MisaTan: Vyombo vya habari vitoe elimu ya uchaguzi

Dar es Salaam. Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, asasi mbalimbali za kiraia pamoja na vyombo vya habari nchini vimetakiwa kushirikiana kuhakikisha elimu ya uraia na ushiriki katika masuala ya uchaguzi inafika kwa wananchi bila kuweka kando kundi lolote.

Wito huo umetolewa  Mei 31 na Mkurugenzi wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan), Elizabeth Riziki wakati wa Kongamano la Siku mbili la Kufanya Tathmini ya Hali ya Kujieleza, Haki ya Kupata taarifa na Uhuru wa Wana Habari Jijini Dar es salaam.

Riziki amesema ili wananchi washiriki ipasavyo kwenye  uchaguzi wanatakiwa kupata taarifa sahihi na elimu kwa njia mbalimbali ikiwamo kupitia vyombo vya habari.

Amesema kutokana na wajibu huo wanahabari wanatakiwa kufuata maadili na misingi ya taaluma zao kwa kuhakikisha habari zinazoandikwa na kutangazwa,  ni sahihi kwani itamsaidia mwananchi kufanya uamuzi sahihi.

Ameongeza kuwa wao kama Misa-Tan jukumu lao ni kuhakikisha wanafanya uchechemuzi katika masuala yanayohusu uhuru wa vyombo vya habari, kujieleza, kutoa pamoja na kupokea taarifa.

“Pia bado tuko katika uchechemuzi wa kuhakikisha hata zile sheria ambazo siyo rafiki katika utoaji na upatikanaji wa habari pamoja na uhuru wa kujieleza zinaboreshwa”

Kauli ya Riziki imeungwa mkono na Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle ambaye amesema kuwa uhuru wa vyombo vya habari unachochea raia wenye taarifa na hivyo  kufanya uamuzi sahihi.

Naye, Ofisa Mtendaji Mkuu wa  Baraza la taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO), Racheal Chagonja,  amesema kuwa katika kuelekea uchaguzi,  mijadala inatakiwa kuendelea katika kuangalia namna gani ya kutengeneza mazingira wezeshi katika kuboresha uhuru wa kujieleza.

Kwa upande wake,  Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema shughuli za kichechemuzi hasa katika kipindi hiki cha kukaribia uchaguzi, zitasaidia kuongeza hamasa kwa wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kushiriki kikamilifu katika chaguzi hizi kwa kuzingatia maslahi ya nchi.

Hata hivyo amesisitiza kuwa uhuru huo wa  kujieleza ni  lazima uzingatie maadili, miongozo na desturi za Mtanzania kwa kulinda utu na utaifa.

“Sekta hii inakua kwa kasi kubwa hivyo umakini na uhakiki wa taarifa ni muhimu, ili kulinda maadili ya sekta na jamii ya Watanzania kwa ujumla”amesema.

Pia amesema uhuru wa kujeleza nchini umeendelea kupiga hatua ambapo kwa mujibu wa “World Freedom Report” ya mwaka 2023/2024 iliyotolewa na taasisi ya Waandishi wa Habari Wasiokuwa na Mipaka (RSF) inaonyesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 97 kutoka nafasi ya 143 mwaka 2022/2023 kidunia na nafasi ya kwanza katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa mafanikio ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari.

“Kwa mujibu wa taarifa nyingine iliyotolewa Aprili 2024 na taasisi ya Afrobarometer inayopima namna watu wanavyojisikia kuwa huru kuhisiana na taarifa, Tanzania inashika nafasi ya kwanza miongoni mwa nchi 39 za bara la Afrika,”amesema.

Related Posts