Arusha. Serikali imewataka wazalishaji na wasambazaji wa rasilimali na vyakula vya wanyama kuhakikisha vyakula na viwanda vyao vimekaguliwa na kufikia ubora na usalama unaohitajika.
Kauali hiyo ya Serikali imekuja baada ya wazalishaji wa vyakula vya mifugo kubaika kutowasilisha sampuli za vyakula wavyotengeza kwa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA),
Dosari nyingine iliyobainika ni vifungashio vya vyakula kutokuwa na tarehe ya utengezwaji, siku ya mwisho wa matumizi na vingine kutowekwa jina la kampuni iliyotengeneza chakula.
“Wanaopuuza suala la kupima na kuhuisha usajili wa viwanda vyao watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama,” amesema Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka TVLA, Dk Zacharia Makondo.
Dk Makondo ameyasema hayo leo Mei 31, 2024 jijini Arusha wakati wa kuhitimisha ziara ya kikazi ya siku tatu ya wakaguzi wa vyakula vya mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na TVLA, baada ya kufanya ukaguzi katika baadhi ya viwanda, wauzaji wa vyakula vya mifugo na kuwatembelea baadhi ya wafugaji wanaotumia vyakula hivyo.
Ukiwa ni utekelezaji wa sheria, Dk Makondo amesema wote ambao hawajasajiliwa watafungiwa kufanya shughuliza za uzalishaji na uuzaji wa vyakula vya wanyama.
Ili kuwabaini wanaokiuka sheria, amesema maabara za kanda zitawezeshwa kuwa na vifaa vya kufanya ukaguzi katika maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa wa kufanywa kwa ukaguzi wa rasilimali za vyakula vya mifugo na vyakula ili kuimarisha usalama.
Aidha, amesema baada ya kufanya program hiyo kwa ufanisi katika Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kaskazini, watahamia kanda zingine kuendelea kukagua na kufanya uchambuzi wa vyakula na rasilimali za vyakula vya mifugo.
Mtaalamu wa Mifugo, Idara ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Theodata Sallema, amewakumbusha wakaguzi kufanya ukaguzi katika maeneo yao na kuhakikisha wadau wanafuata sheria.
Sallema ameeleza kuwa wafungaji wa vyakula vya mifugo kuhakikisha wanakuwa na nembo na maelezo ambayo yanaendana na mfuko wa chakula au madini, husika kinyume na hapo ni ukiukwaji wa sheria na ni ishara ya udanganyifu.
Meneja wa TVLA Kanda ya Kaskazini – Kituo cha Arusha, Dk Rowenya Mushi amesema kanda hiyo inayohudumia Arusha, Manyara na Kilimanjaro imepata chachu ya kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa wazalishaji na wasambazaji wa vyakula vya mifugo juu ya kupima vyakula vyao kuwa na ubora na kuleta matunda kwa wafugaji.
“Chakula bora huwa kinaleta mazao bora kwa wafugaji na hilo ndio lengo kuu la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Serikali kwa ujumla, kuhakikisha mfugaji anafuga kisasa na kupata chakula bora kwa ajili ya mifugo yao, hatimaye kupata mazao bora na kipato kizuri zaidi,” amesema.
Dk Mushi amewasihi wazalishaji wa vyakula vya mifugo kufikisha sampuli ya vyakula vyao katika maabara ya TVLA katika kila toleo kuhakikiwa ubora na kupatiwa elimu na ushauri juu ya vyakula hivyo ili kuleta tija kwa wafugaji.