Mwaka 1982 nilifika Mbagala. Kwa sasa sina kumbukumbu nzuri ya kitongoji hicho jinsi kilivyokuwa.
Tulisafiri kwa basi la UDA mpaka mahala fulani (sijui ni Kurasini pale?), baada ya hapo tulichapa malapa hadi tuliposimama kwenye nyumba pweke kuomba maji ya kunywa. Tukapiga tena mguu hadi kwenye mti uliloanguka, tukapumzika.
Mwanzoni tulikutana na mtu mmoja mmoja na kumuuliza kama hatujapotea njia. Baada ya mwendo mrefu tulingiia porini ambako tulipishana na panya buku, nguchiro, ngiri na wanyama wengine wadogo.
Baada ya hapo ndipo tukaingia kwenye kijiji cha wakulima. Nyumba zao ziliachana kwa urefu wa kiwanja cha mpira, na zilijengwa katikati ya mashamba.
Mwaka 1993 tulihamia Buza. Nina uhakika zaidi ya nusu ya wasomaji wangu wote mlikuwa hamjapata kulisikia jina hilo nyakati zile. Ili kufika Buza katika kipindi hicho ilikupasa kupanda basi la Tandika, ushukie Davis Corner.
Hapo ungetembea msituni kwa kadiri ya Kilometa saba kabla ya kuingia Buza. Ni sehemu nzuri iliyosheheni miembe na mikorosho, lakini haikuwa na barabara wala umeme.
Wakati huo mimi na wazazi wangu tulidamka alfajiri kwenda Tandika kusubiri mabasi ya kwenda Posta ili kuwahi kazini. Tulisubiriana na wafanyakazi wenzetu hadi tulipotimu watu watano au zaidi.
Pale msituni palikuwa si salama sana kwani tulishawahi kukutana na fisi, chatu na wanyama wengine hatari.
Kuanzia mwaka 1995 Hayati Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi alitusaidia kuchonga barabara.
Sasa tukaanza kusafiri na magari madogo maarufu kama “Chai Maharagwe” kutoka Yombo Makangarawe (au Kwa Kimwaga). Zilitupunguzia safari kwa kuwa sasa tulitembea nusu kupanda “Chai Maharagwe”.
Baadaye mabasi makubwa yakaanza kufika Buza. Sasa ungepanda basi kubwa lingekufikisha hadi nyumbani. Lakini mabasi hayo yalikuwa machakavu sana na mengine yalikosa hata breki. Na kwa sababu ilitupasa kuvuka vilima viwili vya hatari, tulilazimika kuteremka kutoka kwenye basi na kuvivuka kwa miguu.
Siku moja tulipanda basi liliondeshwa na dereva mzoefu wa magari ya aina hiyo. Akatuondoa wasiwasi kuwa haina haja ya kuteremka kwani basi lake lilikuwa na “pulling” ya kutosha. Aliliteremsha salama hadi bondeni, akapachika gia namba moja na kulipandisha hadi Yombo Shuleni. Abiria wote tulimshangilia na kuamini adha ile sasa imekwisha.
Kwenye kilima cha pili kuelekea Kwa Mama Kibonge akarudia mtindo ule. Basi lilipanda lakini likaishiwa nguvu kabla ya kufika juu. Abiria sasa wakafunga midomo na kusubiri hatima.
Haikuwezekana tena kuteremka kwani basi halikuwa na breki. Likarudi kwa kasi, na kwa sababu barabara haikuwa ya kokoto wala lami, tuliingia bondeni na kupindukia kwenye mahala panapojulikana kama Sola Pawa kwa sasa.
Mmoja wetu akaropoka: “Ah! Mimi nilijua tu haya yatatokea”. Kwanza hakuna aliyemjali kwani kila mmoja alihangaika kuokoa roho yake. Kwa bahati njema wote tulifanikiwa kutoka salama ukiachilia waliopata majeraha madogo.
Lakini mzee mmoja aliyechubuka mkono alikuwa bize akichunguza sura zetu. Akafanikiwa kumpata aliyemtafuta:
“Enhe… wewe ulijua kuwa yatatokea. Ni kwa nini hukutuambia?” kwanza kila mmoja aliangua kicheko. Lakini mzee alikuwa mkali kupita maelezo: “Umejua kuwa tupo hatarini. Kwa nini ukakaa kimya? nakuuliza wewe!”
Jamaa alijitetea kuwa aliliona basi lilivyozidiwa kwenye mlima wa mwanzo. Hata hivyo mzee aliinama kuokota bakora, akarudia swali lake: kwa nini hukusema ili tuteremke? waungwana tukawahi kumhamisha yule jamaa kabla hajaikoga ile bakora.
“Nilijua” linaweza kuwa neno la hatari sana ukizingatia “Kitendo Mwana Majuto Mjukuu”. Inawezakana kabisa kuwa jamaa alijua kuwa tungeweza kupata ajali.
Mara nyingi tunaambiwa kuwa tumkataze dereva anayeendesha kwa fujo barabarani. Lakini tunakaa kimya hadi ajali inapotokea, kisha tunasema “mimi nilijua tu.”
Katika kipindi hiki tunachoelekea kuwachagua viongozi wetu, wapo watu wanaojua kuwa mgombea fulani ni hatari kwa mustakabali wa maendeleo yetu.
Watu hawa watakaa kimya bila kunong’ona, na pengine watamuunga mkono mgombea huyo pengine baada ya kulewa milungula. Lakini 1itakapotokea la kutokea watasema: “Sisi tulijua tu…” Si jambo jema hata kidogo.
Wapiga kura wanaweza kuweka kando itikadi zao, wakaketi pamoja kuyaangalia matatizo yao kwa ujumla wao.
Wanaweza kuona ni kitu gani wanachohitaji na kuwajadili wagombea mmoja baada ya mwingine. Tunda jema halikosi kutambulika kwa rangi yake, harufu yake na mti wake. Mtu mmoja anaweza kuwadanganya baadhi ya watu kwa muda fulani tu lakini si watu wote kwa wakati wote.
Aliyekwisha kujua atuambie ili nasi tuchanganue. Ukituacha tuingie shimoni na kusema “nilijua tu” tutafanya kama ambavyo babu alitaka kumfanyia yule jamaa aliyejua bila kututahadharisha.