Dabo, Gamondi viti havikaliki | Mwanaspoti

HAKUNA kukaa! Hiyo imewakuta makocha wa Azam FC, Youssouph Dabo na Miguel Gamondi wa Yanga, katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) uliozikutanisha timu hizo na kumaliza dakika 90 bila milango kufunguka kwa kutoka suluhu.

Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, Zanzibar, makocha hao waliamua kuviacha viti vyao na kusimama kwa dakika 90 kabla ya zile za nyongeza huku wakitoa maelekezo.

Gamondi ambaye ni Kocha Mkuu wa Yanga, aliona hana sababu ya kukaa na kumwachia msaidizi wake, Moussa N’Daw, lakini Dabo alimwambia bosi wake, Bruno Ferry atulie yeye atasimamia shoo.

Bruno Ferry ambaye ni Kocha Mkuu wa Azam, imekuwa kawaida yake kutulia benchi huku msaidizi wake, Dabo ndiye huwa na jukumu kubwa la kusimama na kuelekeza katika mechi zote msimu huu.

Dabo na Gamondi muda wote wa mchezo ukiendelea, walionekana kusimama kila mmoja na eneo lake huku kwa nyakati tofauti wakilalamika kupinga baadhi ya maamuzi yaliyokuwa yakitolewa na mwamuzi, Ahmed Arajiga.

Related Posts