Dodoma. Mbunge wa Kawe, Mchungaji Joseph Gwajima amekataa kuuliza swali la nyongeza bungeni akisema swali lake la msingi halikujibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.
Katika swali la msingi Gwajima amehoji kuna mpango gani wa dharura wa kudhibiti mito inayopanuka na kuhatarisha maisha na mali za wananchi katika Jimbo la Kawe.
Akijibu swali hilo, leo Mei 31, 2024, Naibu Waziri wa katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imechukua hatua za dharura za kukabiliana na hali hiyo.
Amezitaja hatua hizo kuwa ni kuandaa Mwongozo wa Usafishaji Mchanga, Tope na Taka Ngumu kwenye Mito na Mabonde katika Mkoa wa Dar es Salaam wa mwaka 2021.
Amesema mwongozo huo una lengo la kuelekeza aina ya mfumo wa usafishaji wa mito kwa kuchimba mchanga, tope na taka ngumu zinazohitaji kuondolewa ili kudhibiti mtiririko wa maji katika.
“Mwongozo huu unatoa maelekezo ya hatua mbalimbali zitakazochukuliwa na wadau wa kuhifadhi mazingira katika kuhakikisha mazingira ya mito yanalindwa na kuhifadhiwa na kutumika katika njia sahihi ikiwa ni pamoja na kudhibiti uchimbaji wa michanga na ujenzi wa makazi ndani ya mita 60 kutoka kwenye kingo za mito,” amesema.
Ametoa wito kwa Serikali za mitaa kote nchini Kusimamia kikamilifu Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 ili kuzuia shughuli za kibinadamu.
Amezitaja shughuli hizo kuwa ni kama vile uchimbaji wa mchanga na kuelimisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Baada ya majibu hayo, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson alimpa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza Gwajima.
Hata hivyo, baada ya kusimama Gwajima amesema anafikiri kuwa hana haja ya kuuliza swali la nyongeza kwa sababu swali lake la msingi halijajibiwa
“Mimi nimeuliza kuna mpango gani wa dharura wa kudhibiti mito inayopanuka na kuhatarisha maisha na mali za wananchi katika Jimbo la Kawe, lakini yeye anajibu Dar es Salaam. Kwa hiyo sitakuwa na swali na kama ikikupendeza mheshimiwa Spika lijibiwe tena baadaye,” amesema.
Kauli hiyo ilimfanya Dk Tulia kumwahidi kuwa atalitazama swali hilo na majibu yake na baadaye atatoa uamuzi.