Sumaye: Kama kuna mahali kutaharibika basi ni sisi huku chini tumezembea

Katesh. Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye ameichambua safu mpya ya Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya Katibu Mkuu, Dk Emmanuel Nchimbi akisema iko imara kukipa ushindi chama hicho katika chaguzi zijazo na ikitokea vinginevyo, viongozi wa chini wanapaswa kuwajibishwa.

Sumaye amesema hilo halina ubishi na kwa sasa hakuna mtu kama Samia Suluhu Hassan, iwe ndani au nje ya CCM, anayeweza kuongoza nchi hii kwa ustadi mkubwa.

Sumaye amesema hayo leo Ijumaa, Mei 31, 2024 katika mkutano wa hadhara wa Dk Nchimb,i uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Katesh, Hanang, Mkoa wa Manyara.

Dk Nchimbi amewasili mkoani Manyara kuendelea na ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Ilani, kusikiliza kero za wananchi na kuangazia maandalizi ya uchaguzi zijazo za serikali za mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

Ziara hiyo imeanzia Singida, kisha Manyara na atakwenda Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Katika mkutano huo, Sumaye amesema kwa nafasi mbalimbali alizoshika Dk Nchimbi ndani ya Serikali, kuwa Balozi na timu inayomzunguka, hana shaka naye juu ya kuipa CCM ushindi katika chaguzi zijazo.

Mbali na Dk Nchimbi, wengine waliomo kwenye Sekretarieti ni Naibu Katibu Mkuu-Bara, John Mongella na Katibu wa Itikadi Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ambao wameteuliwa pamoja na Halmashauri Kuu ya CCM kushika nafasi hizo Januari 15, 2024

Katika mkutano huo, Sumaye amesema “hiyo timu ni ya kuvusha salama.

“Kwa vile timu ya juu tunaiamini, basi huko chini mambo yakiharibika ni sisi huko chini kuna shida. Kama unasema tutashinda na ikatokea tukashindwa, basi lazima tuulizane shida ni nini.

“Nikuhakikishie katibu mkuu, Mkoa wa Manyara, wanakipenda Chama cha Mapinduzi. Kama kuna mahali kutaharibika basi ni sisi huku chini tumezembea. Wote tunakiri katika historia ya nchi hii, katika kipindi hiki fedha nyingi sana zimetolewa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema.

Sumaye ambaye mwaka 2015 alitimkia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na baadaye kurejea CCM, amesema chama hicho kimetimiza wajibu wake kutunga ilani inayotekelezeka, Serikali imeichukua na inaitekeleza vizuri.

“Kama kutatokea sijui kuna kata, vijiji, sijui jimbo limepotea, kura za Rais zimepatikana chache, tutakuwa hatujatimiza wajibu wetu. Sisi wazee wa mkoa, viongozi wa chama tutimize wajibu wetu,” amesema.

Katika kusisitiza hilo, Sumaye amesema:”Hakuna mtu anayeweza kuongoza nchi hii zaidi ya Samia Suluhu Hassan, hata si nje ya CCM, hata ndani ya CCM hakuna anayeweza kuongoza hii nchi kama mama anavyoongoza.”

“Kama hamtazami vizuri, basi tazameni vizuri, huko nje (upinzani) hawajapata madaraka wanaparuana, wakipata madaraka si tutakoma? Kwa hiyo hakuna kama CCM na hakuna kama Samia Suluhu Hassan,” amesema Sumaye.

Kufuatia kauli hiyo, Makalla amesema, kama Sumaye ambaye amekuwa na uzoefu mkubwa wa siasa ndani na nje ya CCM na ameona Samia anatosha, “sasa mimi na wewe tuna cha kuongeza kweli? Yaani kwa uzoefu wake amesema haoni kama Samia.”

“Katika awamu hii, mama amefanya makubwa, ndio maana hata Sumaye amesema hakuna wa kushindana naye. Hatutaiba kura, tutawashinda kwa anayoyafanya,” amesema Makalla.

Makalla amesema chama hicho kimejipanga kupeleka maeneo mbalimbali wagombea wazuri wanaokubalika kwa wananchi katika udiwani na ubunge.

Kauli kama ya Sumaye ilitolewa Desemba 8, 2022 na mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete katika mkutano mkuu wa 10 wa CCM jijini Dodoma.

Kikwete ambaye ni Rais mstaafu alisema haoni mwanachama mwingine ndani ya CCM atakayewania urais mwaka 2025 zaidi ya Rais Samia.

“Mheshimiwa Rais, usisikilize porojo za watu kwamba sijui kuna kijana gani au mzee gani atagombea, ni upuuzi mtupu, sio kwamba nawazuia, lakini simuoni mwana CCM atakayechukua fomu kukupinga mwaka 2025, labda mambo yaharibike sasa hadi wakati huo.

“Lakini siombei iwe hivyo, si mila yetu, lakini niseme ukweli hapa Tanzania leo kuna mwanasiasa maarufu kumshinda Samia? Hayupo ndani ya CCM wala nje ya chama hiki, usibabaishwe na maneno haya,” alisema Kikwete.

Kikwete alimtaka Rais Samia kutobabaishwa na maneno yanayozungumza bila kuwa na ushahidi.  

 “Uongo mtupu, ninachowaombeni ndugu zangu, acheni uongo, katika kipindi cha kuelekea uchaguzi huu ukisoma mitandao maneno ni ovyo ovyoo… ambayo yote ya kutunga.

“Mara fulani sijui yupo hivi, anaungwa mkono na mzee huyu, ni upuuzi mtupu, tuache hii tabia inakigawa chama chetu bila sababu,” alisema.

Related Posts