Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango leo Jumamosi ameongoza viongozi pamoja na wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Dar es Salaam katika zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika soko la Ilala linalotumika kwa biashara mbalimbali ikiwa ni kuelekea katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Akizungumza baada ya kufanya usafi, Makamu wa Rais amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kufanya usafi wakati wote.
Amesema katika hatua za utafutaji maisha ni vema kukumbuka suala la usalama katika maeneo ya shughuli za kiuchumi ikiwemo kufanya usafi na kukusanya taka katika sehemu sahihi.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa watanzania wote kufanya jitihada katika kupiga vita utupaji taka ovyo.
Aidha, amewataka viongozi katika ngazi zote kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi na kuwajengea tabia ya kupenda kufanya usafi.
Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila kuhakikisha fedha zinazotarajiwa kutoka Benki ya Dunia zinatumika katika ujenzi wa madampo ya kisasa yatakayosaidia katika urejerezaji taka kama ilivyopangwa.
Pia ametoa rai ya kuanzishwa kwa mashindano ya usafi katika Wilaya za Dar es salaam ili kuwa motisha ya ufanyaji usafi mkoani humo.
Pia ameagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kuhakikisha inadhibiti maji machafu yanayotiririka katika Soko la Ilala ndani ya wiki moja.
Usafi huo pia umeshirikisha viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Zungu, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wa Taasisi mbalimbali pamoja na Chama Cha Mapinduzi.