Kibaha. Zaidi ya wananchi 100 katika Kata ya Pangani Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani ,wamekosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa na tingatinga leo Mei 31, 2024.
Wakati wananchi hao wakisema hawakupewa taarifa ya ubomoaji huo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Fokas Bundara amesema ni wavamizi na kwamba walipewa taarifa na taratibu zote zilifuatwa.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 31, 2024 kwenye eneo la tukio, wananchi hao wamesema kuwa shughuli ya ubomoaji wa nyumba zao umeanza alfajiri wakiwa wamelala jambo ambalo limewashitua, wakidai kutopewa taarifa.
“Makatapila manne yamekuja kutoka halmashauri yakagawanyika na kuanza kuvunja nyumba zetu lakini hatukuwa na taarifa yoyote hivyo tumepata hasara,” amesema Juma Mfinanga.
Mfinanga amesema kuwa utaratibu walioutumia halmashauri unaashiria kuwa wamewavamia wananchi hao kwa kuwa taratibu za bomoabomoa zinafahamika ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa wahusika kabla ya utekelezaji.
“Niko kwenye wakati mgumu sana sijui nitakwenda wapi nyumba nimeijenga kwa miaka minne hadi kukamilika leo hii imebomolewa na nina familia,” amesema.
Amesema kuwa eneo alilojenga nyumba yake hiyo ambayo imebomolewa alinunua tangu mwaka 2000 na alipoanza ujenzi hakuwahi kupata barua yoyote ya zuio lakini ameshangazwa leo kuvunjiwa bila taarifa.
Kwa upande wake Saida Msengi amesema kuwa bomoabomoa hiyo imewaacha kwenye wakati ngumu hasa kwa kukosa makazi hivyo hawajui watakwenda wapi.
“Hapa sisi tumevamiwa tumevunjiwa haiwezekani mtu aje akuvunjie bila kukupa taarifa yoyote tumepata hasara kubwa sana,” amesema.
Kwa upande wake Peter Kilia amesema kuwa eneo hilo alinunua tangu mwaka 2015 na kuanza kuishi mwaka 2020 alipokamilisha ujenzi, lakini hakuwahi kusikia kama kuna mgogoro wowote na ameshangazwa kubomolewa leo.
Amesema kuwa ombi lao kwa Serikali ni vema ikaangalia uwezekano wa kuwasaidia ili waendelee kuishi ndani ya eneo hilo kwa kuwa wamedumu kwa miaka mingi sasa.
“Wote hawa unaowaona waliuziwa haya maeneo sasa kama kuna kitu nyuma hatujui hivyo ombi kwa serikali ni vizuri watuangalie ikiwezekana watu waendelee kuishi hapa,” amesema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Dk Rogers Shemwelekwa alipoulizwa kwa simu kuhusu ubomoaji huo, amesema hawezi kulizungumzia kwa kuwa yuko safarini kwenye msiba.