Arusha. Mahakama Kuu, Masijala ndogo ya Dar es Salaam imemhukumu Said Bakari, kunyongwa hadi kufa,baada ya kumkuta na hatia ya kumbaka,kumlawiti na kumuua kwa kumnyonga,mtoto wa kike aliyekuwa na umri wa miaka 13.
Hukumu hiyo imetolewa Mei 29, 2024 na Jaji Musa Pomo ambapo katika kesi hiyo ya mauaji namba 120 ya mwaka 2021, Jaji huyo ameeleza upande wa mashitaka na vielelezo walivyotoa mahakamani vimethibitisha makosa dhidi ya mshitakiwa huyo bila kuacha shaka yoyote.
Tukio hilo lilitokea Aprili 19, 2020 katika eneo la Moringe Mbagala wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji amesema upande wa mashtaka kupitia mashahidi wake wanane ulithibitisha kuwa Bakari, aliua mtoto huyo kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
“Ushahidi uliokusanywa kutoka kwa shahidi wa tano na wa nne ambaye ni mtaalamu wa matibabu aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu jinsi mshtakiwa alivyoshikilia shingo ya marehemu kwa nguvu usiku wa manane akimnyonga hadi kufa. Nguvu iliyotumika na sehemu za mwili zilizopigwa inaonyesha wazi kuwa mshtakiwa alikuwa na nia ya kutenda kosa hilo.
“Baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji, kuna hukumu moja tu chini ya sheria, hukumu ya kifo kwa kunyongwa kama ilivyoelezwa chini ya kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu. Kwa kuwa ni msimamo wa sheria, ninamhukumu Bakari, adhabu ya kifo kwa kunyongwa.”ameeleza
Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi,Job Mrema, akishirikiana na mawakili wa Serikali Irene John na Salma Jaffer huku mshitakiwa huyo akitetewa na Wakili Mainda Omary.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa siku ya tukio, mshitakiwa akiwa nyumbani na wanafamilia wengine alikwenda chumbani kwa marehemu na kutekeleza ukatili huo.
Katika ushahidi wa upande wa mashtaka, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo alimtishia mtoto aliyekuwa amelala na marehemu ambaye alikuwa ametokea Nachingwea mkoani Mtwara, na kumtaka kuangalia upande wa pili (ukutani),kisha kumbaka,kumlawiti (marehemu) kabla hajamnyonga hadi kufa.
Shahidi wa kwanza wa mashtaka katika kesi hiyo alikuwa mama wa marehemu alidai kuwa, alipigiwa simu na kujulishwa mtoto wake amefariki huku chanzo cha kifo chake kikidaiwa ni ugonjwa degedege ila baada ya maziko aliitwa katika kituo cha polisi cha Maturubai Kizuiani, kilicho Mbagala jijini Dar es Salaam
Ameeleza mahakama katika kituo hicho cha polisi alielezwa binti yake amefariki baada ya kubakwa, kulawitiwa na kunyongwa na Bakari, ambapo binti yake alikuwa likizo baada ya shule kufungwa kutokana na ugonjwa wa Uviko – 19.
Mama huyo (jina linahifadhiwa), ameieleza mahakama kuwa mwaka 2019 Bakari aliwahi kujaribu kumbaka ndugu wa mke wake na kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 18 na kuwa shahidi huyo aliamini Bakari ameacha tabia hiyo.
Shahidi wa pili katika kesi hiyo ambaye ni mke wa mshtakiwa, aliieleza mahakama kuwa siku Aprili 19, alipokwenda kwenye chumba walichokuwa wamelala watoto hao, alijaribu kumuamsha marehemu ila hakuamka na alipomuomba mshitakiwa msaada.
Bakari alimuuliza nini kimetokea na kutoka nje kuomba msaada ambapo daktari alipomuona aliwaeleza kuwa mtoto huyo amekufa na alikuwa amebakwa.
Alidai kuwa mwaka 2019 alitembelewa na mdogo wake ambaye akiwa nyumbani kwake kwa siku kadhaa alimweleza kuwa mshitakiwa alimtongoza na alitaka wafanye naye mapenzi na kuieleza mahakama kuwa katika eneo walilokuwa wakiishi malalamiko ya majambazi na ubakaji yalikuwepo na hakukuwa na polisi jamii.
Shahidi mwingine ambaye ni shemeji wa mshitakiwa huyo, aliieleza mahakama kuwa alimfahamu mshitakiwa mwaka 2018 ambapo alipokwenda kumtembelea dada yake jijini Dar es Salaam, usiku akiwa amelala alihisi kuna mtu kwenye mwili wake na alipotazama, alimkuta shemeji yake (Bakari).
“Na muda huo tayari alikuwa amenishika sehemu za siri na kuingiza kidole chake, nilipomuuliza, alinijibu wewe ni mtu mzima na si mtoto mdogo, huu akiwa amefunga taulo, nilipokataa matakwa yake, aligeuka kurudi chumbani kwake,”ameeleza shahidi huyo
Ushahidi wa shahidi huyo ulifanana na uliotolewa na shahidi wa tatu ambaye pia ni ndugu wa mke wa mshitakiwa, alidai Bakari aliwahi kuingia katika chumba alichokuwa akilala na kumkuta akimgusa sehemu zake za siri na matiti,na aliposhtuka na kupiga kelele ndipo mshitakiwa akakimbia na asubuhi alipomweleza dada yake(mke wa mshitakiwa) kuwa shemeji yake alitaka kumbaka, dada yake alimwambia anyamaze.
Shahidi mwingine ambaye ni daktari aliyeufanyia uchunguzi wa mwili wa marehemu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Amos Mwakigonja, aliileza baada ya kufanya uchunguzi wa mwili huo alibaini mambo matatu ambayo ni marehemu alikufa kwa kukosa hewa, mwili wale ulionyesha alibakwa na kulawitiwa na kuwa kuna uwezekano mkubwa wakati wa matukio hayo mdomo wa marehemu na pua vilifungwa.
Shahidi wa saba na nane ambao walikuwa maofisa wa polisi waliopeleleza shauri hilo, kwa nyakati tofauti walieleza kuwa baada ya kukamilisha mahojiano ya mdomo, waliunda timu ya uchunguzi ili kubaini aliyetenda kosa hilo ambapo walifanya mahojiano ya kina na watu wote waliokuwa wakiishi katika nyumba hiyo ambapo shahidi wa tano alieleza mshitakiwa ndiye alitenda kosa hilo kwani alimuona kifanya hivyo.
Amedai wakati wa upelelezi wao walibaini nyumbani kwa mshitakiwa kulikuwa na watu tofauti ambao walikuwa wanaishi hapo,na wote waliwahi kulala nyumbani kwa mshitakiwa kwa nyakati tofauti, walipata jaribio la mshitakiwa kutaka kuwabaka na walikuwa ni watu wazima wa zaidi ya miaka 20,hivyo uchunguzi kubaini mtuhumiwa alimbaka, kulawiti na kumnyonga mtoto huyo.
Katika utetezi wake mahakamani hapo, Bakari amedai kuwa siku ya tukio alikwenda kazini kwake Temeke na aliporejea nyumbani mkewe alimwomba pesa kwa ajili ya kwenda kuchukua watoto katika kituo cha mabasi Mbagala (akiwemo marehemu) na asubuhi iliyofuata mke wake alimwita akipiga kelele kuwa kuna tatizo ambapo waliona suruali ya mtoto katika mguu wa kulia umekunjwa, akiwa na damu na kulazimika kumuita balozi wa nyumba kumi na hahusiki na tukio hilo.