu 2008.

Akiwa Simba alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo, Ngao ya Jamii na Kombe la FA pia akiifikisha Simba katika robo fainali tano tofauti katika misimu sita ya michuano ya CAF.

Kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda alisema Bocco ataishi kama shujaa aliyefanya mambo makubwa Tanzania.

Mgunda alifichua kuwa uamuzi aliouchukua nyota huyo kustaafu soka na kusomea ukocha ni ushauri wake, huku akikiri kuwa anajivunia kuwa mmoja wa makocha waliomfundisha.

“Ukimtafuta na kumuuliza kuwa nani alimshauri asomee ukocha atanitaja. Ni kijana wangu mbali na kumfundisha amekuwa muungwana, msikivu. Namtabiria kuwa atakuja kuwa kocha bora miaka ujayo,” alisema.

“Bocco ni mchezaji kiongozi na ndio maana mara nyingi timu alizopita alikuwa nahodha kwa sababu ni mchezaji ambaye anaweza kuishi na kila mtu na ni mwepesi wa kuelekeza mtu akaelewa.”

Mgunda alisema Bocco ni mchezaji ambaye ataendelea kuishi mioyoni mwa Taifa na sio Simba tu kwa sababu mambo makubwa aliyoifanyia hii nchi sio kwa upande wa klabu tu bali hadi timu ya taifa ‘Taifa Stars’

Related Posts