Askofu Shoo awaomba msamaha waumini wa KKKT na Watanzania

Moshi. Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dk Fredrick Shoo amewaomba msamaha waumini wa kanisa hilo na Watanzania wote aliwakosea na kuwakwaza kutokana na misimamo yake, wakati akiwa kiongozi wa kanisa hilo.

Hata hivyo,  Askofu Shoo aliyekuwa mkuu wa Kanisa kuanzia 2015 hadi 2023 hakuweka wazi misimamo anayodhani liwakwaza waumini na Watanzania.

Dk Shoo ameomba msamaha huo jana, wakati wa ibada ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza kipindi chake cha uongozi wa miaka minane wa kanisa hilo.

Ibada hiyo ilifanyika katika Usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini ya kanisa hilo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdini Babu.

Amesema yeye si malaika, hivyo kutokana na misimamo yake au uamuzi akiwa mkuu wa kanisa, huenda aliwakosea au kuwakwaza wengine, hivyo anaomba wasameheane.

“Wapendwa mimi sio malaika, huenda niliwakosea pengine kutokana na misimamo yangu na maamuzi yangu kama mkuu wa kanisa, wengine niliwakwaza kwa kushindwa kunielewa, nasema pale tulipokwaruzana au tuliposhindwa kuelewana, Mungu atusaidie ili tuweze kusameheana,” amesema Dk Shoo.

Aidha, amewashukuru waumini waliombeba kimaombi, kumshauri na kumtia moyo katika kipindi chote akiwa mkuu wa kanisa na kuwataka watumishi wengine na viongozi, kuendelea kufanya kazi ya Mungu kwa uaminifu.

“Kikubwa sasa ni kuendelea kumtumikia Mungu, tuzidi kuitambua kazi yake na kuitenda kazi kwa uaminifu, Mungu tunayemuamini ni Mungu mwaminifu siku zote ambaye ahadi zake ni za kweli kwa wale wote wanaomtumikia,” amesema Askofu Shoo.

“Ndugu zangu ninamshukuru Mungu aliyeniita katika wajibu wa kuliongoza Kanisa la KKKT kwa kipindi chote cha miaka minane, ninawashukuru pia ninyi nyote kwa kuniombea na kunitia moyo katika wajibu huo.”

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdini Babu amempongeza Dk Shoo kwa kumaliza kipindi chake cha uongozi kwa amani na kuliongoza kanisa hilo kwa utumishi mwema na ushirikiano mzuri na Serikali.

Amesema Dk Shoo ni kiongozi makini, msikivu na jasiri na katika uongozi wake alishirikiana vyema na Serikali katika shughuli za maendeleo na nyingine.

“Nimesikia hapa ukiomba msamaha, lakini baba askofu, kwa kiongozi yeyote maneno huwa ni mengi, wewe umeongoza kanisa hili lenye waumini wengi, mimi hapa nawaongoza wananchi wa mkoa huu wa Kilimanjaro tu, lakini maneno ni mengi na tunaendelea kuongoza cha msingi wananchi wako salama,” amesema Babu.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Akizungumzia uchaguzi, Dk Shoo amesema wataendelea kuhamasisha jamii ili kushiriki kikamilifu katika uboreshaji wa daftari la kudumu la mpigakura na ushiriki wa uchaguzi, wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi  Mkuu kwa kuwa ni haki yao kimsingi.

Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati ya KKKT, Dk Solomoni Masangwa amesema Tanzania mwaka huu inafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule mkuu mwakani,  hivyo kila mmoja aiweke nchi katika maombi ili chaguzi hizo zipite salama.

Hata hivyo, amesema wananchi wanapaswa kuwachagua viongozi watumishi ambao watawatumikia kwa uaminifu kwa kipindi chote cha miaka mitano ijayo na kuepuka kuwachagua viongozi kwa masilahi binafsi.

“Mwaka huu na mwaka kesho tuna uchaguzi, chagueni kwa busara, chagueni kiongozi mtumishi, kila mmoja akatimize wajibu wake kikamilifu, kwani bila shaka mmejifunza katika kipindi cha miaka mitano, sasa mkachague watakaowatumikia na si wale wenye maslahi binafsi wala wachumia tumbo,” amesema askofu huyo.

Akizungumzia uchaguzi, Mkuu wa Mkoa Babu amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan amesema uchaguzi utakuwa huru na wa haki na kuliomba Kanisa hilo kushirikiana na serikali kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika hali ya utulivu na amani bila vurugu.

“Tunayo maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa uchaguzi utakuwa huru na haki, na kinachohitajika ni kujipima kama unafaa au unaweza kuongoza na kuwatumikia wananchi, niombe kanisa tushirikiane kusiwepo na mtu wa kuharibu uchaguzi, tushiriki kwenye uchaguzi tukiwa na dhamira moja na tulinde amani yetu,” amesema Babu.

Aidha mkuu huyo wa mkoa ametumia nafasi hiyo kuliomba Kanisa kushirikiana na Serikali ya mkoa huo, kuhamasisha kampeni ya usafi wa mazingira na upandaji wa miti, ili kurudisha kijani na sifa ya Moshi kuongoza kwa usafi nchini.

Sadaka iliyotolewa kwenye shukurani hiyo, imeelekezwa kwa watoto wenye matatizo ya utindio wa ubongo ambao wanahudumiwa na dayosisi hiyo katika usharika wa Moshi mjini.

Related Posts