Baada ya kushuhudia Yanga ikichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara na sasa macho ya wapenda soka yapo visiwani Zanzibar kwenye fainali za Kombe la Shirikisho.
Yanga ilitinga fainali baada ya kuichapa Ihefu bao 1-0 likifungwa na kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz KI katika dakika ya 100 huku Azam ikiingia hatua hiyo baada ya kuitandika Coastal Union 3-0 yaliyowekwa kambani na Abdul Suleiman ‘Sopu’ na Feisal Salum.
Fainali hiyo itapigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar ikiwa na rekodi mbalimbali katika michezo iliyopita na mashabiki wa timu hizo ni vyema tu wakaandaa suti mapema ili kusherehekea ubingwa kwani mechi hii, lazima bingwa atapikane iwe kwa dakika 90 au 120 ama kwa penalti.
Tangu michuano hii iliporejea mwaka 2015, Yanga imeingia fainali nyingi zaidi tofauti na timu yoyote ikifanya hivyo mara tano.
Mara nne ilizoingia ni fainali moja tu ambayo haikuchukua ubingwa ambao ni msimu wa 2020-2021, iliponyukwa na watani wao Simba bao 1-0, lililofungwa na Taddeo Lwanga, mechi ikipigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma Julai 25, 2021.
Tangu kuanza kwa michuano hii mwaka 1967 ikifahamika kwa jina la FAT kabla ya 2015 kubadilishwa na kuitwa ASFC, Yanga ndio timu iliyotwaa mara nyingi ubingwa ikifanya hivyo mara saba kuanzia 1967, 1974, 1998, 2001, 2015-2016, 2021-2022 na 2022-2023.
Timu inayofuatia ni watani wao Simba ambao wamechukua taji hili mara nne ikianzia, 1995, 2016-2017, 2019-2020 na 2020-2021.
Kwa upande wa Azam hii inakuwa fainali ya nne kushiriki katika mashindano haya ambapo katika mara tatu ilizotinga imelichukua mara moja tu ikifanya hivyo msimu wa 2018-2019, ilipoifunga Lipuli ya mkoani Iringa bao 1-0, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi.
Mchezo huo uliopigwa Juni Mosi, 2019, bao pekee la Azam lilifungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo Mzambia, Obrey Chirwa katika dakika ya 64.
Msimu huu ulikuwa 50 kwa 50 kwa timu zote mbili kwani kwenye mechi za ligi kila mmoja kashinda kwake.
Mzunguko wa kwanza Oktoba 23,2023 Yanga ikiwa nyumbani ilitembeza kichapo cha mabao 3-2 Aziz KI akifunga hat-trick kwenye mchezo huo na Azam mzunguko wa pili ilipokuwa nyumbani iliitandika Yanga mabao 2-1 yaliyofungwa na Gibril Sillah na lile la Feisal Salum, Machi 17 mwaka huu.
Licha ya Yanga kuonekana bora karibu kila eneo lakini kulikuwa na vita kwa baadhi ya wachezaji wa timu hizo mbili.
Hapa kulikuwa na vita ya winga wa Azam, Kipre Junior aliyemaliza na asisti tisa Ligi Kuu huku mfungaji bora, Aziz KI alimaliza na nane, Lusajo Mwaikenda, Feisal Salum (Azam) na Yao Attohoula na Clement Mzize wakimaliza na asisti saba kila mmoja.
Ukiachana na presha ya nafasi ya pili ambayo ilikuwa ikiwaniwa na Azam na Simba kulikuwa na vita ya ufungaji bora, ambayo mwishowe Aziz Ki alishinda kwa kumaliza na mabao 21 dhidui ya 19 ya Feisal Salum (Azam).