Dar es Salaam. Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wametakiwa kutosubiri kuajiriwa serikalini au katika sekta binafsi, bali watafute namna ya kutumia ujuzi walioupata katika masomo yao kujipatia kipato.
Hayo yameelezwa jana Ijumaa Mei 31, 2024 na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye wakati wa mahafali ya 54 duru ya kwanza ya chuo hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City.
“Elimu mliyoipata ni lazima ilete faida kwa Watanzania kama alivyosema Mwalimu Julius Nyerere kuwa fedha zinazotumika ni nyingi kuliko uwezo wetu, kuwasomesha watu wachache ili na wao baadaye walete faida kubwa kiasi hicho hicho katika nchi,” amesema Profesa Anangisye.
Aidha, wahitimu hao wametakiwa kuzingatia maadili na utamaduni wa Kiafrika na kutumia ujana kwa faida kwani Watanzania wanatarajia mambo mengi kutoka kwao kwa kuwa hakuna asiyetambua mchango wa kijana katika kuliendeleza Taifa.
Awali Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Balozi Mwanaidi Maajar, amesema baraza hilo limejikita katika kusimamia kushuka kwa ushindani kikanda na kimataifa.
“Baraza limeendelea kutoa angalizo kwa chuo hasa wakati wa uendelezaji wa miradi mbalimbali, kuhakikisha kuwa haiathiri jukumu la msingi la chuo ambalo ni kutoa elimu na huduma kwa jamii,” amesema Maajar.
Sambamba na hilo Mwenyekiti huyo amesema Baraza liliidhinisha mapitio ya sera ya chuo hicho ili kukabiliana na mazingira ya uwekezaji na mabadiliko hayo.
Mahafali hayo yamehudhuriwa na Mkuu wa Chuo hicho, Rais mstaafu Jakaya Kikwete ambapo jumla ya wahitimu 470 wamehitimu katika kozi mbalimbali.