Mwanza. Mungu hamtupi mja wake. Ndivyo unavyoweza kuelezea ushindi wa nafasi ya makamu mwenyekiti alioupata Mariam Mashibe baada ya kuanza kuwaombea wajumbe zaidi ya 300 kisha kutaja sera zake na kuomba kupigiwa kura.
Mariam ambaye ni mkulima wa pamba na mazao mchanganyiko wilayani Kwimba, alikuwa miongoni mwa wagombea 13 wa nafasi tano ya ujumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU 1984).
Akigombea nafasi za mwenyekiti na makamu mwenyekiti, Mariam ameibua shangwe jana Ijumaa Mei 31, 2024 alipoanza kuwaombea wajumbe, kujiombea mwenyewe kisha kuomba kura tofauti na wenzake walivyoanza kuomba kura zao.
“Namshukuru Mungu kwa neema yake ya kuwafikisha salama wajumbe wa mkutano huu mahali hapa, Mungu ni mwema sana na mwaminifu naendelea kumshukuru lakini pia namshukuru kwa kunifikisha mahali hapa salama,
“Wapendwa katika bwana, kwa nafasi hii nimegombea naombeni tumwambie Mungu kwa herufi kubwa ikimpendeza hiyo nafasi niichukue, ili nikakitumikie chama chetu,” amesema Mariamu wakati akiomba kura huku wajumbe wakimshangilia
Baada ya wajumbe wote 13 kuomba kura na kuelezea watachokifanya wakipewa nafasi kwenye bodi hiyo, walipigiwa kura na Mariamu kuwa miongoni mwa wajumbe sita waliochaguliwa kuchuana kwenye nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti kwa kupata kura 358 kati ya kura 391.
Wagombea hao sita walivyopata nafasi nyingine ya kuomba kura ili kupata nafasi hizo, walijinadi kwa sera zao huku Mariamu kama kawaida akianza kumshukuru Mungu na wajumbe kisha kudai yeye angetamani sana kuwa makamu mwenyekiti na kuibua shangwe kwa wajumbe waliosikika wakisema ‘umepata’
Katika kinyang’anyiro hicho wagombea, Fokasi Magumba, Gidion Majima na Leonard Jabalima walichuana kwenye nafasi ya mwenyekiti na hatimaye wajumbe kuamua mwenyekiti wa bodi ya NCU kuwa Leonard Jabalima aliyepigiwa kura 159 kati ya kura 371.
Baada ya mwenyekiti kupatikana muda wa kumchagua makamu wake ulifika, hatahivyo wagombea wengine watatu waliamua kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kuwafanya wajumbe kuibua shangwe kuonesha kukubaliana na uamuzi wao.
Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Kaimu Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mwanza, Leo Zephania licha ya wagombea wengine kujiondoa, alisema lazima wajumbe wapige kura za ndiyo au hapana kama ambavyo taratibu zinavyosema.
“Lazima taratibu zifuate, wajumbe mtapiga kura ya ndiyo au hapana,”alisema Zephania na mchakato wa kura ukaanza.
Kura zilivyopigwa Mariamu aliibuka kidedea kwa kupata kura za ndiyo 367 kati ya kura zilizopigwa 380, za hapana zikiwa tano na zilizoharibika zikiwa nane na kumfanya ashinde nafasi hiyo.
Akianza kutoa sera zake, amesema moja ya kero atakayoishughulikia kwa kushirikiana na bodi pamoja na watendaji wa chama hicho, ni bei ndogo ya zao la pamba wanazolipwa wakulima wanapouza zao hilo, hivyo kuwakatisha tamaa.
Mwakilishi wa wakulima kutoka Chama cha ushirika cha msingi (Amcos) cha Mwanala wilayani Misungwi, Mathias Lufega amesema kilichombeba Mariamu ni kutaja jina la Mwenyezi Mungu kitu kilichowavutia wajumbe.
“Ninampongeza mama aliyepata nafasi ya makamu mwenyekiti kwa sababu alivyokuwa akijinadi sera zake kwa wajumbe zilikuwa zinavutia na hasa kabisa alikuwa anamtanguliza jina la Mwenyezi Mungu ndio maana hata wagombea wenzake aliokuwa akiwania nao walimuachia,”amesema.