Chadema Morogoro mjini wapata viongozi wapya

Morogoro. Baada ya vuta nikuvute ya uchaguzi viongozi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Morogoro mjini, hatimaye chama hicho kimepata viongozi wapya wa jimbo na mabaraza watakaoongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo leo Juni Mosi, 2024, msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu na operesheni kamanda Kanda ya Kati, Patrick Ole Sosopi amemtangaza Pamba Chironge kuwa mwenyekiti wa jimbo hilo.

Ole Sosopi pia amemtangaza Elizeus Rwegasira kuwa katibu wa Chadema jimbo hilo na Gabriel Mdee kuwa katibu mwenezi wa jimbo.

Pia Ole Sosopi amemtangaza Selysius Marumbu kuwa mweka hazina wa chama hicho Jimbo la Morogoro mjini.

Uchaguzi huo pia ulihusisha viongozi wa mabaraza ambapo kwa upande wa Baraza la wazee wa Chadema (Bazecha), Filbert Rushobe ametangazwa kuwa mwenyekiti baada ya kupata kura 62 kati ya 63 zilizopigwa sawa na asilimia 95 ya kura zote.

Naye Charles Kahumbe amechaguliwa kuwa katibu wa Bazecha wa jimbo hilo baada ya kupata kura 60 kati ya 63, huku John Dinya akichaguliwa kuwa Makamu mwenyekiti wa baraza hilo baada ya kupata kura 60 kati ya 63.

Kwa upande wa Baraza la Vijana wa Chadema Bavicha kura zilizopigwa zilikuwa za ndio ama hapana baada ya wagombea kutokuwa na wapinzani, ambapo msimamizi huyo wa uchaguzi amemtangaza Hilda Mbuli kuwa mwenyekiti baada ya kupata kura 76 sawa na asilimia 100.

Msimamizi huyo wa uchaguzi pia amemtangaza Emanuel Mpesa kuwa katibu wa Bavicha baada ya kupata kura 76 sawa na asilimia 100 ya kura zote na pia amemtangaza William Masula kuwa mweka hazina wa baraza hilo naye akipata kura 76 sawa na asilimia 100 ya kura zote.

Wakati huo huo Farida Kyalawa amechaguliwa kuwa ni mwenyekiti wa Baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha) baada ya kupata kura 59 kati ya kura zote halali 59 zilizopigwa na wajumbe wa baraza hilo sawa na asilimia 100.

Pia amemtangaza Doris Mwansasu kuwa  katibu wa baraza hilo baada ya kupata kura 58 kati ya kura halali 59 zilizopigwa na wajumbe wa baraza hilo na pia amemtangaza Faidha Kaswila kuwa mwenezi wa baraza hilo kwa kura 55 kati ya kura 59 zilizopigwa.

Amemtangaza Sarah Manzawa kuwa ni mwekahazina wa baraza hilo baada ya kupata kura 58 kati ya kura halali 59 zilizopigwa na wajumbe wa baraza hilo.

Akizungumza baada ya kutangaza matokeo hayo, Ole Sosopi amesema chama hakitamvumilia mwanachama yeyote atakayebainika kukisaliti chama.

“Ninyi vongozi wapya mliochaguliwa nendeni mkafanyekazi ya kuendelea kukijenga na kukiimarisha chama Ili chaguzi zijazo chama kiweze kupata ushindi katika nafasi zote za uongozi,” amesema.

Naye mwenyekiti wa Bawacha mkoa wa Morogoro Devota Minja,  amewataka wanawake waliochaguliwa katika nafasi za uongozi katika uchaguzi huo kwenye kuonesha mfano wa uongozi bora kwa kuwa wanawake ni jeshi kubwa.

Amesema katika kuwapata viongozi bora, Chadema haibagui rangi wala jinsi hivyo anaamini wanawake waliochaguliwa watakwenda kuwa viongozi bora na watakitumikia vyema chama hicho.

Related Posts