KATIKA kuhakikisha kila mmoja anafanya mambo kwa ufanisi ili kubeba ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa tahadhari kubwa ya mpinzani wake asiibe mbinu, timu za Yanga na Azam zimechukua uamuzi wa kufanya mazoezi zikiwa chini ya ulinzi mkali.
Hilo limejiri katika maandalizi ya timu hizo yanayoendelea visiwani Zanzibar kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) utakaochezwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.
Timu hizo ambazo zote ziliwasili visiwani hapa Zanzibar siku ya Alhamisi kwa nyakati tofauti, zimekuwa zikifanya mazoezi kwenye viwanja vya New Amaan Complex B maarufu Kwa Wazee vilivyopo pembezoni mwa Uwanja wa New Amaan Complex.
Tangu siku ya kwanza ya mazoezi ambapo Mwanaspoti limefanikiwa kufika viwanjani hapo, kumekuwa na ulinzi mkali kiasi cha watu wasiohusika kuzuiwa.
Mwanaspoti imeshuhudia namna askari waliowekwa getini wakiwa wakali kuzuia watu wasiingie wala kuchungulia pindi timu hizo zinapofanya mazoezi.
Siku ya pili ya mazoezi kwa timu hizo yaliyofanyika jana Ijumaa, Azam ilikuwa ya kwanza kufika uwanjani hapo saa 10 jioni.
Wakati Azam ikiwa na mazoezi hapo, uwanja mwingine kulikuwa na mechi ya Ligi Kuu Zanzibar kati ya Mlandege dhidi ya Chipukizi United.
Mashabiki waliokuwa wakiingia uwanjani hapo kwa ajili ya kuangalia mechi hiyo ya Ligi Kuu, walikuwa wakifukuzwa pindi wakionekana wakisogelea sehemu ambayo Azam inafanyia mazoezi kwa kile kilicholezwa kwamba hakuna mtu asiyehusika anayeruhusiwa kuangalia kinachoendelea.
“Hapa haturuhusu watu kuangalia mazoezi, tumepata maagizo kutoka kwa Azam hawataki watu waangalie wanachokifanya, ondokeni,” alisikika mmoja wa askari wanaolinda usalama uwanjani hapo akiwafukuza watazamaji waliokuwa bize kufuatilia mazoezi hayo.
Azam ikiwa inaendelea na mazoezi huku pia mechi ya ligi ikikaribia kumalizika, kikosi cha Yanga kikawasili uwanjani hapo majira ya saa 12 jioni.
Yanga baada ya kufika uwanjani kwa ajili ya mazoezi, ilibidi wasubiri hadi mechi ya ligi imalizike ndipo wautumie uwanja huo kwa sababu ule mwingine Azam walikuwa bado hawajamaliza programu zao.
Baada ya mechi hiyo ya ligi kumalizika, askari walichukua jukumu la kuwatawanya haraka mashabiki, wachezaji na viongozi wa timu za Mlandege na Chipukizi ambapo zoezi hilo lilichukua muda mchache lakini mvutano mkubwa ulitokea kwa baadhi ya watu kugoma kutoka uwanjani hapo, lakini baadaye walikubali kuondoka.