Mitambo ya umeme Kidatu na Mtera kufanyiwa ukarabati

Ifakara. Katika kuhakikisha kuwa Umeme unapatikana kwa uhakika Naibu Waziri Mkuu Dk Doto Biteko amesema Serikali imeanza ukarabati wa mitambo ya kufua umeme katika kituo cha Kidatu na Mtera mkoani Dodoma.

Dk Biteko amesema hayo leo Jana Mei 31, 2024 wakati wa uzinduzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme kwenye gridi ya Taifa  kilichopo halmashauri ya mji Ifakara ambapo alisisitiza kuwa tayari mitambo hiyo imeshaanza kukarabatiwa ili umeme upatikane kwa uhakika hapa nchini.

“Kituo cha kidatu kinahitaji matengenezo makubwa na tumeanza na mashine namba mbili kati ya nne ambazo zilikua zimepitiliza muda wa matengenezo kwa muda wa miaka minne  tumeamua kufanya ukarabati, na kwenye kituo chetu cha Mtera  mashine zetu nne pia zimepitiliza miaka mitano bila ukarabati ila napo tumeshaanza” amesema.

Ameongeza kuwa “Kwa sasa Watanzania hawataki maneno bali wanachotaka wao ni umeme maana kwa kasi ya maendeleo ninayoiona kwa watu wa Kilombero, Mlimba na Malinyi na maeneo mengine  bila shaka mahitaji ya umeme yatakuwa makubwa ndani ya muda mfupi na tusibweteke tukadhani tumefika mwisho hii ni likizo tu, tunapaswa kujipanga miaka 20 ijayo” amesema Dk Biteko

Hata hivyo,  Biteko amelitaka Shirika la Umeme,  kuendelea kuhakikisha umeme unapatikana kwa kiasi kinachotakiwa kwa kuwa mahitaji ya nishati hiyo ni makubwa na watu wanaitumia kujipatia maendeleo yao kiuchimi.

Awali Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Usambazaji Umeme vijijini (REA) Johnes  Olotu amesema Wilaya Kilombero pekee yenye vijiji 110,  vyote vimeshapata umeme na vitongoji 488 bado utaratibu wa kuviwekea umeme unaendelea ambapo mpaka sasa kati ya hivyo 188 vimeshawekewa umeme na vingine utaratibu unaendelea wa huduma hiyo muhimu kuwafikia wananchi.

Simon John mkazi wa Ifakara am esema kitendo cha Serikali kuifanyia ukarabati mitambo hiyo ya kufua umeme,  kitaondoa adha ya kukatika umeme mara kwa mara maana mitambo mingine inashindwa kufanya kazi sababu ya uchakavu.

Related Posts