Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea na zoezi la ufungaji wa mita za malipo ya kabla (prepaid meters) kwenye maeneo mbalimbali ambapo hadi kufikia tarehe 31 Mei mwaka huu, jumla ya mita 150 zimefungwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Utekelezaji wa zoezi hili unatokana na agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilotoa kwa Wizara ya Maji kuanza matumizi ya teknolojia ya mita za malipo ya kabla kwa wateja ili kuboresha huduma na kupunguza changamoto za ankara kwa Wananchi.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Kaimu mkuu wa Kitengo cha TEHAMA- DAWASA, Charles Kayuza amesema kuwa lengo la kufunga mita za malipo ya maji kabla inalenga kuboresha huduma, kusaidia kupunguza changamoto za kihuduma za mara kwa mara kutoka kwa wateja na hivyo kuleta ufanisi wa huduma zitolewazo na Mamlaka.
Ameongeza kuwa teknolojia hii inasaidia kukuza mapato ya Serikali moja kwa moja na kwa Mamlaka kwa kuwa mteja atakuwa analipia huduma ya maji kwa wakati sambamba na matumizi yake.
“Hadi sasa tumefunga mita za malipo ya kabla kwa wateja wakubwa na wadogo, katika Hoteli kubwa, Taasisi za Serikali mbalimbali, Mabalozi na nyumba za viongozi wa Serikali katika Wilaya za Kinondoni na Ilala na katika Mkoa wa Pwani tumefunga katika Halmashauri ya Chalinze” alisisitiza Kayuza.