CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimesema Chama tawala Cha Mapinduzi (CCM), kinapaswa kijifunze kupitia anguko la chama tawala nchini Afrika Kusini (ANC), lililotokana na chama hicho kutojali matatizo ya wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Onyo hilo limetolewa leo tarehe 1 Juni 2024 na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, akizungumza na vionglzi wa chama hicho katika Mkoa wa Pwani.
Ado amesema kitendo cha ANC kutotatua changamoto ya ugumu wa maisha ya wananchi wake, kimepeleka kukosa kura za kuunda Serikali peke yake baada kuambulia asilimia zaidi ya 40, badala ya asilimia 50 inayotakiwa.
“Kinachotokea kwa ANC nchini Afrika ya Kusini kinapaswa kuwa funzo kwa CCM kuwa ukipuuza hisia za wananchi, nao watazungumza kupitia sanduku la kura.
“Kwa mara ya kwanza tangu kushika Serikali mwaka 1994, ANC imeshindwa kufikisha 50% ya kura ili kuunda serikali. Uchambuzi unaonesha hii ni ishara na matokeo ya ANC kushindwa kuwajibika kwenye masuala muhimu ya wananchi kama ukosefu wa ajira, huduma mbovu ya umeme, ufisadi na utawala mbovu.” alisema Ado na kuongeza;
“Ni dhahiri kuwa hata hapa nchini kwetu, ninaamini siku za CCM kutawala nazo zinahesabika kwa sababu kama ilivyo kwa ANC, Chama Cha Mapinduzi nacho kimepuuza kwa kiasi kikubwa hisia za Watanzania.
“Mfano, uchambuzi wetu wa Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) unaonesha kuwa zaidi ya fedha za umma, wananchi wa Tanzania kiasi cha Sh trilioni 3.14 zimepotea kwa sababu ya ubadhirifu na hakuna hatua yoyote ya maana iliyochukuliwa dhidi ya ubadhirifu huo.”
Katika hatua nyingine, Ado amesema ACT Wazalendo kinawasiliana na Asasi mbalimbali za kiraia kufungua kesi mahakamani kuhakikisha kwamba Uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa unasimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi badala ya TAMISEMI.