Wawakilishi wacharuka utalii kupewa fedha kidogo

Unguja. Wakati Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, ikiainisha vipaumbele vinane katika mwaka wa fedha 2024/25, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameonyesha wasiwasi,  kutokana na upatikanaji wa fedha kidogo katika bajeti ya mwaka unaoisha wa 2023/24 ilhali sekta hiyo ndiyo msingi mkuu wa mapato ya Taifa.

Katika bajeti hiyo, kwa programu zake zote nne hakuna hata moja iliyopata fedha angalau asilimia 50 jambo lililowashtua wawakilishi wakihoji utayari wa Serikali kukuza sekta hiyo.

Hayo yamebainika wakati wakichangia bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo Juni Mosi, 2024. Baraza limepitisha bajeti hiyo ya Sh47 bilioni.

Katika programu ya maendeleo ya makumbusho, Mambo ya Kale na Uhifadhi wa Mji Mkongwe,  walipangiwa Sh10 bilioni lakini hadi Machi mwaka huu wamepokea Sh963 milioni sawa na asilimia 29.

Programu ya kusimamia maendeleo ya utalii ilipangiwa Sh411 milioni, imepata Sh121.7 milioni sawa na silimia 30, huku programu ya utangazaji na uhamasishaji utalii ilipangiwa Sh890 milioni lakini imepata Sh313 milioni sawa na silimia 35.

Kwenye programu ya uendelezaji na uratibu wa utalii ilipangiwa Sh1.8 bilioni wamepata Sh885 milioni saa na asilimia 46.

Akichangia bajeti hiyo, Mwakilishi wa Chumbuni, Miraji Khamis Mussa amesema haiwezekani eneo linalotoa mapato makubwa ya Taifa lipuuzwe kiasi hicho.

Sekta ya utalii inachangia zaidi ya asilimia 30 ya uchumi wa Zanzibar.

“Hivi kweli eneo linalotupa mapato makubwa kiasi hiki tunalipuuza, sisi tunajiuliza ni utalii gani huu unatangazwa. Hivi leo pesa inayopangwa haipatikani tunategemea nini na je, utayari wetu ni upi katika sekta hii?” amehoji.

“Kama kuna eneo linatupatia fedha ni utalii, kama eneo linatupa tija twende, kipi tunakwenda kufanya, msije kutuambia kuwa tumeshiriki na mialiko wakati utalii kwetu umechukua sehemu kubwa,” ameongeza.

Mwakilishi wa Fuoni, Yussuf Hassan Iddi amesema lazima Serikali iangalie kwa jicho la tatu wizara hiyo kuipatia fedha za kutosha katika kutekeleza majukumu yake,  kwani iwapo hali ikiendelea hivyo, ipo hatari ya kuanguka kwa  sekta hiyo nyeti na muhimu.

“Hii sekta ndiyo inatupatia fedha, lazima tujue kwamba kama unataka kupewa toa, kwa hiyo lazima Serikali isione tabu kutoa fedha kuipa wizara hii itekeleze majukumu yake,” amesema.

Mwakilishi wa Malindi, Mohamed Ahmada Salum amesema mapato yanapungua lakini wameongezewa idadi ya makusanyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali pamoja na kuchangia hoja ya kushuka kwa mapato, pia aliitaka wizara kukaa na wamiliki wa hoteli katika maeneo ya Pwani kwani licha ya sheria kueleza wazi kwamba fukwe ni mali ya umma wapo baadhi wanajimilikisha.

Amesema hatua hiyo inaibua migogoro kati ya wamiliki hao na wananchi na kushindwa kufurahia maeneo hayo.

“Kuna shida ambayo hoteli zinatumia maeneo haya ya fukwe, wanajimilikisha na kuwanyima wananchi uhuru wa kufurahia. Migogoro mingi imekuwa ikiibuka, kwa hiyo wizara ikutane na wamiliki hawa vinginevyo tutaendelea kupata migogoro maana kwa sasa wapo wanaodiriki kuweka hata mabaunsa kuzuia wananchi wasipite katika maeneo hayo,” amesema.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga,  amesema Kamisheni ya Utalii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii,  imeendelea kuchukua hatua ya kuvitangaza vivutio vya utalii vya Zanzibar ndani na nje ya nchi.

Amesema jitihada hizo zimewezesha kuongezeka kwa idadi ya watalii waliongia nchini mwaka 2023 ambao katika mwaka huo walioingia waliongezeka kwa asilimia 16 kutoka watalii 548,503 mwaka 2022 hadi kufikia watalii 638,498 mwaka 2023.

Awali akiwasilisha bajeti ya wizara, Soraga ameeleza vipaumbele vinane vya wizara hiyo ambavyo wanatarajia kuvitekeleza katika bajeti ya mwaka 2024/25 ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango mkuu wa kukuza utalii wa Kisiwa cha Pemba.

Kuzindua sera ya Taifa ya makumbusho na urithi wa mambo ya kale ya mwaka 2023 na kuifanyia mapitio Sheria ya Utalii ya mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2012.

Pia kuongeza wigo wa bidhaa za utalii,  kuendelea na utekelezaji wa mradi wa kuimarisha maeneo ya kihistoria.

Kipaumbele kingine ni kufanya matengenezo ya baadhi ya nyumba zilizopo katika hali mbaya ndani ya eneo la Mji Mkongwe na kuendelea kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza katika maeneo ya kihistoria.

Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi iliishauri wizara kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato, kwa vile sekta ya utalii inazidi kuimarika kila uchao na idadi ya watalii kuongezeka maradufu.

Akisoma maoni ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti, Said Saleh Salim amesema ongezeko hilo la watalii halina budi kwenda sambamba na ongezeko la mapato katika sekta hiyo.

Pia ametaka udhibiti wa mapato hayo kwa kutumia njia mbalimbali za kielektroniki na kutumia mifumo ya Tehama kwa kuwatambua wageni wote wanaofika Zanzibar na hoteli wanazofikia.

“Hatua hii italeta ufanisi mkubwa katika kuongeza mapato katika nchi yetu kupitia sekta ya utalii,” amesema.

Related Posts