Seoul. Rais Samia Suluhu Hassan ametembelea Kituo cha Kimataifa cha Kubadilishana Ujuzi na Maendeleo (GKEDC) cha Korea ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake nchini hapa.
Pia, amefanya mazungumzo na watayarishaji maarufu wa filamu wa Korea na waandaaji wa filamu wa Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika sekta hiyo.
Alipotembelea GKEDC leo Juni Mosi, 2024, Rais Samia alitembezwa katika jengo la makumbusho la Korea linalohifadhi historia ya maendeleo ya Taifa hilo hasa katika sayansi na teknolojia.
GKEDC ilianzishwa mahsusi kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa maendeleo ya Korea na mataifa mengine na kukuza ushirikiano wa kiuchumi wa kimataifa.
Ndani ya jengo hilo, Rais Samia ameonyeshwa historia ya safari ya maendeleo ya kiuchumi ya Korea iliyoanza mwaka 1945 hadi sasa ikilenga kujenga dhana ya kujivunia kwa Wakorea.
Kituo hicho kinafanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na maonyesho, elimu, utafiti na ushirikiano wa ujuzi kwa mataifa.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amefanya mazungumzo na watayarishaji wa filamu nchini pamoja na waandaaji wa filamu wa Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kukuza tasnia hiyo nchini Tanzania.