Wataja vikwazo vinne elimu ya ufundi

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwa imeanza utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 pamoja na Mitaala mipya kwa elimu ya Sekondari, wadau wametaja vikwazo wa utoaji wa elimu ya amali ikiwamo ufinyu wa bajeti.

Pia, wametaja kutoandaliwa kwa walimu kufundisha mitaala hiyo, ukosefu wa miundombinu na vifaa, uelewa mdogo wa wazazi na Serikali.

Akitoa mada katika tamasha la kitaaluma la Mwalimu Julius Nyerere la 15, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo Mei 31, 2024, mtaalamu wa elimu, Dk Joel Kayombo amesema lengo la elimu ya amali katika sera hiyo ni kuongeza ujuzi na kukabili tatizo la ajira kwa vijana.

Mada hiyo ilikuwa ikieleza kuhusu ujio wa sera mpya na mitalaa mipya kama itatatua tatizo la ujuzi na ajira kwa vijana.

Amesema awali, Mwalimu Julius Nyerere alianzisha Sera ya Ujamaa na Kujitegemea na Elimu ya Kujitegemea ili kuwapa wanafunzi elimu kwa vitendo.

“Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni walikataa watoto wao wasipewe kazi shuleni, wanasema mtoto wangu hakuja kulima, amekuja kusoma,” amesema Dk Kayombo akijenga hoja ya uelewa mdogo wa wazazi kuhusu elimu ya amali.

Akizungumzia ongezeko la tahasusi kutoka 16 hadi 65, Dk Kayombo amesema kuna chablngamoto ya uelewa wa serikali, kwamba wale wanafunzi wasio na uwezo ndio wanapelekwa kwenye elimu ya amali.

“Changamoto nyingine ni kuwapeleka watoto wenye ufaulu wa chini kwenye elimu ya amali, huku waliofaulu zaidi wakienda elimu za juu,” amesema.

Kuhusu bajeti ya uwekezaji katika elimu, Dk Kayombo amesema imekuwa ikishuka kila mwaka.

“Kwa mfano 2017 ilikuwa asilimia 24.4 lakini mwaka 2022 ilishuka kadi asilimia 14.3. Inatakiwa kuweka walau asilimia 20 ili kufikia malengo ya 2030,” amesema.

Ameitaka Serikali itazame namna ya kugharamia elimu ya amali hasa kwenye mafunzo kwa vitendo.

“Changamoto ya miundombinu, kunatakiwa kuwa na karakana, je vitapatikana?”

Ametaja pia suala la uaandaaji walimu akisema wengi hawjaanðaliwq kufundisha mitalaa ya amali

Akichangia mada hiyo, Mwenyekiti wa Haki Elimu, Dk Wilberfoce Meena amesema licha ya Serikali kuanzs kutekeleza mitalaa ya umahiri tangu mwaka 2005, bado hakujawa na mafanikio.

Ameshauri kuwepo kwa mabadiliko ya mfumo ili kutekeleza mtalaa mpya.

“Hivi tunaweza kufanikiwa na mafanikio ya kielimu bila kubadilisha mifumo? Ni sawa na kuchukua mvinyo mpya na kuweka chupa ya zamani,” amesema.

Katika kuwaandaa walimu, ameshauri walimu wapewe uhuru katika ufundishaji bila kubanwa na taratibu za mitalaa.

“Mtalaa wa umahiri na ratiba zetu darasani, zamani vipindi vya elimu ya awali vinachukua dakika 20 na elimu ya msingi dakika 40.

“Wakati mwalimu anafunzisha umahiri, kabla hajamaliza kucheza na watoto, dakika zimeisha, anakuja mwalimu mwingine, mwanafunzi anatakiwa afunike daftari afungue lingine.

“Je, hatuwezi kuwa na utaratibu wa mwalimu mmoja kufundisha masomo yote? Baadhi ya nchi zinafanya hivyo na zinafanikiwa. Kwetu walimu hawana uhuru,” amesema.

Akifafanua zaidi, Profesa Meena amesema hata mitalaa iliyopo inaelekeza kuwa na miongozi na kitabu cha kiada kinachofanana nchi nzima.

“Walimu hawana uhuru. Hata nchi haifanani, kuna milima na mabonde.

Ipo haja ya kuwapa walimu uhuru wa kufundisha.

“Hatuoni haja ya kuwa na vitabu vingi ili kuwa na upana wa maarifa?” amehoji.

Amesema licha ya lengo la kuwajengea wanafunzi fikra tunduizi, lakini si rahisi kukuta mwalimu akiwa rafiki na mwanafunzi na bado kuna adhabu ya viboko.

Kuhusu uelewa wa wazazi, amesema wengi hawaelewi.

“Tunawajengea watoto elimu ya umahiri, kuuliza maswali, lakini wazazi wanachotaka kujua ni mtoto amekuwa wa ngapi? Amefanya home work (kazi za nyumbani)?”

Kuhusu kuwandaa walimu, amesema kuna changamoto ya lugha katika kuwafundisha walimu,.

“Kwa bahati mbaya vitabu vya kufundisha walimu vimenadikwa Kiingereza na havikuandikwa na Watanzania hivyo havina uhalisia wa mazingira ya ya kisaikolojia na kisaikolojia.”

Ameshauri walimu wawe na bodi ya kitaaluma ya kuwasemea.

Akichangia mjadala huo, Salha Aziz wa Binti Salha Foundation amesema wakati Serikali ikitekeleza mtalaa wa umahiri, bado hakuna mwendelezo.

“Kwa mfano watoto wanaosoma shule za ufundi, wakienda kidato cha tano wanachana na ufundi na wanashika masomo mengine.

“Wanaokwenda masomo ya ufundi ni wale waliofeli na hata wanapokwenda Veta, (Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi), hawapati ajira.

Amesema kuondolewa kwa somo la uraia na kuletwa kwa somo la historia na maadili kutawapunguzia wanafunzi uelewa wa demokrasia.

Kwa upande wake Dk Ave Avemaria Semakafu amekosoa uupatikanaji wa udhibiti ubora.

“Wadhibiti wa ubora wamepitia mrengo gani? Zamani walipokuwa wakaguzi walikuwa wanachagua walimu wenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10 na walio bora.

“Vinginevyo mkaguzi atamkagua aliyemzidi uzoefu.”

Kuhusu elimu bila malipo, amehoji sababu ya Serikali kuendelea kutoza ada ya mitihani kwa shule binafsi.

“Tumeshaamua elimu bure kwa nini tuendelee kutoza ada za mitihani kwa shule binafsi? Wale wa Veta hawapati ajira kwa sababu hawafanyi mtihani kwa sababu ya kukosa hela,” amesema.

Related Posts