MABOSI wa Simba wajanja sana. Kwa sasa wameamua kufanya mambo yao kimyakimya katika kuimarisha kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao ili kurudisha heshima mjini na hivi unavyosoma Mwanaspoti wanafanya mazungumzo na mawinga wawili wa maana wa DR Congo, akiwamo anayewaniwa na Yanga.
Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba, pale DR Congo Simba imefanya mazungumzo na winga Elie Mpanzu Kibisawala kutokea AS Vita Club ambaye ni fundi wa mguu wa kushoto aliyekuwa na msimu Bora wa Ligi, uliomalizika wiki hii.
Mpanzu raia wa nchi hiyo mwenye umri wa miaka 22, ameonyesha nia ya kutaka kujiunga na Simba msimu ujao jambo linaloweza kurahisisha dili hilo kutiki licha ya vyanzo kutoka kwa winga huyo vikieleza klabu mbalimbali pia zimekuwa zikimuhitaji.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kililiambia Mwanaspoti ni kweli wako kwenye mazungumzo na nyota huyo, ingawa bado hawajafikia makubaliano ya mwisho japo jambo linalowapa matumaini ya kumpata ni kutokana na yeye kuonyesha utayari.
“Ukweli ni kwamba sisi tumefanya mawasiliano naye ya kuangalia namna ya kumpata, kitu ambacho kimetuvutia kutoka kwake ni uwezo wake mzuri wa kucheza kwa ufasaha winga zote mbili kwa maana ile ya kulia na kushoto,” kilisema chanzo hicho.
Simba ilikuwa ikimhitaji winga huyo tangu mwanzoni wa msimu uliopita ila ilishindwa kuinasa saini yake na sasa imerudi upya kuhakikisha inampata ili kuongeza nguvu huku beki wa timu hiyo Mkongomani wenzake, Henock Inonga akitumika kumpata.
Wekundu hao wamebakiza hatua ya kwenda kumalizana naye tu kwani bajeti ya Mpanzu iko ndani ya uwezo wao, japo Simba inatakiwa kufanya mambo kwa haraka kwani AS Vita, ipo katika hesabu kubwa za kumuongezea mkataba winga huyo.
Lakini wakati Mpanzu akisubiri hatua ya mwisho, mabosi wa Simba wametua kwa winga mwingine wa Mabingwa wa Ligi Kuu ya nchini humo, TP Mazembe, Philippe Kinzumbi ambaye Yanga inampigia hesabu za kumvuta kusaidiana na mastaa wengine waliopo Jangwani kwa sasa.
Kinzumbi amekuwa kwenye hesabu za Yanga kwa msimu mmoja na zaidi kwa mahitaji ya winga wa kushoto ambapo sasa kila timu itakuwa na ushawishi wake kwa fundi huyo wa kujua kuwapangua mabeki na hata kufunga.
Akizungumza na Mwanaspoti jana, Kinzumbi amethibitisha kufuatwa na mabosi wa Simba ingawa bado hawajamalizana nao. “Simba wamenipigia tumeongea mengi, lakini wametaka kujua mkataba wangu Mazembe ukoje, nimewapa na kuwaambia wamalizane na klabu kama ilivyokuwa kwa Yanga, kama tukikubaliana naweza kuja kucheza Tanzania, kiu yangu ni kucheza Tanzania kwa klabu kubwa,” alisema Kinzumbi.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alipoulizwa na Mwanaspoti juu ya dili hizo, alisema suala la usajili kwa sasa ni mapema kulizungumzia ingawa wao wanatambua wana jukumu kubwa la kuboresha timu hiyo kwa ajili ya kuleta ushindani msimu ujao kwenye mashindano tofauti.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua wakati mchakato huo ukiendelea kwa mabosi wa Simba kuzungumza na kumalizana na wachezaji kadhaa akiwamo beki Lameck Lawi kutoka Coastal Union, mambo yamekuwa mengi kwa viongozi kwani akili zipo pia kumalizana na kocha mkuu mpya.
Simba inataka kuhakikisha kwanza dili hilo baada ya kocha mkubwa na mzoefu wa soka la Afrika, Mualgeria Abdelhak Benchikha kuondoka Aprili 28, mwaka huu kufuatia kuipa ubingwa wa Kombe la Muungano lililofanyika visiwani Zanzibar.
Baada ya kuondoka kwa Benchikha, timu hiyo ikawa chini ya mzawa, Juma Mgunda ambaye aliiongoza katika jumla ya michezo tisa ya Ligi Kuu Bara na kati yake alishinda saba na kutoka sare miwili na kuiwezesha kumaliza nafasi ya tatu na pointi 69. Pointi hizo ilizovuna msimu huu Simba ni sawa na za Azam FC iliyomaliza nafasi ya pili ila zikitofautiana katika mabao ya kufunga na kufungwa hivyo kucheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao jambo ambalo halikuwapendeza mabosi.
Hata hivyo, kumekuwa na ugumu wa kupata jina la kocha aliye kwenye rada hizo kutokana na jambo hilo kufanywa kwa usiri mkubwa ukihusisha mabosi wachache kuhofia kuvuja mapema.