Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, ametoa maelekezo kuhakikisha kwamba tatizo la majitaka yanayotiririka na kutoa harufu kali katika soko la Ilala jijini Dar es Salaam linamalizwa ndani ya siku ya saba.
Agizo hilo la Dk Mpango limekuja aliposhiriki usafi wa kila Jumamosi katika soko hilo ambapo amewataka viongozi husika kufanya kazi kwa bidii ili limalizike haraka.
Dk Mpango na viongozi wakuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, walijumuika kufanya usafi ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani inayoadhimishwa kila Juni 5.
Katika maelezo yake, Dk Mpango amesema alipanga kwenda sehemu fulani (hakuitaja) kufanya usafi, lakini ghafla usiku alibadilisha uamuzi huo na kwenda soko la Ilala kwa lengo la kushiriki usafi wa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
“Suala la usafi ni jambo muhimu sana, miji yetu isipokuwa safi na mvua ikinyesha tunaathirika na magonjwa ikiwemo kipindupindu, lakini kuna adha kama hii harufu iliyonipokea nani anapenda hiyo?
“Labda niseme tu jana walitaka kunipeleka sehemu sehemu … nikawaambia hapana nataka kwenda kwa ndugu zangu wananchi wa kawaida nilipoambiwa Ilala nikasema sawa hapo nakwenda nyumbani nakushukuru mkuu wa mkoa (Albert Chalamila) na mabadiliko yalifanyika usiku,” amesema Dk Mpango.
Hata hivyo, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Maji taka Dar es Salaam (Dawasa), Kiula Kungi amemweleza Dk Mpango mikakati ya taasisi hiyo ya kuondokana na tatizo hilo kwa muda mrefu na mfupi.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, Kingu amesema wapo mbioni kuanza ujenzi wa mabwawa ya taka ya kisasa maeneo ya Buruguni mchakato utakaochukua miezi 18.
Amesema mradi huo ukikamilika utapunguza changamoto hiyo, maeneo ya Ilala na Kariakoo na wapo mbioni kumpata mkandarasi atakayetekeleza jukumu hilo.
“Lakini hiyo haizuii Dawasa kutekeleza jukumu la kuondoa majitaka, kwa sababu tumenunua magari makubwa ya kunyonya na kuondoa majitaka yanayosambaa katika maeneo haya.
“Tumeshaelekeza magari matatu na mashine kwa ajili ya kusukuma maji taka kwenda katika maeneo husika, lakini mpango mkubwa ni ujenzi wa mabwawa hayo yatakayochakata pia mbolea,” amesema Kingu.
Hata hivyo, Dk Mpango amemtaka Kingu na timu yake kuchukua hatua za dharura kunusuru hali hiyo, akisema miezi 18 mbali na harufu hiyo inahatarisha maisha ya wananchi, ndipo alipomuuliza ampe muda gani kuondoa adha hiyo.
Baada ya majadiliano ya muda mfupi, Dk Mpango akatangaza kuwa Kingu ameomba apewe muda wa wiki moja kushughulikia hali hiyo, akisema ndani muda hataki kuona maji hayo yakitiririka.
Mbali na hilo, amemuagiza Chalamila kuipitia upya menejimenti ya fedha ya soko la Ilala jijini Dar es Salaam ili kujiridhisha kama fedha hizo zinakusanywa kwa ufanisi na kutumika kama ilivyokusudiwa.
“Nimeshangaa hata fedha inayokusanywa hapa haujui ajabu kweli, ninahofia zinaishia mahali hakikisheni fedha inayotakiwa kukusanywa kutoka kwa wananchi hawa inarudi kuwahudumia,” amesema Dk Mpango.