Sababu uchaguzi TLS kukosa ‘hamasa’

Dar es Salaam. Wakati Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) ikiongeza muda wa siku saba kutoa nafasi kwa wanachama zaidi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho, baadhi ya mawakili wameeleza sababu ya uchaguzi huo kudorora ikiwamo mabadiliko ya sheria ya chama hicho.

 Sababu nyingine imetajwa kuwa ni kuchoshwa kwa baadhi ya mawakili, wakilaumu viongozi wao kushindwa kutetea masilahi yao. 

Akizungumza na Mwananchi Mei 31, 2024, Katibu wa Kamati Uchaguzi TLS, Nelson Frank, amesema awali mwisho wa wanachama kuchukua fomu kuomba kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho ulikuwa Mei 28, 2024.

“Lakini Kamati ya Uchaguzi imeongeza muda wa siku saba kuanzia Mei 31 mpaka Juni 6, 2024 saa 11.00 jioni ili kutoa fursa kwa wanachama zaidi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwani bado kuna nafasi hazijapata wagombea na nyingine waliojitokeza ni wachache,” amesema na kuongeza;

“Wito wangu kwa wanachama ambao wana sifa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za mwaka 2022 na Sheria ya TLS kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, wanahamasishwa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama.’’

Frank amezitaja nafasi zinazogombewa kuwa ni rais, makamu wa rais, mweka hazina, wawakilishi katika Baraza la Elimu ya Sheria, wadhamini wa Mfuko wa Wafu wa Mawakili (DATF) na wadhamini wa mfuko wa Mawakili Tanzania Bara.

Frank amesema uchaguzi wa viongozi na wawakilishi wa nafasi hizo utafanywa na mkutano mkuu wa mwaka wa TLS Agosti 2, 2024 jijini Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.

Nafasi nyingine zinazogombewa amezitaja kuwa ni mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Vijana (AYL) na viongozi wa kanda za chama hicho.

Katika nafasi ya urais ambayo mpaka Mei 28 walikuwa wamejitokeza wagombea wawili, Frank amesema idadi ya wagombea imeongezeka mpaka kufikia wanne.Kwa sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Harold Sungusia.

Nafasi ya makamu wa rais wa TLS amesema ni wagombea wawili waliojitokeza.

Frank amesema orodha kamili ya majina ya wagombea katika kila nafasi itatolewa baada ya kufanyiwa marekebisho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TLS, Jaji Joaquine De-Mello.

Katika nafasi ya mwenyekiti wa AYL inayoshikiliwa na Edward Heche anayemaliza muda wake baada ya kuitumikia kwa vipindi viwili mfululizo, waliojitokeza kumrithi ni wanne.

Kwa mujibu wa Frank, kanda za TLS ambazo zitahusika katika uchaguzi huo ni ya Mzizima (Dar es Salaam), ambayo kwa nafasi ya kiongozi wa kanda waliojitokeza ni wawili.

Pia katika kanda hiyo kuna nafasi ya mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya AYL ambayo aliyekuwa mwakilishi amejiuzulu ili kugombea nafasi nyingine, amejitokeza mgombea mmoja.

Katika Kanda ya Bagamoyo amejitokeza mgombea mmoja wa nafasi ya kiongozi wa kanda, wakati Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kusini hazijapata mgombea.

Nyingine ni Kanda ya Magharibi ambayo kuna mgombea mmoja wa nafasi ya kiongozi wa kanda, Kanda ya Kati, mgombea mmoja na Kanda ya Kaskazini yenye mgombea mmoja.

Katika nafasi za wawakilishi katika Baraza la Elimu ya Sheria (nafasi 2) wamejitokeza wagombea wawili, na kwa upande wa wadhamini wa DATF kati ya nafasi mbili mpaka tano, mpaka sasa wamejitokeza wagombea watatu.

Kwa mujibu wa Frank, katika nafasi ya wadhamini wa Mfuko wa Wakili mpaka sasa hakuna wagombea waliojitokeza.

Kiongozi wa Mawakili Kanda ya Ziwa na pia mjumbe wa GC, Steven Cleophace amesema kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria ya TLS ya mwaka 2023, uchaguzi wa viongozi wa chama hicho utakuwa unafanyika kila baada ya miaka mitatu badala ya kila mwaka kama ilivyokuwa awali.

Sababu uchaguzi kukosa hamasa

Mabadiliko ya Sheria ya TLS yaliyopunguza nguvu ya chama hicho na madai ya viongozi kushindwa kutetea uhuru wa chama hicho, yanatajwa kuwa sababu ya kudorora uchaguzi huo.

Hata hivyo, Rais wa TLS, Harold Sungusia alipoulizwa kuhusu hali hiyo, amesema hawezi kuzungumzia badala yake akamtaka mwandishi amuulize mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa TLS, Jaji Joaquine De-Mello.

“Kamati yetu ya uchaguzi iko huru sana, mimi siruhusiwi kuzungumzia,” amesema.

Hata hivyo, Jaji De-Mello alipoulizwa kwa simu, amesema kwa wakati huo alikuwa kwenye mkutano, hivyo asingeweza kuzungumza.

Mmoja wa mawakili ambaye hakutakutaka kutajwa jina lake gazetini, amesema sababu ya uchaguzi huo kudorora ni mabadiliko ya Sheria ya TLS yaliyoongeza nafasi za uongozi.

“Tuliweka ugatuzi wa madaraka kwa kuongeza nafasi nyingi za uongozi. Kwanza kuna kanda saba na kila kiongozi wake anaingia Baraza la Uongozi na chini yake kuna kamati ya uongozi inayoratibu shughuli za kanda. Ni sheria mpya kwa hiyo inawezekana bado haijazoeleka tu,” amesema.

Hoja hiyo inaungwa mkono na wakili, Dk Onesmo Kyauke akisema baada ya mabadiliko hayo, mawakili wa Serikali wakajiondoa TLS na kwenda kwenye chama chao.

“Sheria pia imezuia viongozi wa vyama vya siasa kugombea uongozi TLS kama ilivyokuwa zamani. Mbali na sheria, hata uongozi wa sasa umekosa ajenda ya mabadiliko,” amesema Dk Kyauke.

Wakili Aloyce Komba amesema wanachama wa TLS wamekatishwa tamaa na uongozi ulioshindwa kupigania uhuru wa chama chao.

“TLS haiko huru na haitakuwa huru kwa sheria hizi ambazo zinafanya chama kisimamiwe na Serikali. Kwa mfano hata kanuni za uchaguzi wetu zinatungwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa nini tusitunge wenyewe?” amehoji.

Amesema hata katika mhimili wa Mahakama mawakili wamebanwa kwa kuundiwa Kamati ya Maadili ya Mawakili.

“Kwa mabadiliko haya ya sheria mawakili wamenyang’anywa kazi zenye masilahi, yaani hawaruhusiwi kutetea hata serikali ya kijiji,” amesema.

“Wakati wenzetu wahandisi wanapewa kazi za halmashauri, sisi haturuhusiwi. Matokeo yake hata kampuni binafsi sasa zinaajiri wanasheria wao, mawakili wa kujitegemea hawapati kazi. Haya yote ni kwa sababu tumesindwa kupigania uhuru wetu,” amesema.

Related Posts