Usajili matibabu bure kwa makundi maalumu mbioni

Unguja. Wasimamizi wa jumuiya zinazohudumia kaya masikini na watoto yatima,  wametakiwa kusimamia kikamilifu usajili wa kundi hilo katika Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) ili kuwarahisishia kupata matibabu.

 Pia, wadau wa maendeleo na watu wenye uwezo,  wameombwa kujitokeza kuchangia mfuko huo kulisaidia kundi hilo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ZHSF, Yaasin Ameir Juma ametoa kauli hiyo Juni Mosi, 2024 alipofungua semina ya jumuiya hizo Unguja, Zanzibar.

Amesema usajili wa kundi hilo unatarajiwa kuanza rasmi Juni 3, 2024 ili wasibaki nyuma na kufikia azma ya Serikali ya  kutoa matibabu bora kwa wote likiwemo kundi hilo la wasiojiweza kupata huduma za afya kwa haraka na kuondoa usumbufu wanaoupata wanapotafuta matibabu.

“Si vyema kuona watumishi wa sekta rasmi na zisizo rasmi wanapata huduma za afya, huku kundi hili lisilokua na uwezo tukiliacha nyuma na hata baadhi yao wakahisi tumewasahau,” amesema Yaasin.

Amesema ZHSF imeanzisha akaunti ya Hesabu ya Usawa ambayo itasimamia upatikanaji wa rasilimali fedha,  kwa ajili ya kugharamia utoaji wa huduma bora za afya kwa watu wasiokuwa na uwezo na makundi maalumu.

Amesema mtu yeyote anaweza kuchangia katika akaunti hiyo na kuona kundi hilo linaendelea kupata huduma kupitia mfuko huo.

“Yeyote anayehitaji kujitolea kuchangia kama sehemu ya sadaka kwa wenzetu hawa anakaribishwa, ili waweze kuendelea kupata huduma kupitia mfuko huu siku hadi siku,” amsema.

Mbali na hayo amesema ili kundi hilo liendelee kupata huduma kupitia ZHSF,  ushirikiano wa pamoja unahitajika kati ya Serikali, wadau na watu wenye uwezo katika kuichangia akaunti ya usawa inayogharamia matibabu ya kundi hilo.

Ofisa Sheria wa mfuko huo, Thurea Ghalib Mussa,  amesema misingi ya kuanzishwa ZHSF ni umoja, kusaidiana, pamoja na  Serikali kusaidia wasio na uwezo katika kupata huduma bora za afya.

Kaimu Mkurugenzi Mipango na uwekezaji ZHSF, Khalifa Muumin Hilal amewaomba wawekezaji kuwekeza katika mfuko huo,  ili kuwasaidia wasio na uwezo, zikiwemo kaya masikini na watoto yatima.

Kwa mujibu wa Sheria Namba 1 ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar ya mwaka 2023, Kifungu cha 40 (1), akaunti ya Hesabu ya Usawa itapokea na kuweka fedha inayotokana na kodi maalumu kutoka serikalini, mashirika ya maendeleo, taasisi zisizo za kiserikali, kampuni au vyanzo vyingine halali.

Related Posts