Fainali FA Zazibar, Mzize, Sopu kazi ipo

ILE vita iliyokuwapo katika Ligi Kuu Bara iliyomalizika mapema wiki hii katika mbio za Mfungaji Bora inajirudia tena Zanzibar katika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).

Katika Ligi Kuu Bara kulikuwa na vita ya nyota wa Yanga na Azam, Stephane Aziz KI (Yanga) na Feisal Salum ‘Fei Toto’ (Azam FC) kila mmoja akitokwa jasho na mwishoni staa wa Yanga alimaliza kibabe akimzidi mwenzake kwa kutupia nyavuni mabao 21 dhidi ya 18 aliyomaliza nayo Fei Toto.

Lakini, katika mwendelezo wa hilo kesho inapigwa fainali ya Kombe la Shirikisho na kuna vita nyingine nzito ya kuwania ubingwa wa michuano hiyo sambamba na nyota wa timu hizo watakuwa katika mchuano mkali wa kuwania tuzo ya Mfungaji Bora kwa msimu huu.

Mechi hiyo ya fainali inapigwa usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex  uliopo Unguja, huku Clement Mzize wa Yanga na Abdul Suleiman ‘Sopu’ watakuwa na ‘ligi’ yao ya kumaliza msimu kwa heshima kupitia michuano hiyo.

Hii itakuwa mara ya nne kwa timu hizo kukutana msimu huu, awamu ya kwanza ilikuwa Agosti 9 katika mchezo wa Ngao ya Jamii kwa ajili ya ufunguzi wa msimu huu iliyopigwa jijini Tanga na  Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, zikakutana tena Oktoba 23 katika Ligi Kuu Bara na Wananchi wakafurahi kwa ushindi wa mabao 3-2.

Mechi ya tatu ikifuata Machi 17 ambapo safari hii, Azam ikalipa mapigo kwa kushinda mabao 2-1.

Na safari hii timu hizo zinakutana tena zikiwania taji hilo katika pambano la nne kwa msimu huu, lakini likiwa ni la tatu katika fainali ya FA tangu michuano iliporejeshwa upya katika msimu wa 2015-2016 baada ya awali kusimama kwa muda mrefu tangu 2002 wakati michuano hiyo ikifahamika kama Kombe la FA.

Awali zilikutana mwaka 2015-2016 na Yanga kushinda kwa mabao 3-1 kabla ya msimu uliopita kukutana tena kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga na Wananchi wakashinda bao 1-0 kupitia Kennedy Musonda.

Kitendawili cha bingwa wa msimu huu, kitatenguliwa kesho Jumapili kwa timu hizo, huku Mzize na Sopu watakutana kwenye vita yao kama ilivyokuwa kwa Fei na Aziz Ki na atakayezitumia vyema dakika za mechi hiyo basi atamaliza kwa heshima kwa kutwaa tuzo hiyo

Mzize, yupo katika nafasi nzuri zaidi kwani hadi sasa anaongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao matano kama aliyonayo Edward Songo wa JKT Tanzania ambaye timu yake ilishaaga michuano.

Mzize atakuwa na mtiani wa kuisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa pili msimu huu huku akitimiza kile ambacho alikuwa akikihitaji cha kuwa mfungaji bora, akichuana na Sopu aliyetwaa tuzo hiyo misimu miwili iliyopita wakati akiwa na Coastal Union iliyofungwa na Yanga kwa penalti baada ya dakika 120 kuisha kwa sate ya 3-3.

Sopu ni mmoja ya wachezaji wawili wanaowafuata Mzize na Songo akiwa na mabao manne sawa na aliyonayo Yohana Mkomola wa Tabora United ambayo iliaga michuano hiyo mapema.

Iwapo Sopu atarudia alichofanya katika sare ya Yanga na Coastal kwa kufunga hat trick japo Wagosi walikosa ubingwa kwa penalti, itakuwa na maana ndiye atakayebeba kiatu, hasa kama Mzize atapita mswaki kama ilivyokuwa katika mechi mbili zilizopita za robo na nusu fainali dhidi ya Tabora na Ihefu.

Sopu pia ana kazi ya kuibebesha Azam taji la pili la michuano hiyo baada ya awali kutwaa 2028-2019, lakini akiwa na vita hiyo dhidi ya Mzize ambaye kama atafunga bao moja tu na staa wa huyo wa Azam akatoka patupu basi atamaliza gundu kwa kutwaa tuzo hiyo aliyoikosa msimu ujao alipozidiwa bao moja na Andrew Simchimba wa Ihefu.

Kama makocha wa vikosi vyote viwili, Gamondi na Dabo  wataamua kuanzisha busta zao zote, tunaweza kushuhudia vinara hao wa ufungaji kwa kila upande wakianzia benchi.

Kwanini? Hivi karibuni Gamondi amekuwa akipendelea kuanza katika safu yake ya ushambuliaji na Joseph Guede ambaye kama ni gari linaonekana kuwaka ndiye mshambuliaji hatari zaidi kwa sasa kwenye kikosi cha Yanga.

Kwa kuzingatia mgawanyo wa mechi kwa kila mchezaji aliokuwa akiufanya Gamondi kulingana na wingi wa michezo iliyokuwa mbele yao basi huenda Mzize akaongoza safu ya ushambuliaji ya Wananchi maana ndiye aliyekuwa na jukumu hilo katika michuano hiyo.

Pia kocha huyo anaweza kuamua kuanza na washambuliaji wawili kiasili huku akipunguza idadi ya viungo ili kuwa na nguvu kubwa katika safu yake ya ushambuliaji jambo ambalo limeonakana msimu huu katika michezo kadhaa ikiwemo katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini.

Kwa upande wa Azam, hivi karibuni wakati ambao Dabo amekuwa akihitaji kuwa salama amekuwa akipenda kuanza na washambuliaji watatu Kipre Junior, Gibril Sillah na Fei Toto huku nyuma akijaza viungo wenye uwezo wa kuzuia.

Kama atamka hivyo basi huenda nafasi ya Sopu kuanza katika fainali ikawa finyu, lakini akihitaji kuwa na wigo mpana wa kujenga mashambulizi yake kama ilivyokuwa dhidi ya Geita Gold katika mechi ya mwisho katika ligi basi anaweza kuanza na wachezaji wote hao kwa wakati mmoja.

Kuhusu nani anaweza kuanza katika kikosi chake cha kwanza Dabo anasema itategemea na mpango ambao wataingia nao katika mchezo huo; Itapendeza kumaliza msimu tukiwa na ubingwa, tunajua sio kazi nyepesi lakini tufanya kile ambacho tunaweza kuufanya mchezo kuwa mgumu kwa wapinzani wetu.”

Kocha wa zamani wa Azam FC na Yanga, Hans van der Pluijm amewatakia kila kheri Mzize na Sopu katika mchezo huo wa fainali huku akiwazungumzia kama nyota wajao wa Taifa Stars. “Napenda uchezaji wao, wanakasi na hata maarifa na jambo zuri kwao wamekuwa wakipata nafasi ya kuonyesha katika timu kubwa, wanakila sababu ya kuendelea kukua na baadae kuwa wachezaji wa kutegemewa katika vikosi hivyo na hata upande wa timu ya taifa la Tanzania,” alisema kocha huyo.

Yanga 5-1 Hausung (Jonas Mkude 20′, Clement Mzize 27′, 33′, 57′, Skudu Makudubela 25′)

Yanga 5-0 Polisi TZ (Joseph Guede 13′, 45′, Farid Mussa 33′, Clement Mzize 82′, Ibrahim Shekhan 87’p)

 Dodoma Jiji 0-2 Yanga (Emmanuel Martins 8’OG, Clement Mzize 66′)

Azam 5-0 Green Warriors (Kipre Jr 23, Idd Nado 32′, Paul Kyoba 56’OG Abdul Sopu 65′ Lyanga 83′)

Azam FC 3-0 Mtibwa Sugar (Abdul Suleiman ‘Sopu’, Ayoub Lyanga, Feisal Salum)

Related Posts