Wafugaji watajwa tembo kuvamia makazi ya watu

Dodoma. Wakati vilio vya wanyama waharibifu wakiwemo viboko, tembo na nyani kuvamia makazi ya watu vikisikika bungeni, wafugaji wanatajwa kuchangia hali hiyo.

Wabunge pia wamepigia kelele fidia kwa wananchi wanaopata madhara kutokana na wanyama hao, wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2024/25.

Wamechangia mjadala kwa hisia kuonyesha madhara wanayoyapata wananchi, huku wengine wakibainisha chanzo cha wanyama hao kutoka kwenye hifadhi na kwenda kuvamia makazi ya watu.

Akichangia mjadala huo Mei 31, 2024 mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida alisema Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, iliyopandishwa hadi kutoka Pori Tengefu la Selous ilikuwa na wanyama wengi hasa tembo lakini wafugaji wamepeleka ng’ombe wengi hifadhini hivyo kusababisha vurugu.

“Sasa najiuliza kama ng’ombe ameingia Selous tembo atakwenda wapi? Lazima atakwenda kwa watu. Ina maana mmemuharibia njia yake ndani ya Selous,” amesema.

“Sasa wanataka kuvuka Ruvuma kwenda Msumbiji ni uvunjivu wa taratibu na sheria na ndiyo matokeo yake migogoro itaendelea kuwa mikubwa,” amesema.

Amesema katika hifadhi ya Tendeguru, watu wamevamia na mifugo yao kwa hiyo tembo wanapoenda katika eneo hilo wanakuta mifugo.

Amesema wanyamapori hawawezi kukaa hapo, wanalazimika kubadilisha njia, hivyo kwenda kwenye makazi ya binadamu.

“Tulikwenda na waziri, akasema atawatoa wafugaji lakini hadi leo wapo na kwamba wasitegemee migogoro  itaisha. Nchi isipofuata sheria na taratibu haiwezi kumaliza changamoto,” amesema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Jacqueline Msongozi amehoji kama Serikali imewahi kufanya utafiti kufahamu kwa nini tembo wamekuwa wakitoka hifadhini au katika mapori na kwenda katika maeneo ya makazi.

Amesema kwa miaka mitano amekuwa akipiga kelele kuhusu tembo,  lakini wakati huu ataishauri Serikali jinsi ya kutatua changamoto hiyo.

“Sasa hivi yamekuwa siyo mapori ya wanyamapori yamekuwa mapori ya wanyama watu. Kwa sasa wafugaji wamejaa huko wanatembeza ng’ombe zao kila sehemu. Na wanyama siyo tembo tu bali na wengine. Tunawaona (tembo) kwa kuwa wamekuwa na athari katika jamii,” amesema.

“Lakini hivi sasa fisi, tumbili wote tunapishana nao huko kwa sababu wale wafungaji ng’ombe wao wamefungwa kengele zinapopiga tembo wanakimbia na wanyama wengine wanakimbia, waende wapi,” amehoji.

Amesema iko haja ya kufanya utafiti na kuwaondoa watu ambao wamekuwa wakifuga wanyama katika mapori kinyume cha taratibu na sheria.

Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali za kutengeneza mabomu, kuongeza idadi ya askari, amesema hazitoshelezi.

“Nataka nimuulize waziri anayehusika (Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki) anataka kuona ng’ombe hawa wanaingia Ikulu?” amehoji.

Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu amesema yeye anawatetea tembo na wanyama wengine waliopo nchini.

“Unajua wabunge, tukilia sana Mungu anaweza kusema ninyi nyote ni viumbe wangu, kama hawa (tembo) wanawasumbua sana basi ngoja niwachukue wote kama alivyofanya nchi nyingine lakini tutakuwa hatueleweki,” amesema.

Amesema wanyamapori ndiyo wanaowavutia watalii kuja nchini baada ya kuadimika katika nchi nyingine.

Mbunge huyo amesema kinachotakiwa ni watu kutumia akili na utashi waliopewa ambao wamenyimwa wanyama.

Msambatavangu ameitaka Serikali kufanya utafiti wa tembo kuangalia mabadiliko yao kwa kuwa wanyama hao hawafanani na wa zamani kwa kuwa wameongezeka uzito.

Amesema utafiti utakaofanyika ndiyo utaonyesha iwapo tabia za tembo wa sasa zimebadilika na wanavutiwa kuishi karibu na binadamu.

Mbunge wa Nanyumbu, Yahya Mhata amesema jimbo lake anazungukwa na Mto Ruvuma ambako watu 10 wameshaliwa na mamba lakini waliolipwa fidia ni watatu pekee.

“Maisha ya binadamu yanapotea kwa mamba walioko katika mto, nimemsikiliza waziri hakuzungumzia jinsi gani ya kupunguza mamba kule Mto Ruvuma hili halikubaliki, tumepoteza watu 10 na wengine 30 wamejeruhiwa,” amesema.

Amesema katika jimbo lake kuna watu wamepoteza maisha yao lakini wizara haijatoa rambirambi.

“Tembo wamekuwa kikwazo ndani ya jimbo langu ndani ya mwaka huu wameshambulia ekari 460 za mazao lakini hadi nazungumza ni ekari 11 tu za watu watatu ndio wamelipwa fidia, hii tunafanya mchezo na maisha ya binadamu. Watu hao mazao ndiyo maisha yao,” amesema.

Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka amesema katika mwaka 2023 Wizara ya Maliasili na Utalii inaonyesha imevuna nyani 10 tu wakati akielekea Tabora njiani anaweza kukutana na nyani zaidi ya 100 wakivizia mahindi na mazao mengine.

“Kwa kuvuna nyani 10 sijajua vizuri lakini viboko 28 tu kuvuna ni kidogo sana mimi nina tatizo kubwa sana la viboko. Kule tuna bwawa la Igombe, nimeshazungumza na wizara tuangalie namna gani ya kuwavuna wale viboko kwa sababu watu wengi wanauawa,” amesema.

Aliwataka kuzidisha uvunaji wa wanyamapori na kuwapeleka katika mbuga nyingine ambazo hazina wanyama wengi.

Pia alipendekeza kuwekwa uzio katika shoroba kuzuia tembo kuvuka na kuingia kwenye maeneo ya makazi ya watu kwa sababu wanyama hao lazima wapite katika maeneo hayo.

Mbunge wa Serengeti, Dk Jeremiah Mrimi amesema Wizara ya Maliasili na Utalii ichukue kazi ya kudhibiti wanyama badala ya kuziachia halmashauri kazi hiyo kwa kuwa hazina fedha za kutatua changamoto hiyo.

“Watu wa Tamisemi (Ofisi ya Rais Tawala za Mikao na Serikali za Mitaa) waachiwe jukumu lake la kuhudumia watu na ofisa wanyamapori wa wilaya arudishwe chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na awezeshwe fedha kwa ajili ya kuhakikisha wanyama wanapoingia kwenye makazi ya watu wanadhibitiwa,” alisema.

Wabunge wengine waliochangia hoja hiyo ni Mwita Getere (Bunda Vijijini) Daimu Mpakate (Tunduru Kusini), Dk Christine Ishengoma (Viti Maalum), Cecilia Pareso (Viti Maalumu) na Cosato Chumi (Mafinga Mjini).

Related Posts