Moshi. Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Kanda ya Moshi, imewahukumu kifungo cha maisha jela, Abdalah Halfan Mkwizu na Samwel Eliud Lyakurya wakazi wa Rombo, baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha kilo 690.767 za dawa za kulevya aina ya mirungi.
Mbali na kifungo hicho, Mahakama hiyo imeamuru kutaifishwa kwa gari aina ya Toyota Mark 11 lililotumika kusafirisha dawa hizo kuwa mali ya Serikali.
Hukumu ya kesi ilitolewa Mei 29, 2023 na Jaji, Jaji Elineza Luvanda.
Katika hukumu huyo, Jaji Luvanda amesema Mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 15 (1) (A) cha Sheria ya Upambanaji na Udhibiti wa dawa za kulevya namba 15 ya mwaka 2015, kama ilivyofanyiwa marekebisho ya kifungu cha 8 cha sheria ya Udhibiti na Upambanaji wa dawa za kulevya sheria namba 15 ya mwaka 2017.
Akirejea mwenendo wa shauri hilo, jaji amesema Desemba 6, mwaka 2017 watuhumiwa hao wakiwa katika eneo la Marangu Kitowo, Wilaya ya Rombo walikutwa wakisafirisha dawa hizo kwa kutumia gari aina ya Toyota Mark 11 .
“Washtakiwa walikuwa wakisukuma gari lililokuwa limekwama kwenye matope kutokana na mvua iliyokuwa ikinyesha, Washtakiwa hao waliomba msaada kwa aliyekuwa diwani wa eneo hilo, Dionis Happymark Shirima na hapo ndipo askari waliokuwepo doria walifika kwenye gari hilo na kubaini lilikuwa na dawa hizo za kulevya.”
Baada ya kusikiliza mashahidi wa pande zote mbili, Jaji amesema Mahakama imejiridhisha pasipo na shaka kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo na hivyo walitiwa hatiani kwa kuhusika na usafirishaji wa dawa kulevya.
“Kwa mshtakiwa wa kwanza na wa pili wametiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kinyume na sheria na hivyo kuhukumiwa adhabu hiyo.
“Mahakama hii imejiridhisha pasipo shaka kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo na mshtakiwa wa kwanza na wa pili wanahukumiwa kifungo cha maisha jela, pia Mahakama imeamuru gari aina ya Toyota Mark 11 lenye namba za usajili T656 BYA ambalo lilitumika kusafirisha dawa hizo linataifaishwa na kuwa mali ya Serikali,”
Upande wa Jamhuri uliongozwa na mawakili wa Serikali Marietha Maguta na Bora Mfinanga na washtakiwa wakitetewa na Denis Maro na Rashid Shaban.