WALIMU SEKONDARI FUNDISHENI KIINGEREZA KWA UMAHIRI-Dkt. Msonde

Na. James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amewataka walimu wa shule za Sekondari nchini kufundisha wanafunzi lugha ya kiingereza kwa umahiri ili kuwawezesha kupata ufaulu mzuri katika masomo yote ya mtihani wa kidato cha nne, ikizingatiwa kuwa kiingereza ndio lugha rasmi ya kufundishia.

Dkt. Msonde ametoa wito huo kwa walimu wote wa sekondari nchini, wakati wa vikao kazi vyake na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri za Wilaya ya Misenyi na Karagwe.

“Walimu zingatieni kufundisha kiingereza kwani wanafunzi wakiwa na umahiri wa kuongea, kusoma na kuandika lugha ya kiingereza watapa ufaulu mzuri katika mtihani wa kidato cha nne, na hakutakuwa na divisheni ziro,” Dkt. Msonde amesisitiza.

Dkt. Msonde amesema, hivisasa walimu wanapaswa kuwa vitani katika kuleta mapinduzi ya elimu nchini hivyo ufundishaji wa mazoea hauna nafasi katika kipindi hiki cha utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita ambayo ina dhamira ya dhati ya kuboresha elimu kwa masilahi na manufaa ya taifa.

“Haiwezekani mtoto afundishwe na mwalimu kiingereza mwaka mzima alafu ashindwe hata kutamka neno la kiingereza uncle, kamwe haiwezekani na ndio maana walimu mnapaswa kuingia vitani ili kutatua changamoto hii ya lugha ya kiingereza,” Dkt. Msonde amesisitiza.

Dkt. Msonde ameongeza kuwa, katika elimu ya Sekondari lugha rasmi ya kufundishia ni kiingereza hivyo walimu wanapaswa kuitumia lugha hiyo kuwafundisha watoto mpaka waelewe, kwani mkakati wa kuboresha elimu umemlenga mtoto ili apate ujuzi kama ulivyoanishwa kwenye mtaala.

Dkt. Msonde amehitimisha siku ya tatu ya ziara yake mkoani Kagera kwa kufanya vikao kazi na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi na Karagwe ambapo amehimiza uwajibikaji kwa maafisa hao.

Related Posts