Moshi. Mamia ya waombolezaji kutoka ndani na nje ya mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro wamefurika katika Parokia ya Bikira Maria Mtolewa Hekaluni, Katanini, Karanga kuuaga mwili wa Ephagro Msele (43) ambaye aliuawa na mkewe Beatrice Elias (36) akiwa nyumbani kwa mwanamke aliyezaa naye katika Kitongoji cha Pumuani A, Manispaa ya Moshi.
Msele ambaye ni mkazi wa Katanini, kata ya Karanga, Manispaa ya Moshi anadaiwa kuuawa Mei 25, mwaka huu na mkewe baada ya kumvizia akiwa nyumbani kwa mzazi mwenzake huyo na kumshambulia na kitu kinachodhaniwa kuwa ni kisu.
Msele ambaye anatarajiwa kuzikwa leo Jumamosi, Juni Mosi mwaka huu nyumbani kwake, eneo la Katanini, wilayani hapa ameacha watoto saba, wakiwemo watoto sita wa mke wa ndoa na mmoja wa mwanamke huyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Simon Maigwa, tukio hilo lilitokea Mei 25, mwaka huu majira ya saa 3:30 usiku maeneo ya Kitongoji cha Pumuani A akisema tukio hilo, lilihusishwa na wivu wa mapenzi.
Hata hivyo, vilio na simanzi vimetawala nje na ndani ya kanisa hilo wakati mwili wa Msele ukiagwa huku baadhi yao wakizimia kanisani hapo.
Mapdri zaidi ya tisa waliingia kwa maandamano kanisani hapo kushiriki katika misa hiyo ya ibada ya mazishi ambayo inafanyika katika kanisa hilo.