Dk Biteko ataja maumivu ya walimu

Dodoma. Naibu Waziri Mkuu,  Dk Doto Biteko ameeleza uzoefu wake katika kazi ya ufundishaji, akisema walimu wamekuwa wakiumia wanafunzi wao wanapofeli darasani na maishani.

Dk Biteko ambaye amewahi kuwa mwalimu wa msingi, sekondari,  mkufunzi wa walimu na ofisa elimu,  amesema hayo leo Jumamosi, Juni 1, 2024 jijini Dodoma wakati wa hafla ya chakula cha pamoja baina ya Mbunge wa Dodoma na walimu wakuu wote wa Wilaya ya Dodoma Mjini.

Katika hafla hiyo iliyolenga kujadili muhula wa elimu ulivyokuwa na mipango ya muhula ujao,  Dk Biteko amewataka wazazi kutowaadhibu walimu na kuwalaumu kutokana na kufeli kwa wanafunzi,  bali watafiti tatizo ni nini na kulitatua kwani hawafurahii kufeli kwa wanafunzi

“Raha yetu ni kuona mtoto anasogea mbele na tukiona mtoto anarudi nyuma sisi walimu huwa inatuuma, na ikitokea mwanafunzi amefeli mahali fulani mjue na sisi tunaumia. Msitupe adhabu kwamba kwa kuwa wamefeli watoto wako na nyie walimu wakuu hamfai” amesema Dk Biteko.

Amesema walimu wanachohitaji ni thamani yao na hakuna kinachowafurahisha kama kuona mafanikio ya mwanafunzi ambaye wamemfundisha akifaulu maishani.

Akitolea mfano wake mwenyewe Dk Biteko amesema walimu waliomfundisha, wanajivunia mafanikio yake zaidi hata ya wazazi wake na wanafarijika kusema hadharani kuwa walimfundisha

“Kuna walimu wangu walinifundisha shule ya msingi, wamestaafu wengi ni wazee sasa, ukimkuta kwenye kahawa anasema unajua Biteko ni mwanafunzi wangu na anajivunia kuliko hata baba yangu” ameeleza Dk Biteko.

Dk Biteko amesema kuna baadhi ya familia zinazowadekeza watoto wao, jambo ambalo watoto hawalipati shuleni, hivyo jukumu la kutengeneza jamii imara kubakia kwa walimu pekee

“Kuna familia nyingine watoto wamedekezwa haujawahi kuona, mtoto akichomwa mwiba inapigwa tarumbeta moja wote wanakutana kwenye tukio, dada anaulizwa ulikuwa wapi mpaka mtoto anachomwa mwiba, shuleni hauwezi kukuta hiyo, mwalimu atamwambia pole basi utoe na kama akishindwa baadaye ndio atamsaidia”

Dk Biteko amesema Mwalimu amekuwa na majukumu ya msingi ya kulea mtoto anapokuwa shuleni.

Kwa mfano, mwalimu ni kamaa daktari wa kumpatia huduma ya kwanza, kama msuluhishi  wanapogombana shuleni, kumpa ushauri nasaha anapopatwa na changamoto na kama mwalimu  kwa kumfundisha  hadi aelimike.

“Mwalimu ndiye anayetengeneza mwelekeo wa jamii duniani, baada ya mzazi kumzaa mtoto mwalimu ndiye anayemfundisha huyo mtoto njia za maisha” amesema Biteko.

“Kama tunataka kujenga taifa lenye ustaarabu, kustahimiliana na lenye amani,  mahali pekee pa kuwekeza ni kwenye elimu, mataifa yote yaliyoendelea uwekezaji wake mkubwa upo kwenye elimu” ameongeza.

Naye Mbunge wa Dodoma Mjini ambaye ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema katika kunusuru hali ya elimu katika Wilaya ya Dodoma, wamekuja na mpango wa kukutana na walimu wakuu wote kujadiliana changamoto

“Sisi tunawapenda walimu wetu, leo tumesema tukutane hapa tujadiliane msimu uliopita umeendaje na msimu ujao tufanye nini ili tuweze kulitendea haki jiji letu la Dodoma kwenye sekta ya elimu” amesema Mavunde

Akielezea msukumo wa kukutana na walimu hao,  Mavunde amesema kuwa siku za nyuma watu wanaotafuta wafanyakazi wa ndani walifanya Dodoma kama ndio sehemu ya kuwavuna.

“Wakati naingia kwenye ubunge hapa nilikuwa najisikia vibaya kuona tuna vyuo vikuu lakini hakukuwa na watoto wengi wanaotoka jimboni Dodoma wanaoenda kusoma, ilikuwa ukiwakuta watoto wetu Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wameenda si kama kuwauzia chipsi wanawafulia nguo” ameeleza Mavunde

“Zamani ilikuwa mtu yoyote anayetafuta wafanyakazi wa ndani, simu ya kwanza inapigwa Dodoma kana kwamba hapa ndio kituo cha kuzalisha wafanyakazi wa ndani. Nikaamua kuweka mikakati ya kuhakikisha watoto wetu wananufaika na fursa ya elimu,” ameongeza.

Mageuzi kwenye Sekta ya Elimu

Naye Waziri wa Elimu, Profesa Adolph Mkenda amesema Serikali inajenga vyuo 64 vya veta nchi nzima, kampasi za vyuo vikuu kwenye mikoa yote nchini ili kuboresha upatikanaji wa elimu kwenye maeneo jirani.

Mkenda pia ameeleza kuwa Serikali imeendelea na mapitio ya sera ambapo kila mtoto kwa sasa lazima akae shuleni miaka 10 .

“Sasa hivi mtoto anaanza shule akiwa na miaka sita na anamaliza elimu ya msingi akiwa na miaka 13, halafu useme huyu mtoto aajiriwe, ataajiriwa wapi?, ni lazima mtoto asome mpaka miaka 17 mpaka 18 kwenye shule nyingine.

Profesa Mkenda amepongeza hatua ya Mavunde kukutana na walimu akieleza kuwa italeta tija kwa wakazi wa jiji la Dodoma kuwa na watoto wenye elimu.

Shule mbalimbali nchini zimefunga baada ya muhula wa kwanza wa masomo kukamilika huku wanafunzi na walimu wakiendelea na mapumziko ya shule ya mwezi Juni kabla ya kuanza kwa muhula mpya wa masomo  Julai.

Related Posts