Dk Mpango ataka punguzo bei ya gesi

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameziomba kampuni za gesi nchini kupunguza bei ili Watanzania wengi waweze kutumia nishati safi.

Dk Mpango amebainisha hayo jana Mei 31, 2024 alipohudhuria kongamano lililoandaliwa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) jijini Dar es Salaam.

“Kama wadau wetu, tutazidi kuwaomba muendelee kupunguza bei ya gesi ili kuwawezesha Watanzania kununua na kutumia nishati safi,” amesema Dk Mpango.

Meneja  Mauzo wa Kampuni ya Taifa Gas, Joseph Nzumbi wakati akijibu swali la Makamu wa Rai kuhusu upatikanaji wa gesi kwa bei nafuu,  amesema kwamba Taifa Gas ndiyo kampuni pekee ya gesi nchini inayotoa nishati hiyo kwa bei nafuu.

Alimweleza Dk Mpango kuwa Taifa Gas inapoteza takribani Sh36, 000 kwa kila mtungi wa kilo 15 wa gesi unaouzwa nchini sambamba na mitungi mingine kama vile wa kilo tatu, kilo sita na kilo 38 .

“Hii ni kwa sababu tumeamua kama kampuni  kushirikiana na Serikali ili tuweze kutimiza malengo yetu ya Tanzania ya nishati safi ifikapo 2034,” amesema Nzumbi.

Pia, meneja huyo amesema punguzo hilo la bei ya gesi, lina lengo la kuwafikia Watanzania wengi, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaongoza katika kampeni ya matumizi ya nishati safi.

Itakumbukwa Rais Samia Suluhu Hassan Mei 14, 2024 katika mkutano wa nishati safi ya kupikia uliofanyika katia ukumbi wa Unesco jijini Paris nchini Ufaransa,  alitaja changamoto tatu zinazokwamisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, ikiwamo gharama kubwa za vyanzo vya nishati.

Changamoto nyingine ni mataifa tajiri kutotoa kipaumbele kwa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na kutoshirikishwa kwa wadau wakiwamo wa teknolojia za kuzalisha nishati hiyo.

Rais Samia ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA) katika mkutano huo wa nishati safi ya kupikia,  alizitaka nchi wahisani kuchangia mpango wa kupatikana kwa nishati safi ya kupikia Afrika.

Related Posts